Barcelona yajitoa kwa Marc Guehi, Liverpool freshi
Muktasari:
- Guehi, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi alikuwa kwenye rada za Barca kama chaguo la kwanza katika mipango yao ya kuimarisha safu ya ulinzi.
BARCELONA ilifanya mazungumzo na wakala wa beki wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Marc Guehi, 25, ili kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini kwa sasa imesitisha mpango huo kutokana na changamoto za kifedha huku Liverpool ikionekana kuwa karibu kumpata.
Guehi, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika dirisha lijalo la majira ya kiangazi alikuwa kwenye rada za Barca kama chaguo la kwanza katika mipango yao ya kuimarisha safu ya ulinzi.
Hata hivyo, timu hiyo imesitisha mchakato kwa sababu ya mshahara mkubwa na bonasi ya usajili ambayo Guehi anaitaka ili kujiunga nao.
Mkataba wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na timu nyingi zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kutokana na hali yake hiyo ya kimkataba.
Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi Liverpool ilikuwa karibu kuipata saini yake kabla ya mchakato kufeli katika dakika za mwisho za dirisha la usajili na sasa inadaiwa kuwa na nafasi nzuri tena ya kuanzia pale ilipoishia.
Jorgen Strand Larsen
CRYSTAL Palace inataka kuingia kwenye vita kali na West Ham United ili kumsajili mshambuliaji wa Wolves na Norway, Jorgen Strand Larsen, 25, dirisha la usajili la Januari. Larsen ameonekana kuzivutia klabu kadhaa za Ligi Kuu England kutokana na uwezo wake wa kufunga licha ya timu yake kuonekana kuwa katika hali mbaya tangu kuanza kwa msimu huu. Wolves iko tayari kusikiliza ofa, lakini zile zitakazokuwa nono pekee kwa sababu bado inahitaji sana huduma yake.
Radu Dragusin
ROMA inaandaa mpango wa kumsajili beki wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Romania, Radu Dragusin, 23, kwa mkopo katika dirisha la usajili la Januari. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Italia, Roma inataka kumsajili staa huyu kwa mkopo ambao utakuwa na kipengele cha kununua moja kwa moja mwishoni mwa msimu. Dragusin amepata nafasi ndogo ya kucheza Spurs tangu ajiunge na klabu hiyo, jambo linalosababisha ahitaji kuondoka.
Bradley Barcola
LIVERPOOL imehamishia macho yake kwa winga wa Paris St-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa, Bradley Barcola, 23, baada ya Antoine Semenyo kuonyesha wazi kuwa anapendelea kujiunga na Manchester City. Barcola amekuwa akihusishwa kuondoka kutokana na kutopata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha PSG na mechi nyingi amekuwa akiingizwa akitokea benchi. Mkataba wa Barcola unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Andre Onana
KIPA wa Manchester United anayecheza kwa mkopo Trabzonspor ya Uturuki, Andre Onana, 29, ameweka wazi ana furaha katika timu yake hiyo mpya na anatamani kuendelea kusalia katika viunga hivyo. Onana, ambaye alijiunga na Trabzonspor Septemba mwaka huu, alikuwa anapitia kipindi kigumu katika kikosi cha kwanza cha Man United kiasi cha kuamua kuondoka kutafuta mahali kwingine. Hatma yake baada ya msimu huu bado haijulikani.
MarioGila
BOURNEMOUTH na Chelsea zimeingia vitani kuwania saini ya beki wa Lazio, Mario Gila, 25. Hata hivyo, Lazio haiko tayari kumwachia kirahisi na itahitaji ofa nono ili kufanya uamuzi huo jambo ambalo timu hizo zinaonekana kuwa tayari kulifanya. Chelsea inamwona kama sehemu ya mpango wao wa kuendelea kuwekeza kwa wachezaji vijana, huku Bournemouth ikimwona kama sehemu ya kuimarisha safu yao ya ulinzi.
Dayot Upamecano
REAL Madrid na PSG zinaonyesha nia ya kumsajili beki wa Bayern Munich, Dayot Upamecano, 27. Hata hivyo, Bayern haiko tayari kumwacha kwa urahisi na badala yake wanapanga kuanza mazungumzo ya mkataba mpya. Upamecano ni miongoni mwa mabeki tegemeo wa Bayern, akijulikana kwa nguvu, kasi na uwezo wa kucheza mpira wa kujenga mashambulizi kutoka nyuma.
Guglielmo Vicario
KIPA wa Tottenham Guglielmo Vicario, 29, inadaiwa kufanya makubaliano binafsi na Inter Milan inayohitaji saini yake kuelekea dirisha lijalo la majira ya baridi. Vicario amecheza mechi 14 za Ligu Kuu England msimu huu na amemaliza nne kati ya hizo bila ya kuruhusu bao. Inter inamwona kama mrithi sahihi wa muda mrefu wa Yann Sommer, hasa baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na Spurs.