Barcelona yafikia patamu ishu ya Frenkie de Jong
Muktasari:
- Awali, alikuwa analipwa takribani Euro 18 milioni kwa mwaka, lakini sasa atapokea chini ya hapo ili kusaidia klabu kupunguza mzigo wa mishahara.
BARCELONA imepiga hatua kubwa katika mazungumzo na kiungo Frenkie de Jong, 28, ambaye amekubali kuongeza mkataba hadi mwaka 2029, pamoja na kukubali kupunguziwa mshahara.
Awali, alikuwa analipwa takribani Euro 18 milioni kwa mwaka, lakini sasa atapokea chini ya hapo ili kusaidia klabu kupunguza mzigo wa mishahara.
De Jong alijiunga na Barca mwaka 2019 akitokea Ajax kwa Euro 75 milioni na hadi sasa ameendelea kuwa mchezaji tegemeo wa kikosi chao.
Kabla ya kufikiwa makubaliano hayo, awali ripoti kutoka Hispania zilifichua kwamba Barca inafikiria kumuuza staa huyu kwenda England Januari ambako timu kibao zilionyesha nia ya kumsajili.
Chelsea pamoja na Manchester City ni miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zinainyemelea huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa Uholanzi.
Changamoto ya awali iliyosababisha Barca kutaka kumuuza De Jong ni masuala ya mshahara lakini baada ya kukubali kupunguza imeonekana kuwa rahisi. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani.
Ryan Gravenberch
LIVERPOOL inaendela kufanya mazungumzo kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya kiungo wake wa kimataifa wa Uholanzi, Ryan Gravenberch mwenye umri wa miaka 23. Mkataba wa sasa wa Ryan unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, na Liverpool inapambana kumsainisha mkataba mpya kutokana na kiwango alichoonyesha akiwa katika kikosi hicho. Liverpool inataka kumsainisha mkataba mpya mapema ili kuepuka presha pale utakapokaribia kuisha.
Takefusa Kubo
ARSENAL imeonyesha nia ya kumsajili winga wa Real Sociedad na timu ya taifa ya Japan, Takefusa Kubo katika dirisha lijalo la majira ya baridi.
Kubo mwenye umri wa miaka 24, ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Sociedad na msimu huu amecheza mechi tano za michuano yote.
Mabosi wa Sociedad wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 40 milioni kwa ajili ya kumuuza.
Adam Wharton
LIVERPOOL imeambiwa kuwa haitaweza kumpata kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton, 21, katika dirisha la usajili la Januari.
Mkataba wa sasa wa Wharton unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, na Liverpool ilitamani kumsajili Januari lakini kocha wa Palace amewaambia mabosi wake kwamba anahitaji sana huduma ya fundi huyo kwa msimu huu, hivyo asiuzwe.
Patrick Bamford
STRAIKA wa zamani wa Leeds United, Patrick Bamford, 32, yupo karibu kusaini mkataba na Getafe ya La Liga katika siku chache zijazo baada ya kufikia makubaliano ya maslahi.
Bamford ambaye pia amewahi kucheza Chelsea kwa sasa ni mchezaji huru tangu mkataba wake na Leeds umalizika mwisho wa msimu uliopita.
Harry Wilson
KOCHA wa Fulham, Marco Silva, amethibitisha kuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo na timu ya taifa ya Wales, Harry Wilson, 28, atafanya mazungumzo ya kuongeza mkataba siku za hivi karibuni. Wilson alijiunga na Fulham kutoka Liverpool 2021 kwa ada ya takribani Pauni 12 milioni na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu lakini bado yupo katika mipango ya kocha Silva.
Oihan Sancet
TOTTENHAM Hotspur na Arsenal ni kati ya klabu za Ligi Kuu England zinazomfuatilia kiungo wa Athletic Bilbao, Oihan Sancet, 25, raia wa Hispania. Sancet ameonyesha ubora mkubwa hususani katika suala la kutengeneza mashambulizi jambo ambalo limezishawishi timu hizo kutoka London. Msimu uliopita alifunga mabao 10 katika mechi 34 pamoja na kutoa asisti nane.
Manor Solomon
CRYSTAL Palace imeanza mazungumzo tena kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Israeli, Manor Solomon, 26, kutoka Tottenham, katika dirisha lijalo baada ya kufeli katika dirisha lililopita la majira ya baridi. Dili hilo lilifeli katika dirisha lililopita kwa sababu Spurs ilikuwa inataka Palace ilipe mshahara wote wa staa huyo pia itoe ada ya uhamisho wa mkopo. Palace haikuwa tayari.