Erling Haaland aweka rekodi ya kipekee EPL
Muktasari:
- Baada ya kufunga dhidi ya Sunderland katika ushindi wa Manchester City wa mabao 5-3 kwenye Uwanja wa Etihad, Jumapili, Haaland sasa amefunga bao dhidi ya timu zote 25 ambazo amekutana nazo katika ligi hiyo tangu alipocheza mechi yake ya kwanza Agosti 2022.
LONDON, ENGLAND: BAO la Erling Haaland katika dakika za mwisho za ushindi wa Man City dhidi ya Sunderland hivi karibuni linamaanisha kwamba sasa amefunga dhidi ya timu zote 25 ambazo amewahi kucheza nazo Ligi Kuu England (EPL).
Baada ya kufunga dhidi ya Sunderland katika ushindi wa Manchester City wa mabao 5-3 kwenye Uwanja wa Etihad, Jumapili, Haaland sasa amefunga bao dhidi ya timu zote 25 ambazo amekutana nazo katika ligi hiyo tangu alipocheza mechi yake ya kwanza Agosti 2022.
Katika mechi zake mbili zilizotangulia dhidi ya Sunderland kwenye mashindano hayo, alimaliza bila kufunga licha ya kupiga mashuti matatu katika dakika 159 alizocheza.
Haaland huenda angekuwa na wasiwasi kwamba mfululizo wake wa kutofunga dhidi ya Sunderland ungeendelea hadi pale alipoteleza na kufunga kwenye dakika ya 81 ya mchezo. Hata hivyo, alilazimika kusubiri kujua kama bao hilo lingehesabiwa baada ya VAR kulikagua, lakini kama ilivyokuwa wiki iliyopita katika mchezo wa Dabi ya Manchester bao hilo lilikubaliwa baada ya awali kukataliwa.
Kwa kuwa hajawahi kucheza dhidi ya Hull City katika mashindano hayo, atalazimika kufunga, endapo atachaguliwa kucheza dhidi ya Tigers katika mchezo wa mwisho wa ligi kabla ya Krismasi, ambao kwa sasa umepangwa kupigwa Desemba 19 ili kufikisha rekodi ya 26/26 na kuendeleza asilimia 100 ya kutupia nyavuni.
Mchezaji mwingine pekee ambaye amecheza zaidi ya mechi moja katika Ligi Kuu England na kufunga dhidi ya kila timu aliyokutana nayo ni Harry Kane, ambapo mshambuliaji huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur ambaye sasa anacheza Bayern Munich alifunga dhidi ya wapinzani wote 32 aliokutana nao katika EPL Pia yupo karibu kufanya hivyo katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) tangu alipojiunga na Bayern Munich ambapo nahodha huyo wa England kwa sasa amefunga dhidi ya timu 21 kati ya 22 alizokutana nazo Ujerumani akishindwa kufunga dhidi ya Schalke 04 pekee katika mchezo mmoja aliocheza dhidi yao.
Kuna wachezaji wengine wanne ambao wamefunga dhidi ya kila mpinzani waliyekutana naye katika Ligi Kuu England, lakini wote wamecheza mchezo mmoja tu katika mashindano hayo; Aidan Newhouse, Gary Bull, Chris David na Josh Harrop. Hata hivyo, Haaland bado yupo mbali na rekodi ya EPL ya idadi ya jumla ya timu ambazo mchezaji amefunga dhidi yake.
Frank Lampard anashika rekodi hiyo baada ya kufunga dhidi ya timu 39 tofauti katika kipindi cha maisha yake ya soka kwenye Ligi Kuu England. Idadi hiyo ni timu moja zaidi ya Andy Cole (38) na mbili zaidi ya Jermain Defoe (37) pamoja na kinara wa muda wote wa mabao katika ligi hiyo, Alan Shearer (37).