Prime
Ruben Amorim, mgonjwa mwingine hospital ileile, wodi ileile
VIMEMALIZIKA vidole vya mwanadamu. Vichukue vya mkono wa kushoto vihesabu, halafu vichukue vya mkono wa kulia vihesabu. Ndio idadi ya makocha wa Manchester United waliopita baada ya Sir Alex Ferguson kufungasha mabegi yake pale Carrington na kuamua kuondoka zake.
Ni simulizi ya kusikitisha pale Carrington. Simulizi ya unapopita katika wodi kadhaa za hospitali. Kitanda kimoja kinaweza kuwa kimebeba watu wengi waliofariki.
Ruben Amorim ameondoka zake Old Trafford hapa katikati ya wiki. Kusema ameondoka zake ni kumuheshimu. Lakini tuseme tu amefukuzwa. Nakujumlishia hesabu za makocha walioondoka Manchester United bila ya kujali kama walikuwa wa kudumu au walikuwa kwa muda.
Alianza David Moyes, halafu Ryan Giggs, halafuLouis van Gaal, halafu Jose Mourinho, halafu Ole Gunnar Solskjaer, Michael Carrick, Ralf Rangnick, Erik ten Hag, Ruud van Nistelrooy halafu akaja rafiki yetu Amorim.
Kasoro hawa makocha wa muda, wengi wa kudumu waliweka tabasamu katika sura za mashabiki wa Manchester United. Hata huyu anayeondoka aliwaacha mashabiki wa Manchester United wakitembea vifua wazi akiwa hata kabla hajakanyaga viwanja vya mazoezi vya Carrington.
Amorim alikuwa ametangazwa kuwa kocha mpya wa Manchester United wakati akiwa bado na Sporting Lisbon. Halafu likaja pambano la ligi ya mabingwa kati ya Sporting Lisbon dhidi ya Manchester City. Watani wa Manchester United ndugu zetu City wakafa mbao 4-1. Victor Gyokeres akiondoka uwanjani na Hat Trick.
United wakaamini wamepata kocha. Leo ameondoka klabunbi huku mashabiki wakiwa wanasonya. Tangu amekuja hadi anaondoka hawajawahi kumuelewa yeye wala timu yao. Sio kocha yule ambaye walimshangilia wakati anakuja kuisuka Manchester United.
Na mpaka sasa mashabiki wa Manchester United wanashindwa kuelewa. Tatizo ni nini katika klabu yao. Nakutana na mashabiki wengi wa Manchester United ambao wananiuliza tatizo lao la timu yao ni nini. Ni uongozi? Mashabiki? Makocha wanaokuja na kuondoka? Au wao mashabiki wenyewe. Binafsi sielewi.
Mfano tu majuzi wakati Amorim anaondoka. Nimecheka. Siku moja kabla hajafukuzwa, nadhani huku akijua kwamba anakaribia kufukuzwa alisikika akidai kwamba aliamini anakuja Manchester United kuwa Meneja na sio kocha.
Kuna tofauti kati ya kocha na meneja. Kocha anasimamia zaidi timu uwanjani. Kuanzia katika mazoezi na katika mechi lakini hauhusiki na mambo mengi ambayo yanaendelea katika usimamizi wa mambo kama vile uhamisho wa wachezaji, kupanga maskauti, na mambo mengine.
Najiuliza ilikuwaje akaja kutuambia suala hilo juzi wakati mkataba wake upo wazi. Kwanini hakujadiliana na mabosi wa Manchester United wakati anasaini mkataba nao? Kuna mambo mengi ambayo huwa yanajadiliwa wakati wa mazungumzo ya mkataba kwa wenzetu kule wazungu.
Kama Amorim alikuwa anaona vipengele vya mkataba havifuatwi kwanini alisema hilo wakati maji yakiwa ya shingo? Kwanini alisema hilo wakati Wolves, moja kati ya timu mbovu katika ligi kuu ya England msimu huu ikivuna pointi yake ya tatu ya msimu Old Trafford?
Manchester United haieleweki tangu Sir Alex Ferguson aondoke. kuna mambo mawili tu ambayo mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakijivunia kwa sasa. Jambo la kwanza ni kwamba timu yao imekuwa ikisogea katika fainali mbalimbali. Huyu huyu Amorim aliipeleka United katika fainali za Europa. Hata hivyo wanajivunia hilo huku wakijua kwamba Manchester United yao sio ile ambayo wanaifahamu.
Ni vile tu wanatumia jambo hilo kama ngao ya kuwakoga baadhi ya mashabiki wa timu nyingine kama Arsenal lakini hata wao wenyewe wanajua kwamba kwa kandanda uwanjani Arsenal wapo mbali kuliko wao na kwa kiwango wanachoonyesha hata wao wenyewe wanatamani wangekuwa Arsenal.
Kitu kingine ambacho kinawapa furaha mashabiki wa Manchester United ni nyakati kama hizi zinapowadia. Anapofukuzwa kocha aliyepo wanaamini kwamba labda kocha ajaye anaweza kuwa na mwanzo mpya ambao utairudisha timu yao katika zama za Sir Alex.
Kama walivyoamini kwa Amorim basi wamewahi kuamini kwamba makocha wengi waliopita kwamba timu inahitaji Pep Guardiola wao, au Jurgen Klopp wao, au Mikel Arteta wao. Bahati mbaya kwao ni kwamba kila wanapoweka kidole huwa wanaungua.
Zaidi ya kuungua, United hawaelewi tatizo ni nini? Fikiria kwamba kuna hata mashabiki ambao wanaamini kwamba ni jambo zuri kwa Ole Gunnar Solskajer kurudishwa kama kocha wa muda katika kikosi chao. Ole huyu huyu ambaye alifukuzwa na akashangiliwa. Ole huyu huyu ambaye amefukuzwa kule Besiktas ya Uturuki.
Kama tatizo ni wachezaji, United imesajili wachezaji wengi wazuri tangu Sir Alex aondoke. United imewahi kuvunja hata rekodi ya uhamisho wa dunia wakati alipomnunua Paul Pogba katika utawala wa Jose Mourinho. Hesabu wachezaji wakali ambao walikuja Manchester United baada ya kuondoka kwa Sir Alex.
Akina Angel Di Maria, Ramadel Falcao, Juan Mata,Victor Valdes, Ander Herrera, Bastian Schweinsteiger, Memphis Depay, Zlatan Ibrahimovic, Henrikh Mkhitaryan, Romelu Lukaku, Alexis Sanchez, Fred, Bruno Fernades, Casemiro na wengineo kibao ambao walikotoka walikuwa wanatamba.
Mchezaji ambaye ameendelea kuwa na ubora ule ule wa huko alikotoka na ambaye anacheza katika kiwango cha Manchester United ni Bruno Fernandes tu. tunaweza kumsamehe Cristiano Ronaldo ambaye walirudi wakati umri ulikuwa umesogea lakini hata hivyo alionyesha makali yake kuliko hata vijana ambao walipaswa kuwa juu yake kwa wakati huo.
Amorim ameendelea kuwa katika simulizi ile ile ya kitanda cha hospitali ile ile ambacho kimeshindwa kumtibu mgonjwa. Tusubiri nani atakuwa kocha mkuu na kama ataweza kuitibu Manchester United. Kwa sasa Manchester United imeendelea kuwa ile ile tu. Amorim amekuwa wa 10 katika orodha ya kitanda kilekile.