Balotelli atangaza kurudi kwenye soka
Muktasari:
- Staa huyo, aliyewahi kuzichezea pia Manchester City na Liverpool, amekuwa hana mkataba tangu alipoachwa na Genoa kwenye dirisha lililopita. Kwa sasa amekuwa akihusishwa na timu nyingi za nje ya Ulaya.
MILAN, ITALIA: STRAIKA wa zamani wa AC Milan na Inter Milan, Mario Balotelli amesema yupo tayari kurejea kwenye soka.
Staa huyo, aliyewahi kuzichezea pia Manchester City na Liverpool, amekuwa hana mkataba tangu alipoachwa na Genoa kwenye dirisha lililopita. Kwa sasa amekuwa akihusishwa na timu nyingi za nje ya Ulaya.
Alipozungumza kwenye tamasha la Trento Sports Festival, fowadi huyo wa zamani wa Italia amesema: "Nimetulia kidogo. Nimekuwa nikifanya mazoezi mwenyewe mara kadhaa kwa wiki, najiona nipo kwenye hali nzuri kabisa. Nina ofa za kutoka nje ya Ulaya, lakini natumai nitapata timu hapa Italia.
"Nimekuwa na ofa kadhaa sasa, lakini bado sijafanya uamuzi kama nisaini sasa hivi au nisubiri dirisha la Januari litakapofunguliwa."
Balotelli aliongeza: "Kwangu mimi, timu ya taifa ni kitu muhimu. Sio shambulio kwa yeyote, lakini nawaona wachezaji wanapoichezea timu ya taifa hawana dhamira, hawaipiganii jezi ya nchi na hivyo vitu havinifurahishi.
"Nilipokuwa naichezea timu ya taifa, nilijivunia kuiwakilisha Italia, kitu ambacho kwa sasa nakimisi sana. Nilikuwa mshambuliaji wa kati wa mwisho kucheza Kombe la Dunia? Ndiyo, wameniambia hilo."