Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bale akaribia kuinunua Sevilla

Muktasari:

  • Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid anatajwa kuwa kiongozi wa mojawapo ya makundi yanayofikiria kuinunua klabu hiyo yenye maskani yake Nervion, ambayo bado ipo sokoni baada ya mpango wa kuinunuliwa ulioongozwa na Sergio Ramos kuvunjika miezi michache iliyopita.

SEVILLA, HISPANIA: STAA wa zamani wa kimataifa wa Wales na Tottenham Hotspur, Gareth Bale anashauriana na mojawapo ya makundi ya wawekezaji wanaotaka kuinunua Klabu ya Sevilla, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la El Confidencial.

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid anatajwa kuwa kiongozi wa mojawapo ya makundi yanayofikiria kuinunua klabu hiyo yenye maskani yake Nervion, ambayo bado ipo sokoni baada ya mpango wa kuinunuliwa ulioongozwa na Sergio Ramos kuvunjika miezi michache iliyopita.

Taarifa hiyo pia inadai Bale amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Sevilla HD Ventures, kampuni inayomilikiwa na ndugu wawili raia wa Saudi Arabia, Mansoor na Haider Syed. Mauzo ya hivi karibuni ya asilimia 42 ya hisa za Klabu ya Valencia kwa kundi la wawekezaji kutoka Marekani, Pitchwise Holdings, yamechochea wafanyabiashara wengine kuanza kuchunguza uwezekano wa kununua klabu nyingine kongwe ya Hispania, inayotumia Uwanja wa Ramon Sanchez-Pizjuan kama maskani yake.

Kundi jingine linalotaka kuinunua Sevilla ni lile linaloitwa Third Way, mpango uliowasilishwa na wafanyabiashara wanaotoka mjini Seville, Federico Quintero na Antonio Lappi. Kundi hilo ndilo pekee ambalo hadi sasa limewasilisha ofa rasmi ya kuinunua klabu hiyo na bado halijakata tamaa katika jitihada zake za kupata udhibiti wa Sevilla.

Bila kujali matokeo ya mchakato huo, klabu hiyo ya Nervion inahitaji kwa haraka kuongezewa mtaji ili kurekebisha hali yake ya kifedha, ambayo bado ni tete. Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, Sevilla imekusanya deni la karibu Dola 200 milioni, huku hasara za kifedha zikiendelea pia katika msimu wa 2025/26, ambapo ilirekodi nakisi ya Dola 31.8 milioni.

Hata hatua kubwa za kufanya marekebisho katika kikosi cha kwanza na muundo mzima wa uendeshaji wa klabu hiyo hazijafanikiwa kuifikisha Sevilla katika kiwango kilichokusudiwa cha uwiano wa kifedha, ambapo mapato yanalingana na matumizi. Hivyo, yeyote atakayefanikiwa kuinunua klabu hiyo atalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha ili kupata hisa nyingi na kudhibiti klabu, kabla ya kuingiza angalau Dola 93 milioni kwa ajili ya kuiimarisha kifedha.