Mfalme wa Ligi Kuu Marekani ni huyu!
Muktasari:
- Kwa sasa nyota hao walioacha majina yao kwenye mbao za mafanikio Ligi Kuu Hispania wanakipiga katika ligi hiyo kwenye timu tofauti Messi akiwa Inter Miami, Lewandowski akiichezea Chicago Fire huku Griezmann akiitumikia Orlando City.
WASHINGTON, MAREKANI: HATUA ya mtoano ya Ligi Kuu Marekani (MLS) inaanza keshokutwa, Alhamisi, Novemba 19, 2026, usiku wa manane ambayo ni Ijumaa alfajiri, Novemba 20, 2026 kwa saa za Afrika Mashariki na mashindano hayo yatafunguliwa kwa mechi za mchujo wa awali kati ya timu zilizomaliza nafasi ya nane na tisa katika kila kanda.
Hata hivyo wakati MLS ikiingia katika hatua muhimu ya uamuzi, ligi hiyo inatarajiwa kushuhudia vita ya ufalme ikiamriwa na mastaa waliowahi kucheza Barcelona, kwa nyakati tofauti, ambao ni Lionel Messi, Robert Lewandowski na Antoine Griezmann.
Kwa sasa nyota hao walioacha majina yao kwenye mbao za mafanikio Ligi Kuu Hispania wanakipiga katika ligi hiyo kwenye timu tofauti Messi akiwa Inter Miami, Lewandowski akiichezea Chicago Fire huku Griezmann akiitumikia Orlando City.
Ukuaji unaoendelea wa MLS umeendelea kuvutia mastaa wengi wa soka kutoka maeneo mbalimbali duniani kila mwaka na wamejazana nyota wanaokipiga katika ligi na nchi kubwa kisoka duniani na katika utabiri uliotolewa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani unaonyesha kuna uwezekano wa Messi, Lewandowski au Griezmann mmojawao kutwaa ubingwa wa hatua ya mtoano ya ligi hiyo.
Kwa kuzingatia viwango vyao katika msimu huu, mwenendo wa matokeo na mambo mengine yanayoweza kuathiri mafanikio yao baada ya kukamilika kwa siku ya mwisho ya michezo ya msimu wa kawaida (Decision Day), wote watatu walifanikiwa kufuzu hatua ya mtoano ya Kanda ya Mashariki.
Hata hivyo, ni mmoja tu atakayeweza kutwaa ubingwa wa kanda hiyo na kusonga mbele hadi fainali ya Kombe la MLS.
MESSI (INTER MIAMI)
Kwa mujibu wa tathmini, Messi ndiye anayeonyesha zaidi kutetea taji na kuwa bingwa wa Kombe la MLS kwa misimu miwili mfululizo akipewa asilimia 60. Ingawa kikosi cha Inter Miami, kinachojulikana kwa jina la utani la ‘Herons’, kimekuwa kikionyesha kutokuwa na matokeo ya kuridhisha katika baadhi ya nyakati, kimeendelea kuwa imara katika kipindi chote cha msimu na kumaliza nafasi ya pili kwenye Kanda ya Mashariki, nyuma ya Nashville iliyofanya vizuri.
Utabiri unaoipa nafasi Inter Miami kuchomoza mabingwa unachagizwa na nafasi ya nyota huyo wa Argentina katika soka la Marekani na timu hiyo inavyoweza kuzichanga karata katika hatua hii.
“Faida yao kubwa ya ushindani inatokana na uzoefu wa kucheza hatua za mtoano, muunganiko mzuri uliojengeka ndani ya kikosi cha Miami na faida ya kucheza nyumbani katika hatua muhimu. Mambo hayo yanaifanya Inter Miami kuwa timu yenye uwezekano mkubwa zaidi wa kufika fainali ya Kombe la MLS,” inalezwa na muungano wa vyombo vya habari vya michezo nchini humo.
LEWANDOWSKI (CHICAGO FIRE)
Katika nafasi ya pili ni mshambuliaji wa zamani wa Bayern Munich, Robert Lewand owski, ambapo nyota huyo wa Poland amekuwa mhimili mkuu wa kikosi hicho cha Illinois kutokana na mfululizo wake mzuri wa kufunga mabao. Hadi sasa ametupia nyavuni mabao tisa na asisti nne katika mechi 19 alizocheza akipewa asilimia 30 ya kunyanyua kombe msimu huu wake wa kwanza kucheza katika ligi hiyo.
Hata hivyo, udhaifu wa safu ya ulinzi wa kikosi hicho unaweza kuigharimu timu hiyo katika hatua ya mtoano, ambako hata Lewandowski hawezi kufanya kila kitu peke yake. “Timu hiyo imeonyesha kutokuwa na uimara wa kiulinzi katika michezo ya mwisho ya msimu.
Itategemea Lewandowski kuendelea kuwa katika kiwango cha juu cha ufungaji mabao ili kuzishinda timu zenye vikosi imara na wachezaji wengi wenye uwezo katika hatua za baadaye,” inalezwa na muungano huyo.
GRIEZMANN (ORLANDO CITY)
Ingawa Mfaransa huyo pia amevutia tangu alipowasili Marekani, akiwa amefunga mabao 14 katika mechi 18 alizocheza, ukweli ni kwamba kikosi chake hakina wachezaji wengi wenye uwezo wa kutosha kama ilivyo kwa timu nyingine zinazowania ubingwa. Hata hivyo anapewa asilimia 10 za kutwaa ubingwa wa Kanda ya Mashariki ya MLS.
Aidha, nafasi yao katika msimamo wa ligi inamaanisha wanapaswa kucheza mechi moja ya ziada ikilinganishwa na timu hizo mbili zilizotajwa hapo juu, jambo linalopunguza zaidi nafasi ya kutwaa taji hilo.
“Nafasi yao ya kutwaa ubingwa wa Kanda ya Mashariki ni ndogo zaidi kutokana na njia wanayopaswa kupitia. Orlando itaanzia hatua ya awali, ikiwa na changamoto ya kucheza ugenini dhidi ya timu zilizomaliza katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
Ingawa ubora binafsi wa Griezmann unaweza kuamua matokeo ya mchezo wowote, ratiba ngumu ya michezo na uchovu wa kimwili vinaifanya timu hiyo kuwa na nafasi ndogo zaidi ikilinganishwa na nafasi ya Messi kutwaa ubingwa au mwenendo mzuri wa Chicago,” unaeleza muungano huo wa vyombo vya habari.
Kana kwamba changamoto hizo hazitoshi, timu zote tatu zinazowania taji hilo zinapaswa pia kukabiliana na kikwazo kingine cha pamoja. Hiyo ni Nashville ambayo pia inashiriki Kanda ya Mashariki na ambayo kila timu italazimika kuifunga ili kufanikisha malengo yake.
Baada ya kuweka rekodi mpya ya pointi nyingi zaidi katika historia ya klabu hiyo, kikosi hicho kimetoa ujumbe mzito kwa wapinzani wote kiliokutana nao.
Kwa sasa, Nashville inaonekana kuwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kukamilisha mafanikio makubwa ya kihistoria kwa kutwaa mataji mawili katika msimu mmoja, Kombe la MLS na Ngao ya Wafuasi (Supporters’ Shield).