Pochettino achimba mkwara Man United
Muktasari:
- Chini ya Michael Carrick, wachezaji walikuwa wakipumzika siku inayofuata baada ya mechi, lakini Pochettino anataka wote wafike uwanjani kwa ajili ya mazoezi ya kurejesha nguvu za mwili.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA mpya wa Manchester United, Mauricio Pochettino anataka kubadili utaratibu wa mazoezi kwa wachezaji wa timu hiyo kwa kufuta mapumziko ya siku moja baada ya mechi na kuwataka kuripoti Carrington kwa mazoezi ya kurejesha nguvu za mwili.
Chini ya Michael Carrick, wachezaji walikuwa wakipumzika siku inayofuata baada ya mechi, lakini Pochettino anataka wote wafike uwanjani kwa ajili ya mazoezi ya kurejesha nguvu za mwili.
Sababu ni takwimu za United, ambayo ipo nafasi ya 19 kwenye Ligi Kuu England kwa umbali wa kukimbia uwanjani na nafasi ya 17 kwa kasi ya kukimbia kwa nguvu.
Pochettino atakuja na mwanawe, Sebastiano Pochettino, ambaye atahusika na masuala ya utimamu wa mwili na sayansi ya michezo.
Wakati huo huo, aliyekuwa mshambuliaji wa England, Gary Lineker ametabiri kuwa Pochettino hatadumu kwa muda mrefu Manchester United.
Lineker amesema United ni klabu kubwa kwa jina, lakini anaamini kocha huyo ataanza vizuri kabla mambo hayajaharibika na hatimaye kufutwa kazi.
“United ni klabu kubwa kwa Pochettino, kubwa kwa jina tu. Ataanza vizuri, halafu mambo yataharibika na atafukuzwa. Nitashangaa kama bado atakuwepo baada ya miezi 18,” amesema Lineker.
Hata hivyo, Pochettino anaondoka Marekani akiwa na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Haiti katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mataifa ya Amerika Kaskazini, uliofanyika Miami.
Ushindi huo umekuwa zawadi ya kuaga kwa kocha huyo kutoka kwa wachezaji wa Marekani kabla ya mchezo wa marudiano dhidi ya Haiti utakaochezwa Jumanne, Novemba 18, jijini Cincinnati.
Pochettino amesema kuondoka Marekani na kukubali kazi ya Manchester United haukuwa uamuzi rahisi, akieleza kuwa hakutarajia kurejea Ligi Kuu England baada ya kusaini mkataba mpya na timu hiyo ya taifa hadi mwaka 2030 mwezi Agosti.
“Kuchukua kazi ya Manchester United ni uamuzi mgumu zaidi maishani mwangu. Kufundisha Marekani ni heshima kubwa sana, lakini klabu kama United ikikuita, huwezi kukataa,” amesema Pochettino, ambaye alionyesha hisia wakati wa kuwaaga wachezaji na viongozi wa Marekani.
Kocha huyo anatarajiwa kuanza kazi United na watu watano wa benchi lake la ufundi, ambao ni Jesus Perez na Miguel D'Agostino, wasaidizi wake, Toni Jimenez, kocha wa makipa, Sebastiano Pochettino, mtaalamu wa utimamu wa mwili, na Silvia Tuya, mtaalamu wa sayansi ya michezo na nguvu.
Tuya, raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 46, anatarajiwa kuwa mwanamke wa kwanza kuhudumu kwenye benchi la timu ya kwanza ya wanaume ya Manchester United.
Kwa upande wa usajili wa Januari, Pochettino amekataa wazo la kumsajili beki wa kulia wa Chelsea, Malo Gusto, licha ya kufanya naye kazi Stamford Bridge na kumtumia katika michezo 37.
Vipaumbele vyake ni beki wa kati, mshambuliaji na beki wa kushoto. United pia inamtaka Nico Paz wa Como, ambaye anaweza kusajiliwa katika dirisha la majira ya kiangazi.
Uongozi wa United unatarajiwa kumpa Pochettino fedha za kuimarisha safu ya ulinzi katika dirisha la usajili la Januari.
Pochettino anatarajiwa kumaliza majukumu yake na Marekani Jumanne, Novemba 18, kisha kuanza mazoezi Carrington Alhamisi, Novemba 19, kabla ya kuiongoza United katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Liverpool, Novemba 22, kwenye uwanja wa Anfield.
Rekodi yake dhidi ya Liverpool si nzuri. Katika michezo 19 aliyokutana nao, ameshinda mara tatu, ametoka sare mara tano na kupoteza mara 11.