Badiashile pasua kichwa, Napoli ikiongeza mzigo
Muktasari:
- Chelsea inadaiwa kutaka kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi msimu huu wa kiangazi, ambapo Trevoh Chalobah amejiunga na Como, huku Maxence Lacroix akijiunga na Chelsea akitokea Crystal Palace.
NAPOLI inadaiwa kwamba imeongeza fungu la pesa ili kumsajili beki wa kati wa Chelsea, Benoit Badiashile, ambapo mazungumzo yanaelekea ukingoni kati ya klabu hizo pamoja na wawakilishi wa mchezaji huyo.
Chelsea inadaiwa kutaka kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi msimu huu wa kiangazi, ambapo Trevoh Chalobah amejiunga na Como, huku Maxence Lacroix akijiunga na Chelsea akitokea Crystal Palace.
Levi Colwill, Tosin, Wesley Fofana na Lacroix wanatarajiwa kuwa mabeki wa kwanza wa kati wa Chelsea msimu huu. Hata hivyo, bado haijafahamika iwapo Axel Disasi, Mamadou Sarr na Aaron Anselmino wataondoka Stamford Bridge.
Kinachoelezwa ni kwamba kuwapo kwa mastaa wengi katika kikosi hicho kumewaibua baadhi kutaka kuondoka. Vyovyote ilivyo, Badiashile lazima asepe.
Tijjani Reijnders
KIUNGO wa kimataifa wa Uholanzi na Manchester City, Tijjani Reijnders huenda akakamilisha dili lake la kutua Al Qadsiah ya Saudi Arabia kwa Pauni 61 milioni. Reijnders, mwenye umri wa miaka 28 alisajiliwa na City kutoka AC Milan msimu uliopita kwa ada ya Pauni 46 milioni.
Harry Kane
KWA mara nyingine Barcelona inadaiwa kuulizia Bayern Munich kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa England, Harry Kane, mwenye umri wa miaka 33, katika dirisha hili la uhamisho wa kiangazi. Hata hivyo, Bayern inadaiwa kwamba imeshaeleza haitamuachia straika huyo msimu huu, lakini mabingwa hao wa LaLiga wanadaiwa kukomaa wakiitaka saini yake.
Ayyoub Bouaddi
MANCHESTER City na Manchester United zinadaiwa kupimana ubavu kuitaka saini ya Ayyoub Bouaddi mwenye umri wa miaka 18 kutoka Lille. Inadaiwa kwamba kiungo huyo wa kimataifa wa Morocco anayethaminishwa kwa Pauni 85 milioni ameshaitaarifu Lille juu ya kutaka kuondoka kwake katika dirisha hili la usajili.
Bradley Barcola
BRADLEY Barcola, mwenye umri wa miaka 23, amekubali kujiunga na Liverpool, lakini dili hilo linaweza kusitishwa iwapo PSG haitapata mbadala wake haraka. Arsenal nayo imefanya jaribio la kumsajili mshambuliaji huyo wa Ufaransa ambaye thamani yake inadaiwa kuwa Pauni 130 milioni.
Gabriel Martinelli
AS Roma imefanya mazungumzo ya awali na wawakilishi wa Gabriel Martinelli, huku ikichunguza uwezekano wa kumsajili winga huyo wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil mwenye umri wa miaka 25. Martinelli bado anapenda kuitumikia Arsenal msimu ujao, lakini lolote linaweza kutokea.
Joao Felix
MSHAMBULIAJi wa Al Nassr na Ureno, Joao Felix anadaiwa kuanza kufikiria kuondoka Saudi Arabia ambako alikuwa na msimu bora uliopita. Hata hivyo, huenda nyota huyo akakumbana na wakati mgumu kupata timu kubwa Ulaya kwani nyingi zimekuwa zikimkwepa kwa miaka mingi kutokana na kutoingia kwake vyema kwenye mfumo alikocheza.
Alessandro Bastoni
BEKI wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Alessandro Bastoni, mwenye umri wa miaka 27, anadaiwa kutakiwa Real Madrid na huenda lolote likatokea kuanzia sasa hadi mwishoni mwa wiki ijayo. Real Madrid inapambana kuweka sawa mambo katika eneo la ukuta wake ambao msimu uliopita uliruhusu mabao mengi.
Martin Zubimendi
REAL Madrid inavutiwa kumsajili kiungo wa kimataiafa wa Hispania aliyeshinda Kombe la Dunia 2026, Martin Zubimendi, mwenye umri wa miaka 25, kutoka Arsenal. Kwa sasa pande hizo zinaendelea na mazungumzo ili kufikia muafaka.
Joao Palhinha
JOAO Palhinha yupo tayari kuhamia Aston Villa kwa mkopo kutoka Bayern Munich, kwa mujibu wa The Sun, ambapo kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 alicheza kwa mkopo Tottenham Hotspur msimu uliopita, huku Newcastle United pia ikiripotiwa kuwa inamtaka.