Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nondo tano za Aziz Ki Yanga

AZIZ KI Pict


MUDA wowote kuanzia sasa, Yanga inaweza kumtambulisha rasmi Stephane Aziz KI kurejea Jangwani, ikiwa sehemu ya mpango wa klabu hiyo kujiimarisha kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.


Aziz Ki, raia wa Burkina Faso mwenye uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji, si mgeni ndani ya Yanga. Alikuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho kabla ya kuondoka na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morocco mwaka 2025 baada ya kufanya mambo makubwa akiwa na kikosi hicho kilichomtambulisha zaidi Afrika.


Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Yanga imemrejesha fundi huyo kwa ada ya Dola 450,000 (zaidi ya Sh1.2 bilioni) huku akipewa kitita cha Dola 300,000 zaidi ya (Sh790 milioni), malipo ya kusaini kwake mkataba wa miaka miwili na timu hiyo.

Hivyo, gharama yote ya kumpata mchezaji huyo inafikia karibu dola 750,000 ambazo ni zaidi ya sh 1.9 milioni hata hivyo, mkwanja huo Yanga italipa kwa awamu kwa mchezaji na hata klabu anayotoka ya Al-Ittihad Tripoli.

Kwa klabu kutumia kiasi hicho cha fedha kumrudisha mchezaji, inaonyesha wazi kuwa Aziz KI anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Yanga huku ikielezwa kuwa anaweza kupishana na Allan Okello. Haya ndiyo mambo matano muhimu ambayo kiungo huyo ambaye ni mume halali wa Mwanamitindo Hamisa Mobetto anaweza kuyaongeza Jangwani.

MIPIRA YA ADHABU

Moja ya silaha ambazo Aziz Ki amekuwa akizitumia vizuri ni mipira iliyokufa, hasa mipira ya adhabu.

Uwezo wake wa kutumia mguu wa kushoto, kupiga mipira kwa usahihi na kutengeneza hatari akiwa nje ya eneo la hatari unaweza kuipa Yanga chaguo jingine katika mechi ambazo wapinzani wanajilinda kwa idadi kubwa.

Kwa timu inayocheza mechi nyingi za ushindani, hasa Ligi Kuu Bara na mashindano ya CAF, uwezo wa kupata bao kupitia mpira wa adhabu inaweza kuwa faida ya ziada huku ikirahisisha mipango ya timu.

Aziz Ki pia anaweza kutumika katika mipira ya kona na mipira ya pembeni, akitengeneza nafasi kwa washambuliaji na mabeki wenye uwezo wa kucheza mipira ya juu, tayari kumbukumbu zinaonyesha kuwa alishafanya mambo hayo kwa ufasaha wakati akiitumikia Yanga.

AZIZ Pict
AZIZ Pict

MABAO NA ASISTI

Hapa ndipo Aziz Ki anapokuja na rekodi inayomfanya Yanga iamue kutumia fedha nyingi kumrudisha.

Katika kipindi chake cha kwanza Jangwani, alionyesha uwezo wa kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kufunga na hata kutoa usaidizi wa mabao.

Katika msimu wake wa kwanza 2022/23, alifunga mabao tisa na kutoa asisti tatu kipindi hicho Yanga ilikuwa na Feisal Salum, msimu wa 2023/24 alikuwa moto wa kuotea mbali kufuatia kufunga mabao mabao 21 na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa ndiye mchezaji wa mwisho kufunga mabao mengi kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu Bara.

Mabao hayo yalimfanya afikie rekodi ya Amissi Tambwe, ambaye pia alifunga mabao 21 kwa Yanga msimu wa 2015/16 huku msimu wake wa mwisho 2024/25 akifunga mabao tisa kabla ya kwenda Morocco. Hizi ni namba zinazomweka Aziz Ki katika kundi la viungo wenye uwezo mkubwa wa kuamua matokeo, kuisaidia timu lakini pia kuwa na namba bora kuliko wageni wote nchini.

UBUNIFU KIUNGO

Yanga imekuwa ikihitaji wachezaji wenye uwezo wa kuvunja mistari ya wapinzani na kuunganisha kiungo na safu ya ushambuliaji.

Aziz Ki ana uwezo huo. Akiwa kiungo mshambuliaji, anaweza kucheza nyuma ya mshambuliaji, kuingia katikati kutoka upande wa kushoto au kushuka chini kuchukua mpira na kuanzisha mashambulizi.

Kwa kuwa anatumia mguu wa kushoto, uwepo wake unaweza kumpa kocha chaguo tofauti la kujenga mashambulizi, hasa dhidi ya timu zinazocheza kwa kujilinda.

Hili linaweza kuwa muhimu zaidi kwenye mechi ambazo Yanga inahitaji ubunifu kuliko nguvu kwa kuwa pia pia kiungo huyo mshambuliaji ana uwezo mkubwa wa kuhamisha mashambulizi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

UZOEFU

Aziz Ki ana uzoefu wa kucheza Ligi Kuu, mashindano ya CAF na pia amepitia mazingira ya soka la Morocco akiwa na Wydad moja ya timu kubwa barani Afrika akiwa pia alikwenda na timu hiyo kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Dunia.

Akiwa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/25, alifunga mabao manne katika mechi tisa huku katika msimu wa 2023/24 akicheza mechi 12 za Ligi ya Mabingwa na kufunga mabao mawili pamoja na kutoa asisti mbili.

Huo ni uzoefu ambao unaweza kuwa muhimu kwa Yanga katika mechi zenye presha kubwa ikumbukwe kuwa huyu ndiye aliyewafanya 2024, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kidogo waumbuke katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa alichia mkwaju ambao ulizua utata baada ya kugonga mwamba na kuingia wavuni lakini mwamuzi akasema mpira haukuvuka mstari.

Kama bao lile lingekubaliwa huenda Yanga ingetinga nusu fainali ya michuano ya mwaka huo lakini badala yake iliishia hatua hiyo kufuatia kufungwa kwa mikwaju ya penalti 3-2, baada ya mechi zote kumalizika kwa suluhu.

Zaidi ya hapo, Aziz Ki pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Burkina Faso, hivyo amekuwa katika mazingira ya ushindani wa kimataifa kwa muda mrefu akiwa mmoja kati ya wachezaji wachache ambao wameshiriki Michuano ya AFCON.

CHAGUO KIMFUMO

Mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja huwa na thamani kubwa kwa kocha.

Aziz Ki anaweza kutumika kama namba 10, kucheza kama kiungo mshambuliaji au kupewa uhuru wa kuingia katika maeneo tofauti zikiwemo winga zote mbili kulia na kushoto, lakini wakati mwingine anaweza kutumika kama namba nane. Hilo litampa kocha Manqoba Mngqithi nafasi ya kubadilisha mfumo ndani ya mchezo bila kufanya mabadiliko mengi ya wachezaji.

Kwa mfano, anaweza kuanza kama kiungo mshambuliaji katika mfumo wa 4-2-3-1, lakini wakati wa mchezo akasogea pembeni au kucheza karibu zaidi na mshambuliaji.

Kwa mchezaji ambaye ana uwezo wa kufunga, kutoa pasi za mwisho na kutumia mipira iliyokufa, uwepo wake unaweza kuongeza aina ya mashambulizi ambayo Yanga inaweza kutumia.