Baada ya straika Gyokeres, Eberechi anafuata Arsenal
Muktasari:
- Arsenal imekuwa katika harakati za kutaka kumsajili fundi huyo tangu mwanzoni mwa dirisha hili lakini hivi karibuni ilipunguza nguvu kwa sababu ya dili la Gyokeres.
BAADA ya kumpata straika wa Viktor Gyokeres, mabosi wa Arsenal sasa rasmi wamehamishia nguvu zao kwenye dili la mshambuliaji wa Crystal Palace, Eberechi Eze katika dirisha hili.
Arsenal imekuwa katika harakati za kutaka kumsajili fundi huyo tangu mwanzoni mwa dirisha hili lakini hivi karibuni ilipunguza nguvu kwa sababu ya dili la Gyokeres.
Palace inadaiwa kuhitaji zaidi ya Pauni 68 milioni kama ada ya uhamisho ya Eze mwenye umri wa miaka 27, ambaye anatamani sana kujiunga na kikosi cha Mikel Arteta.
Eze mwenyewe anaripotiwa kuichagua Arsenal na watu wa karibu na mchezaji huyo wana matumaini kuwa makubaliano yatafikiwa katika wiki chache zijazo.
Arsenal wanatarajia kukubaliana ada ya uhamisho ya jumla ya Pauni 60 milioni, badala ya kifungu cha Pauni 68 milioni kilichoripotiwa kuwa katika mkataba wake.
Ingawa bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati ya klabu hizo mbili, mapendekezo yanaonyesha kuwa Palace haina shida na ipo tayari kumuuza Eze.
Tovuti ya The Independent iliripoti awali kuwa katika Pauni 60 milioni ambazo Arsenal imepanga kutoa, itatoa kwa awamu tatu ambazo ni Pauni 20 milioni kila baada ya muda.
Mkataba wa sasa wa Eze unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 43 za michuano yote na kufunga mabao 14.
Adam Aznou
EVERTON iko kwenye mazungumzo na Bayern Munich kuhusu uhamisho wa Pauni 7.8 milioni wa beki wa kushoto wa timu hiyo na Morocco mwenye umri wa miaka 19, Adam Aznou.
Beki huyu anatamani sana kuondoka katika dirisha hili kwa sababu anataka kujiunga na timu itakayompa nafasi kubwa zaidi ya kucheza katika kikosi cha kwanza tofauti na ilivyo sasa. Katika msimu uliopita Aznou alicheza mechi 29 za michuano yote. Mkataba wake unamalizika mwaka 2027.
Gabriel Jesus
FLAMENGO ya Brazil inataka kumsajili mshambuliaji wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil, Gabriel Jesus, mwenye umri wa miaka 28 ambaye amepewa ruhusa ya kuondoka ikiwa atapata timu itakayokuwa tayari kutoa pesa na kumnunua.
Vigogo wa Flamengo wanataka sana kumsajili fundi huyu wakiamini atawasaidia sana katika michuano ya kimataifa. Mkataba wa Jesus na Arsenal unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Joao Felix
BENFICA bado ina matumaini ya kuipindua Al Nassr katika dili la kuiwania saini ya mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Ureno, Joao Felix katika dirisha hili. Taarifa zinaeleza Al Nassr ipo tayari kutoa Pauni 40 milioni kwenda Chelsea kwa ajili ya kuipata huduma ya Felix mwenye umri wa miaka 25. Mazungumzo baina ya wawakilishi wa Felix na Al Nassr pamoja na Benfica bado yanaendelea kwa sasa kwani bado staa huyo hajaamua ni timu gani atajiunge nayo hadi sasa.
Reiss Nelson
FULHAM iko katika mazungumzo ya hatua za mwisho ili kumsajili tena winga wa Arsenal mwenye umri wa miaka 25, Reiss Nelson, kwa mkopo wenye chaguo la kumnunua moja kwa moja mwisho wa msimu. Msimu uliopita, Nelson alicheza kwa mkopo Fulham na kiwango chake kilionekana kulivutia sana benchi la ufundi la Fulham. Mkataba wa Nelson unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu uliopita alicheza mechi 13 za michuano yote.
Malick Fofana
EVERTON iko kwenye mazungumzo na Olympique Lyon kuhusu dili la kumsajili winga wa timu hiyo na Ubelgiji mwenye umri wa miaka 20, Malick Fofana.
Ripoti kutoka tovuti ya L’Equipe zinafichua kwamba Everton imewasilisha ofa ya takribani Pauni 31 milioni kwenda Lyon kwa ajili ya kumpata staa huyu.
Idrissa Gueye
MANCHESTER United na Burnley zimejumuika na Brentford, Southampton na Borussia Dortmund katika vita ya kumsajili mshambuliaji wa Metz mwenye umri wa miaka 18, Idrissa Gueye katika dirisha hili. Fundi huyu wa kimataifa wa Senegal alikuwa akifuatiliwa na maskauti wa timu mbalimbali msimu uliopita. Mkataba wa sasa wa Gueye unaisha 2029.
Raheem Sterling
CHELSEA ipo tayari kutoa sehemu ya mshahara wa winga wa Manchester City na timu ya taifa ya England, Raheem Sterling ili kukamilisha uhamisho wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 kwenda Fulham katika dirisha hili. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca anadaiwa kumpa ruhusa Sterling kuondoka katika dirisha hili.