Baada ya hukumu ya Man City, Roy Keane atoa kauli
Muktasari:
- City ilitangazwa kuwa na hatia ya makosa yote yaliyohusishwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za fedha za Ligi Kuu katika taarifa iliyotolewa Jumanne.
MANCHESTER, England: NYOTA wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, amewataka wachezaji wa Manchester City kuzitupa medali zao za ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya klabu hiyo kutangazwa kuwa na hatia ya kuvunja kanuni za kifedha za mashindano hayo.
City ilitangazwa kuwa na hatia ya makosa yote yaliyohusishwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za fedha za Ligi Kuu katika taarifa iliyotolewa Jumanne.
Hata hivyo, klabu hiyo imeendelea kukataa kufanya makosa hayo na kusisitiza kuwa haina hatia.
Kwa sasa haijafahamika adhabu ambayo City itapewa, lakini miongoni mwa hatua zilizopendekezwa ni kukatwa kwa pointi nyingi au hata kushushwa daraja.
Pia, kumekuwa na madai kwamba klabu hiyo inaweza kupokonywa baadhi ya mataji iliyoandika katika kipindi kinachohusishwa na uchunguzi huo.
Katika kipindi cha uchunguzi, kuanzia mwaka 2009 hadi 2018, City ilitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu, pamoja na Kombe la FA mara mbili, Kombe la Ligi manne na Ngao ya Jamii.
Keane, ambaye alikuwa akichambua mchezo wa England dhidi ya Czech, alisema wachezaji wa City wana sababu ya kujisikia wameangushwa na uongozi wa klabu hiyo.
“Walijua jambo hili lingeumiza watu wengi, lakini bado walilifanya,” alisema Keane kupitia ITV.
“Na kama ningekuwa mchezaji aliyepata mafanikio hayo katika miaka ya karibuni, kwa asilimia 100 ningekuwa nazitupa hizo medali kwenye taka.”
Alipoulizwa na mtangazaji Mark Pougatch kama wachezaji wanaweza kujisikia wameangushwa na klabu, Keane alijibu:“Kwa asilimia 100. Ungejisikia hivyo. Ni udanganyifu. Unasikia wachezaji wa zamani wakisema walishinda uwanjani, lakini ulikuwa udanganyifu. Kulikuwa na udanganyifu unaoendelea.
“Ni jambo gumu kwa wachezaji na kocha. Una wamiliki ambao wanaonekana kuwa tayari kufanya udanganyifu.
“Itakuwa vigumu sana kwa wachezaji hawa kuendelea kudumisha kiwango hicho cha ubora.”
Mchambuzi mwenzake, Ian Wright, alielezea vitendo vinavyodaiwa kufanywa na wamiliki wa City kuwa “vibaya”, huku akisema taarifa hiyo ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa.
“Wamiliki wa City wamekuwa wakiwaambia kwamba hakuna jambo baya linaloendelea. Kama wewe ni mchezaji, lazima uhisi kuna jambo haliko sawa.
“Ni jambo ambalo halijawahi kutokea tunaloliona sasa. Lakini kuhusu wamiliki na walichokifanya, ni jambo baya,” alisema Wright.
Taarifa ya Ligi Kuu ilieleza matokeo ya uchunguzi wa tume huru, ambayo ilidai kuwa City ilificha pauni milioni 900 kupitia mikataba ya kibiashara iliyodaiwa kuwa ya kutengenezwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, City ilikiuka kwa utaratibu kanuni za Ligi Kuu kwa kipindi cha karibu muongo mmoja.
Manchester City ina hadi Oktoba 2 kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Tume ya Ligi Kuu England iliyobaini klabu hiyo kuwa na hatia katika tuhuma zinazohusiana na ukiukaji wa kanuni za kifedha.
Klabu hiyo imesema imesikitishwa na kushangazwa na uamuzi huo, ikisisitiza kuwa itaendelea kupambana na kesi hiyo kupitia njia zote za kisheria na kiudhibiti zinazopatikana.
Katika taarifa yake, City ilisema inaamini haina hatia dhidi ya tuhuma zilizowasilishwa na Ligi Kuu na kwamba ina ushahidi wa kutosha kuunga mkono msimamo wake.
“Manchester City FC imesikitishwa na kushangazwa na uamuzi wa Tume ya Ligi Kuu uliotolewa.
“Klabu haina hatia dhidi ya tuhuma zilizotolewa na Ligi Kuu na ina ushahidi mpana na usiopingika unaounga mkono msimamo wake katika suala hili.
“Kwa hiyo, klabu itaendelea kupambana kwa nguvu na, pale inapohitajika, kuchukua hatua kupitia taasisi zote zinazofaa za udhibiti na kisheria.
“Mchakato wa Ligi Kuu bado unaendelea, huku baadhi ya vipengele muhimu vikiwa havijakamilika.
“Manchester City FC sasa itatumia njia za rufaa ilizopewa, kwa msingi kwamba uamuzi huo una makosa ya wazi na ya msingi katika sheria, kanuni na ukweli, hivyo hauwezi kuwa msingi salama wa uamuzi.”
Kwa hiyo, licha ya uamuzi wa tume hiyo, suala hilo bado halijafikia mwisho wa mchakato wake wa kisheria, huku City ikijiandaa kutumia haki yake ya kukata rufaa.