Aston Villa yaikomalia Man United kwa Martinez
Muktasari:
Martinez mwenye umri wa miaka 32, aliibua tetesi za kuondoka mara baada ya msimu uliopita kumalizika ambapo alionekana akitoa ishara ya kuwaaga mashabiki wa Villa.
MABOSI wa Aston Villa wamekataa ombi la Manchester United inayohitaji kuipata huduma ya kipa wake wa kimataifa wa Argentina, Emiliano Martinez, kwa mkopo wa msimu mmoja.
Martinez mwenye umri wa miaka 32, aliibua tetesi za kuondoka mara baada ya msimu uliopita kumalizika ambapo alionekana akitoa ishara ya kuwaaga mashabiki wa Villa.
Mara baada ya hapo, kumekuwa na timu nyingi zinazohusishwa naye ikiwemo Manchester United.
Benchi la ufundi la Man United linahitaji sana huduma ya kipa mpya katika dirisha hili baada ya Andre Onana kutoonyesha kiwango bora msimu uliopita.
Martinez, mwenye umri wa miaka 32, amewavutia viongozi wa Man United kutokana na kiwango chake akiwa na Aston Villa na timu ya taifa ya Argentina.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usajili Fabrizio Romano, mshindi huyo wa Kombe la Dunia anaonekana kuwa tayari kuhamia Old Trafford.
Hata hivyo, baada ya United kuwasilisha ombi la kumchukua kwa mkopo, Aston Villa ilitoa msimamo kuwa kipa wao huyo hauzwi.
Kikosi hicho cha Unai Emery kipo katika nafasi nzuri ya mazungumzo, kwani Martinez bado ana mkataba wa miaka minne kuendelea na klabu hiyo.
Majadiliano yanaendelea ndani ya Man United kuhusu iwapo itoe ofa ili kumsajili mazima au ingalie
Igor Paixao
LEEDS United imewasilisha ofa Feyenoord ya zaidi ya Pauni 26 milioni ili kuipata huduma ya winga wa timu hiyo, Igor Paixao katika dirisha hili. Licha ya kuweka mzigo huo mezani bado kuna ushindani mkali kutoka AS Roma na Marseille ambazo pia zimeonyesha nia ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 25. Paixao amezivutia timu nyingi Ulaya kutokana na kiwango bora ambacho ameonyesha msimu uliopita ambapo alifunga mabao 18 katika mechi 47 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2029.
Jens Cajuste
BURNLEY imeulizia uwezekano wa kuipata huduma ya kiungo wa Napoli na timu ya taifa ya Sweden, Jens Cajuste mwenye umri wa miaka 25 katika dirisha hili la usajili Ulaya. Benchi la ufundi la Burnley limevitiwa na kiwango ambacho staa huyo alichokionyesha msimu uliopita alipokuwa akicheza kwa mkopo Ipswich Town. Jens ambaye ana mkataba na Napoli unaotamatika 2028 ambaye msimu uliopita alifunga bao moja katika mechi 33 za michuano yote.
Facundo Buonanotte
BORUSSIA Dortmund inatarajiwa kuwasilisha ofa Brighton kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo Facundo Buonanotte, 22, ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Leicester City. Mkataba wake umebakisha miaka mitatu kabla ya kumalizika, lakini ameshawaambia mabosi wa Brighton kwamba hataki kukosa nafasi ya kwenda Dortmund. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina anadaiwa kuuzwa kwa kiasi kisichopungua Euro 30 milioni. Msimu uliopita alicheza mechi 35 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Jacob Ramsey
NOTTINGHAM Forest imefikia hatua nzuri katika mazungumzo yao ya kumsajili kiungo wa Aston Villa, Jacob Ramsey, 24, katika dirisha hili. Mkataba wa Ramsey ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri msimu uliopita unamalizika 2027. Katika msimu uliopita alicheza mechi 46 za michuano yote. Forest inahitaji huduma ya fundi huyo wa kimataifa wa England kwa ajili ya kuboresha kikosi kuelekea michuano ya kimataifa msimu ujao.
Javi Guerra
VALENCIA bado inapambana kuhakikisha inamsainisha mkataba mpya Javi Guerra katika dirisha hili ikidaiwa anataka kuondoka na kutua Manchester United ambayo imeshaanza mazungumzo na wawakilishi wake. Guerra, 22, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote akafunga mabao matatu na kutoa asisti tatu. Kiungo ameshawaambia hadi mabosi wa Valencia kwamba anahitaji kuondoka.
Kobbie Mainoo
TOTTENHAM Hotspur inatarajiwa kuwasilisha ofa Manchester United hivi karibuni kwa ajili ya kumsajili kiungo wa timu hiyo, Kobbie Mainoo, katika dirisha hili. Mainoo ambaye mkataba wake unamalizika 2027 anaripotiwa kupewa ruhusa ya kuondoka ikiwa atapata timu ya kumsajili. Staa huyo ameripotiwa kugoma kusaini mkataba mpya kutokana na ofa ya mshahara ambayo amewekewa mezani.
Tyler Dibling
WINGA wa Southampton, Tyler Dibling ameingia katika orodha ya wachezaji ambao Everton inahitaji kuwasajili katika dirisha hili ili kuendelea kuboresha safu ya ushambuliaji kuelekea msimu ujao. Dibling mwenye umri wa miaka 19, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027 na msimu uliopita alicheza mechi 33 za michuano yote.