Arteta afurahia pointi tatu
Muktasari:
- Arsenal ilipata ushindi huo kupitia bao la dakika ya 80 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Noni Madueke, aliyekuwa akiingia akitokea benchi, katika mchezo ambao The Gunners walitawala umiliki wa mpira lakini walipata wakati mgumu kutengeneza nafasi za wazi za kufunga.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amepongeza ustahimilivu wa kikosi chake baada ya kuibuka na ushindi mwembamba dhidi ya Nottingham Forest, akisema wachezaji wake walilazimika kuvumilia presha na kusubiri wakati sahihi ili kupata matokeo.
Arsenal ilipata ushindi huo kupitia bao la dakika ya 80 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Noni Madueke, aliyekuwa akiingia akitokea benchi, katika mchezo ambao The Gunners walitawala umiliki wa mpira lakini walipata wakati mgumu kutengeneza nafasi za wazi za kufunga.
Bao hilo lilikuwa shuti pekee la Arsenal lililolenga lango katika mchezo huo, huku Arteta akionyesha tena umuhimu wa wachezaji wake wa akiba katika kuamua matokeo ya mechi.
Kikosi hicho cha London Kaskazini kilianza kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu, lakini kilishindwa kupenya ngome ya Forest iliyocheza kwa mfumo wa 3-4-1-2, maarufu kama 'Christmas tree'. Hali hiyo iliwalazimu Arsenal kufanya mabadiliko manne kipindi cha pili, yakiwamo kumwingiza Madueke, hatua iliyosaidia kubadili mwelekeo wa mchezo.
Ushindi huo umeifanya Arsenal kufikisha ushindi sita katika mechi saba za Ligi Kuu England, ikiendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi tatu pungufu ya Manchester City.
Akizungumzia mchezo huo, Arteta amesema kikosi chake kimeonyesha uwezo wa kushinda katika mazingira tofauti, licha ya kukabiliwa na wapinzani wanaocheza kwa kujilinda kwa nguvu.
“Tumecheza mechi 11 za mashindano mbalimbali na kushinda 10. Hivyo, tutalazimika kutafuta njia tofauti za kushinda katika mazingira tofauti. Tulijua leo tusingefunga ndani ya dakika 20 au 30 za kwanza,” amesema Arteta.
Ameongeza kuwa Nottingham Forest ilikuwa imejipanga vizuri kwa upande wa ulinzi, jambo lililofanya Arsenal ikose nafasi za kutumia kasi yake katika eneo la mwisho la ushambuliaji.
“Walikuwa wamejipanga vizuri sana. Hakukuwa na nafasi za kutosha kucheza. Ilitubidi kuwa makini katika pasi zetu na kufanya maamuzi sahihi. Vinginevyo, ulipaswa kuleta vurugu nyingi ndani ya eneo la hatari, iwe kupitia mchezo wa kawaida au mipira iliyokufa,” amesema.
Arteta alikiri kuwa timu yake ilishindwa kulenga lango kwa muda mrefu, akieleza kuwa wachezaji wake walihitaji kudhibiti hisia na kuepuka kufanya maamuzi ya haraka kutokana na kukosa bao.
Amesema kadiri mchezo ulivyoendelea, Arsenal ilipaswa kubadili namna ya kucheza ili isijiweke kwenye hatari ya kushambuliwa kwa sababu ya kuongezeka kwa presha.
“Niliamini kuwa nguvu za wapinzani zingepungua kadiri muda ulivyopita na nafasi zingekuwa kubwa zaidi. Hatimaye tulipata umaliziaji mzuri kwa sababu mchezo na mazingira yake yalibadilika kidogo. Baadaye tulilazimika kuteseka, hasa baada ya kukumbana na matukio mawili au matatu yaliyokuwa ya kushangaza,” ameongeza.
MADUEKE AIPA SIFA BENCHI LA ARSENAL
Arteta pia alimpongeza Madueke kwa mchango wake, akisema mshambuliaji huyo amekuwa akionyesha kiwango kingine tangu kurejea kwa mapumziko.
“Ninatabasamu kwa sababu yeye ni mtu wa kipekee. Yuko kwenye wakati mzuri. Baada ya mapumziko, ameonyesha kitu tofauti, kiwango kingine cha hamasa na kujiamini katika matendo yake. Ameanza kuwa mchezaji anayeamua matokeo ya mechi, jambo tunalotarajia kutoka kwa mchezaji wa aina yake,” amesema Arteta.
Kwa upande wake, Madueke amesema Arsenal ililazimika kupambana kwa nguvu ili kupata pointi zote tatu katika uwanja wa Nottingham Forest, akisisitiza kuwa ushindi huo ulikuwa muhimu licha ya ugumu wa mchezo.
“Ilitubidi kupambana kwa kina. Tunajua si rahisi kuja hapa. Namshukuru Mungu tuliweza kupata ushindi na sasa tunaendelea na safari yetu tukiwa na pointi tatu,” amesema.
Madueke pia alilisifu benchi la Arsenal, akieleza kuwa ubora wa wachezaji waliopo kikosini unatoa ushindani mkubwa na nafasi ya kila mmoja kuchangia matokeo, iwe anaanza mchezo au anaingia kipindi cha pili.
“Ukiangalia ubora wa kikosi chetu cha kwanza na wachezaji wa akiba, ni wa kiwango cha juu sana. Tunajua baadhi yetu tutaanza mechi na wengine tutamalizia. Kwangu, mtazamo unabaki uleule kila wakati; nataka kutengeneza nafasi au kufunga,” amesema.