Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Atletico yachefukwa kunyimwa penalti

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hispania, wachezaji na benchi la ufundi la Atletico walikerwa na mwenendo wa wapinzani pamoja na uamuzi wa waamuzi katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Emirates.

LONDON, ENGLAND: ATLETICO Madrid inadai kuchukizwa na kile kilichotokea katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal kufuatia kichapo cha bao 1-0 kilichoiondoa juzi kwenye mashindano hayo jijini London.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hispania, wachezaji na benchi la ufundi la Atletico walikerwa na mwenendo wa wapinzani pamoja na uamuzi wa waamuzi katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Emirates.

Hasira hizo zilionekana wazi wakati kocha Diego Simeone, alipomsukuma mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta, mwishoni mwa mchezo huo.

Hata hivyo, Simeone alionekana kujizuia mbele ya vyombo vya habari baada ya mechi akisisitiza kuwa hataki kutoa visingizio kufuatia kipigo hicho, lakini nyuma ya pazia taarifa zinaeleza kuwa hali ilikuwa tofauti kabisa huku klabu ikidaiwa kuanza kulalamika tangu ilipowasili England.

Inaelezwa kuwa mashabiki wa Arsenal waliwakaribisha kwa fataki karibu na hoteli yao, jambo lililochukuliwa kama vitisho na Atletico wakafikiria kuwasilisha malalamiko kwa UEFA.

Pia, uteuzi wa waamuzi uliibua sintofahamu, hasa kwa kuwepo kwa Daniel Siebert kama mwamuzi mkuu na Bastian Dankert kwenye VAR ambao rekodi zao na Atletico dhidi ya timu za England hazikuwa nzuri.

Atletico pia waliishutumu Arsenal kwa kutumia mbinu walizodai kuwa si za kiungwana, wakisema walikosa ulinzi wa kutosha walipokuwa wakielekea uwanjani huku wakikabiliwa na shamrashamra kali za mashabiki wa nyumbani.

Ndani ya uwanja, matukio kadhaa yalizua mjadala, ikiwemo kitendo cha Gabriel Martinelli kurusha mpira kwa mashabiki kuchelewesha mchezo, kabla ya kipa wa akiba Kepa Arrizabalaga kuupiga mbali uliporudishwa uwanjani.

Licha ya hayo, Atletico walidai kunyimwa penalti tatu muhimu. Tukio la kwanza lilihusisha Giuliano Simeone akidai kusukumwa ndani ya eneo la hatari huku jingine likimhusisha Gabriel Magalhaes kwa kumchezea rafu bila kuchukuliwa hatua.

Malalamiko makubwa zaidi yalikuwa pale Antoine Griezmann alipokanyagwa mguuni ndani ya box, lakini badala ya penalti, mwamuzi aliamua kutoa faulo dhidi ya Atletico kutokana na kosa lililotangulia.

Baada ya mechi, Simeone alisema: “Sitaki kuzungumzia tukio la Griezmann kwa sababu ni wazi kabisa. Kufanya hivyo itakuwa kutafuta visingizio na hilo sitaki.”

Katika tukio lingine lililozua gumzo, Simeone alionekana kukanyaga nembo ya Arsenal alipokuwa akielekea vyumbani, ishara iliyotafsiriwa kama kuonesha hasira yake.

Kwa upande wake, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, aliwasifu waamuzi akisema walifanya kazi nzuri bila matatizo yoyote huku akifurahia kuifikisha timu hiyo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006.