Arsenal kuna kitu kimetiki!

Muktasari:
- Arsenal ipo sokoni kusaka straika wa mabao dirisha hili ili kuwapa nguvu mpya kwenye msako wao wa ubingwa wa Ligi Kuu England, ambao imeshindwa kuubeba kwa zaidi ya miaka 20.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Arsenal sasa wameanza kuamini ni straika gani wa kiwango cha dunia watakayekwenda kumsajili kwenye dirisha hili baada ya kuwa follow kwenye ukurasa wa Instagram na kisha kinyozi wake akaweka mambo hadharani.
Arsenal ipo sokoni kusaka straika wa mabao dirisha hili ili kuwapa nguvu mpya kwenye msako wao wa ubingwa wa Ligi Kuu England, ambao imeshindwa kuubeba kwa zaidi ya miaka 20.
Na kwenye hilo, kikosi hicho kinachonolewa na Mhispaniola Mikel Arteta kimehusishwa na mastraika wengi, lakini wote wakiwa wa gharama kubwa.
Moja ya mastraika inaowasaka ni staa wa miaka 22, Benjamin Sesko, ambaye thamani yake inaripotiwa kuwa kati ya Pauni 68.5 milioni na Pauni 85.5 milioni na klabu yake ya RB Leipzig.
Ripoti zinafichua Arsenal ipo tayari kulipa Pauni 70 milioni kwa ajili ya kunasa saini ya straika huyo wa kimataifa wa Slovenia, ambaye amefunga mabao 21 na kuasisti sita katika michuano yote aliyotumikia timu yake msimu uliopita.
Sasa straika huyo mwenye kimo cha futi 6 na inchi 5 amefanya kitu kinachowapa mashabiki wa Arsenal matumaini anakwenda kujiunga nao dirisha hili baada ya kuwa mfuasi mpya wa ukurasa wa Instagram wa klabu hiyo yenye maskani yake Emirates.
Sambamba na hilo, kinyozi wa Sesko - ambaye akaunti yake ya Insta inasomeka kama Sensei.London, ambaye ana wafuasi 3,000 - naye ameshea ujumbe kwa staa huyo na kuzidi kuchochea uvumi wa atakuja kupiga mzigo huko Emirates msimu ujao.
Kuzungumzia ishu hiyo ya Instagram, posti ilimwonyesha Sesko akiwa amevaa miwani akiwa kwenye mapumziko na kufurahia jambo na kinyozi wake huyo walipokuwa huko Mykonos, Ugiriki. Posti hiyo ilikuwa na maelezo haya:
“Siku zote ni furaha kuwa na wewe kaka @Benjaminsesko.
“Tunaimani tutakuwa na wewe London.”
Kutokana na jambo hilo lililoendelea huko mtandaoni, shabiki mmoja wa Arsenal aliandika hivi: “Huu utakuwa usajili mzuri.” Shabiki wa pili aliandika: “Hebu acheni kunishawishi na hii furaha.”
Na shabiki wa tatu aliongeza: “Asante Mungu.”
Shabiki mwingine alisema: “Ni wakwetu sasa! Karibu nyumbani Benjamin Sesko.”
Na shabiki wa tano alisema: “Arsenal itahitaji mataji manne msimu ujao.”
Hata hivyo, wakati mashabiki wa Arsenal wakipagawa kwa straika huyo kuwa follow kwenye Insta, kwa Sesko hiyo si klabu kubwa ya kwanza kufanya hivyo, kwani pia amezifollow, Manchester City na Real Madrid.
Arsenal yenyewe ipo bize kwenye dirisha hili kusaka straika mpya, huku ikifichua imefikia pazuri kunasa saini ya nahodha wa Brentford, Christian Norgaard kwa dili lenye thamani ya Pauni 9.3 milioni.
Ipo pia kwenye hatua za mwisho za kunasa saini ya kipa Kepa Arrizabalaga kwa dili la Pauni 5 milioni.
Saini ya kiungo Martin Zubimendi ni kama imeshanaswa na kinachosubiriwa ni dili tu kutangazwa Julai Mosi, huku miamba hiyo ikiwa kwenye mchakamchaka pia wa kumfukuzia straika Viktor Gyokeres, ambaye pia yupo kwenye rada za Liverpool na Manchester United.