Argentina yaichakaza Burkina Faso
Muktasari:
- Argentina imeibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Burkina Faso, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki, uliochezwa kuanzia saa 9 alfajiri ya kuamkia leo kwa muda wa Tanzania katika Uwanja wa Monumental, Buenos Aires.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: Argentina imepata ushindi mnono wa mabao 7-0 dhidi ya Burkina Faso katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Monumental, Buenos Aires.
Argentina ilianza kwa kasi na kupata bao la kwanza kupitia Lautaro Martínez katika dakika ya nne, baada ya kumalizia mpira uliorejea baada ya yeye kukosa penalti.
Moumouni Diallo alijifunga katika dakika ya nane kuipa Argentina bao la pili, kisha Gianluca Prestianni kuongeza bao la tatu katika dakika ya 12.
Nicolás Paz aliifanya Argentina kuongozakwa mabao 4-0 katika dakika ya 35, huku Julián Álvarez akifunga bao la tano dakika moja baadaye na kuifanya Argentina kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 5-0.
Katika kipindi cha pili, Franco Mastantuono alifunga bao la sita katika dakika ya 57, na Giuliano Simeone kukamilisha ushindi huo katika dakika za majeruhi.
Kwa mujibu wa takwimu za mchezo, Argentina ilitawala umiliki wa mpira kwa asilimia 75 na kupiga mashuti 30, huku Burkina Faso ikiwa na mashuti matatu pekee.
Ushindi huo unaendeleza maandalizi ya Argentina katika dirisha hili la kimataifa, huku mechi hiyo ikiwa sehemu ya ratiba yake ya michezo ya kirafiki.
Burkina Faso, ambayo iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na changamoto za usafiri na ililazimika kutumia kwa kiasi kikubwa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 23, ilishindwa kuhimili kasi na ubora wa wenyeji.
Argentina sasa inatarajiwa kumaliza ratiba yake ya dirisha hili la FIFA kwa mchezo dhidi ya Benin Jumanne, Oktoba 6, katika Uwanja wa Monumental, ambao pia unatarajiwa kuwa mchezo wa kuagwa kwa Lionel Messi katika timu hiyo.