Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kwenye hatua za mwisho za AFCON 2027, Motsepe akagua Kwa Mkapa

Muktasari:

  • Uwanja wa Benjamin Mkapa ulifungwa Machi 2026 ili kupisha awamu ya mwisho ya maboresho ya eneo la kuchezea na miundombinu mengine muhimu.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, leo Septemba 17, 2026 amekagua Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa maandalizi ya Tanzania kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.

CAF imesema ziara hiyo inalenga kutathmini maendeleo ya miundombinu na maeneo mengine muhimu kuelekea mashindano hayo.

Uwanja wa Benjamin Mkapa ulifungwa Machi 2026 ili kupisha awamu ya mwisho ya maboresho ya eneo la kuchezea na miundombinu mengine muhimu.

Awamu hiyo ilikadiriwa kuchukua kati ya miezi sita na mwaka mmoja, huku maboresho yakihusisha pia maeneo ya majukwaa ya VIP, VVIP na miundombinu ya vyombo vya habari.

Kabla ya awamu hiyo, Uwanja wa Benjamin Mkapa tayari ulikuwa umefanyiwa maboresho mbalimbali, ikiwamo uwekaji wa viti vipya na kuboreshwa kwa vyumba vya kubadilishia nguo.

Aprili 2026, serikali ilieleza kuwa ukarabati wa uwanja huo ulikuwa umefikia asilimia 95.

Serikali katika bajeti ya mwaka 2025/26 iliweka Sh179.8 bilioni kwa ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mpira kama sehemu ya maandalizi ya AFCON 2027.

Kiasi hicho ni cha miradi ya viwanja kwa ujumla na si gharama ya Benjamin Mkapa pekee.

Mradi wenye gharama kubwa zaidi ni wa ujenzi wa Uwanja wa Samia Suluhu Hassan jijini Arusha, ambao gharama yake imefikia Sh338.54 bilioni, kutoka makadirio ya awali ya Sh187 bilioni.

Serikali imeeleza kuwa makadirio ya awali yaliandaliwa mwaka 2021, kabla Tanzania haijapata idhini ya CAF kuwa mwenyeji wa mechi za AFCON 2027, jambo lililohitaji viwango na mahitaji ya ziada.

Uwanja wa Arusha wenye uwezo wa kuingiza takriban watazamaji 30,000 ni miongoni mwa miundombinu mipya inayojengwa kwa ajili ya mashindano hayo. Kufikia Septemba 2026, Serikali ilisema ujenzi ulikuwa umefikia takriban asilimia 95, huku ukitarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Mbali na Arusha na Mkapa, Tanzania inaendelea na maandalizi ya Fumba, Zanzibar, wakati pia ujenzi wa Uwanja wa Dodoma ukiendelea.

Dodoma ni mradi mwingine mkubwa uliotangazwa kama sehemu ya upanuzi wa miundombinu ya michezo nchini, ukiwa na uwezo wa kubeba watazamaji 32,000.

Hata hivyo kati ya viwanja hivyo vitano, ni viwanja vinne tu vya Tanzania vinavyoandaliwa kutumika kwa AFCON 2027 kwa vile uwanja wa Dodoma utachelewa kumalizika.

Hadi sasa Benjamin Mkapa, Arusha, New Amaan Conplex na Fumba vimekuwa miongoni mwa vituo vilivyokaguliwa katika maandalizi.

CAF pia hukagua viwanja vya mazoezi, hoteli, hospitali, usafiri na miundombinu mingine muhimu kabla ya kuthibitisha venues za mashindano.

Ziara ya Motsepe hivyo inakuja wakati Tanzania ikiingia katika hatua za mwisho za maandalizi, huku Serikali ikiendelea na maboresho ya viwanja na miundombinu mingine.

AFCON 2027 imepangwa kufanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027, ingawa CAF bado haijatangaza rasmi orodha ya mwisho ya viwanja vitakavyotumika katika fainali hizo.