Nahodha Ngorongoro Heroes ataja malengo makubwa CECAFA
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, mabao hayo matatu yalifungwa na Faraji Kayanda dakika ya 30, Juma Abushiri dakika ya 37 na lile la tatu likifungwa na Evastus Lukanima dakika ya 41.
NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, Arafat Ally amesema ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Rwanda umeongeza kujiamini kwa wachezaji katika harakati za kutetea taji na kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Ghana 2027.
Mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, mabao hayo matatu yalifungwa na Faraji Kayanda dakika ya 30, Juma Abushiri dakika ya 37 na lile la tatu likifungwa na Evastus Lukanima dakika ya 41.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo huo wa kwanza wa michuano ya CECAFA U-20, nahodha huyo alisema matokeo hayo yana umuhimu mkubwa kwao kwa sababu yamewapa mwanzo mzuri wa mashindano.
“Pointi tatu zina maana kubwa kwetu sisi kama wachezaji, maana tunahitaji kupambana kushinda kila mchezo ili kutetea taji hili. Pia zinatia motisha kwa wachezaji, maana ni mchezo wa kwanza unaweza kujitia presha au ukajenga kujiamini,” alisema.
Nahodha huyo alisema wanaelekeza nguvu zao kwenye mechi inayofuata dhidi ya Ethiopia itakayopigwa Septemba 19 Uwanja wa Uhuru saa 2 usiku.
“Kwa sasa tunafokasi na mchezo unaokuja, ila zina maana kubwa sana kwetu sisi kama wachezaji kwa sababu zimetutengenezea hali ya kuingia mechi ijayo tukiwa kifua mbele na morali kubwa,” alisema.
Ngorongoro Heroes ilianza kampeni yake ya CECAFA U-20 kwa nguvu baada ya kuifunga Rwanda mabao 3-0, matokeo ambayo yamekiweka kikosi hicho katika nafasi nzuri ya kutetea taji hilo.
Tanzania inalenga kufanya vizuri katika michuano hiyo ili kupata nafasi ya kufuzu Fainali za AFCON U-20 zitakazofanyika Ghana mwaka 2027.