Arsenal yaivizia saini ya Nico Paz
Muktasari:
Paz, raia wa Argentina, amekuwa mmoja wa vipaji vinavyong’ara Serie A chini ya kocha Cesc Fabregas, hali iliyovutia pia klabu kadhaa kubwa Ulaya. Arsenal sasa ni miongoni mwa zinazofuatilia maendeleo yake.
MABINGWA wa England, Arsenal inafuatilia kwa karibu kiungo mshambuliaji wa Como, Nico Paz, 22, huku kocha Mikel Arteta akitafuta wachezaji wa aina hiyo watakaoweza kuimarisha kikosi chake kwa muda mrefu.
Paz, raia wa Argentina, amekuwa mmoja wa vipaji vinavyong’ara Serie A chini ya kocha Cesc Fabregas, hali iliyovutia pia klabu kadhaa kubwa Ulaya. Arsenal sasa ni miongoni mwa zinazofuatilia maendeleo yake.
Como ilimsajili moja kwa moja Paz msimu huu kwa takriban Euro 60 milioni, lakini Real Madrid iliweka kipengele cha kumrudisha mchezaji huyo kwa Euro 80 milioni katika kiangazi cha 2027.
Hilo linaweza kuwa kikwazo kwa Arsenal, kwani hata kama itafikia makubaliano na Como, Real Madrid inaweza kutumia kipengele hicho na kumrudisha Paz Santiago Bernabeu.
Fabregas amewahi kumfananisha Paz na gwiji wa Argentina, Lionel Messi, kutokana na namna wapinzani wanavyomkabili uwanjani. Paz mwenyewe amesisitiza kuwa alichagua kubaki Italia ili kupata muda zaidi wa kucheza badala ya kurejea Madrid na kugombea nafasi na viungo wakubwa waliopo kikosini.
Cher Ndour
Kiungo wa Fiorentina, Cher Ndour (22), ameanza kuwa miongoni mwa wachezaji wanaosakwa zaidi katika dirisha la usajili kutokana na kiwango chake cha uchezaji, ukomavu na nguvu anazoonyesha katikati ya uwanja. Miongoni mwa klabu zinazosaka huduma yake ni pamoja na Liverpool na Aston Villa.
Geny Catamo
Sunderland bado haijakata tamaa kumnasa winga wa Msumbiji, Geny Catamo, 25, kutoka Sporting, licha ya kushindwa kumsajili dirisha la usajili lililopita. Nyota huyo amekuwa msaada mkubwa Sporting na katika Ligi ya Mabingwa msimu huu amefunga bao moja katika mechi ya kwanza timu hiyo ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Galatasaray.
Lamine Camara
Monaco inaamini inaweza kupata Euro 70 milioni kwa kiungo wa Senegal, Lamine Camara, 22, anayewindwa na Chelsea na Liverpool, baada ya uhamisho wake kwenda Stamford Bridge kuvurugika siku ya mwisho ya usajili. Miamba hiyo ya Ligi Kuu England inawinda saini yake akaongeze nguvu katika vikosi vyao.
Lukas Nmecha
Mshambuliaji wa Ujerumani, Lukas Nmecha, 25, anatarajia kuondoka Leeds United mwishoni mwa msimu huu mkataba wake utakapomalizika, iwapo hatapewa nafasi zaidi ya kucheza. Nmecha amekuwa hapati nafasi na hilo linaweza likamfanya akaondoka hata dirisha la usajili la Januari.
Luke Chambers
Celtic inafuatilia kwa karibu maendeleo ya beki wa kushoto wa Liverpool, Luke Chambers, mwenye umri wa miaka 22, huku ikipanga uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la Januari. Chambers amekuwa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi hicho cha Majogoo na uwezekano wa kuondoka ni mkubwa.
Wilfried Zaha
Winga wa Ivory Coast, Wilfried Zaha, 33, amepewa nafasi ya kujiunga na Malaga baada ya kuondoka Galatasaray kama mchezaji huru. Zaha ameondoka Uturuki baada ya vipindi viwili vya mkopo akiwa na Charlotte FC ya Marekani. Malaga inamwona kama mshambuliaji sahihi wa kwenda kuongeza nguvu kikosini
Raphinha
Barcelona imeanza kufikiria kumuongezea mkataba winga wake wa Brazil, Raphinha, 29, licha ya mkataba wake wa sasa kumalizika mwaka 2028. Mabingwa hao wa Hispania wanataka kumbakiza hadi 2030. Msimu huu nyota huyo wa kimataifa wa Brazil amekuwa na kiwango kizuri katika mechi za timu hiyo.
Hamza Abdelkarim
Barcelona imekamilisha mchakato wa kumuongezea mkataba mshambuliaji wa Misri, Hamza Abdelkarim, 18, hadi mwaka 2030. Mkataba huo umewekewa kipengele cha kuuvunja cha Euro 150 milioni endapo atataka kuondoka kama timu nyingine inataka huduma yake.
Gabriel Rajkovic
Arsenal na Chelsea zinaongoza mbio za kumsajili kinda wa Norway, Gabriel Rajkovic, 15, anayetajwa kuwa miongoni mwa vipaji vinavyong’ara zaidi Ulaya. Rajkovic anafanya msimu wa kuvutia mwaka 2026, akivunja rekodi kadhaa na tayari kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Valerenga licha ya umri wake mdogo.