Andre Onana atua katika anga za Inter Milan Ulaya
Muktasari:
- Onana, 29, alijiunga na Manchester United Julai 2023 akitokea Inter Milan kwa ada ya takribani Pauni 47.2 milioni alisajiliwa kuchukua nafasi ya David de Gea aliyekuwa kipa namba moja kwa zaidi ya miaka 12.
INTER Milan inamfuatilia kwa karibu kipa wa Manchester United na timu ya taifa ya Cameroon, Andre Onana, ambaye anahusishwa kuwa katika mpango wa kuachana na Mashetani Wekundu katika dirisha hili.
Onana, 29, alijiunga na Manchester United Julai 2023 akitokea Inter Milan kwa ada ya takribani Pauni 47.2 milioni alisajiliwa kuchukua nafasi ya David de Gea aliyekuwa kipa namba moja kwa zaidi ya miaka 12.
Hata hivyo, msimu wake wa kwanza Old Trafford ulikuwa na changamoto nyingi kutokana na makosa ya mara kwa mara na presha kubwa kutoka kwa mashabiki.
Vyanzo vya karibu na klabu vinadai kuwa Man United tayari imeanza kuangalia mbadala wake ikihusishwa na Mike Maignan wa AC Milan na Diogo Costa kutoka FC Porto. Inter Milan ambayo msimu uliopita ilicheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG inadaiwa kuwa tayari kutoa takribani Pauni 30 milioni ili kumrejesha kipa huyo.
Raheem Sterling
CHELSEA imeweka wazi kwamba iko tayari kumtoa kwa mkopo winga raia wa England, Raheem Sterling, 30, pamoja na wachezaji wengine wanane kabla ya kufungwa kwa dirisha hili la usajili. Sterling aliyejiunga na Chelsea 2022 kutoka Manchester City, amekuwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo jambo linalosababisha atolewe kwa mkopo mara kadhaa. Msimu uliopita alicheza Arsenal kwa mkopo.
Christopher Nkunku
MABOSI wa Chelsea wamekataa ombi la Bayern Munich inayohitaji huduma ya mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Christopher Nkunku kwa mkopo wa msimu mmoja. Klabu hiyo yenye maskani yake London inaripotiwa kuhitaji karibu Pauni 40 milioni kama ada ya uhamisho ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27. Mkataba wa Nkuku unatarajiwa kumalizika 2029.
Yoane Wissa
NEWCASTLE United inajiandaa kuwasilisha ofa mpya ya Pauni 35 milioni kwa ajili ya mshambuliaji wa Brentfird na DR Congo, Yoane Wissa. Hata hivyo, taarifa zinadai Brentford imesitisha mpango wa kumuuza staa huyo mwenye umri wa miaka 28, hadi pale itakapokuwa na uhakika wa kupata mbadala wake. Vigogo wa Newcastle wamehamia kwa Wissa kwa muda sasa.
Eberechi Eze
CRYSTAL Palace inataka kuendelea kusalia na mastaa wake, Eberechi Eze na Marc Guehi kuhakikisha inafanya vizuri kimataifa ambako inashiriki Europa Conference League. Tottenham Hotspur na Liverpool ndizo zinadaiwa kuhitaji sana huduma za mafundi hao. Tottenham tayari imeshatuma ombi kwa Palace kuhusu muundo wa malipo ya Pauni 55 milioni ili kumpata Eze.
Jadon Sancho
WINGA wa Manchester United na England, Jadon Sancho, 25, amekataa nafasi ya kujiunga na AS Roma dirisha hili licha ya timu hiyo kuwa tayari kulipa Pauni 20 milioni inayokuwa ikihitajika kama ada ya uhamisho. Inaelezwa Sancho ambaye alitua Man United 2021, anataka kurudi Dortmund. Man United haionekani kuwa tayari kwa hilo kwani Dortmund inataka kumchukua kwa mkopo badala ya kumnunua.
Federico Chiesa
WINGA wa Liverpool na timu ya taifa ya Italia, Federico Chiesa, 27, ameiambia timu hiyo kwamba anataka kubaki msimu ujao kupambania namba katika kikosi cha kwanza. Chiesa aliyejiunga na Liverpool akitokea Juventus msimu uliopita, amekuwa na wakati mgumu kwenye timu hiyo akiandamwa na majeraha ambayo yalisababisha asipate nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Nicolas Jackson
ASTON Villa imemuongeza mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Senegal, Nicolas Jackson, kwenye orodha yao ya wachezaji eneo la ushambuliaji ambao inataka kuwasajili katika dirisha hili. Mbali ya Villa, saini ya staa huyo pia inahitajika Bayern Munich ambayo inavutiwa naye. Jackson ameripotiwa kuwa hayupo tayari kuondoka England kwa sasa, hivyo anaangalia zaidi ofa za timu za EPL.