Amorim kuwapiga chini wachezaji hawa!

Muktasari:
- Kocha huyo Mreno anaonekana kutokuwa tayari kufanya kazi na mawinga hao wanne wanaolipwa pesa ndefu huko Old Trafford na kitu kinachoonekana wazi wakali hao siku zao zimefikia ukomo.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amepanga kuwapiga chini Alejandro Garnacho, Marcus Rashford, Antony na Jadon Sancho kwenye orodha ya mastaa atakaowajumuisha kwenye kikosi chake kitakachokwenda kwenye ziara ya michezo ya pre-season huko Marekani.
Kocha huyo Mreno anaonekana kutokuwa tayari kufanya kazi na mawinga hao wanne wanaolipwa pesa ndefu huko Old Trafford na kitu kinachoonekana wazi wakali hao siku zao zimefikia ukomo.
Na kwenye hilo, kama wakali hao wanne hawatakuwa wamepata timu za kujiunga nazo hadi kufikia wakati huo timu hiyo itakapohitaji kupanda ndege kwenda Marekani, Julai mwaka huu basi watalazimika kufanya mazoezi kivyao huko Carrington.
Chanzo kutoka ndani ya klabu kilibainisha hivi: “Amorim anajaribu kuweka mamlaka yake kwenye klabu. Ilikuwa ngumu kwake kuwasili katikati ya msimu, lakini sasa ana fursa nzuri ya kutengeneza timu kwa namna anavyotaka. Na hataki kupoteza muda kwenye hilo.
“Anataka wachezaji tu ambao watafia timu na watakubaliana na mtindo wake. Anataka pia kikosi kisichokuwa na wachezaji wengi ili kuweka mshikamano na kutoa nafasi ya kutosha ya kucheza kwa wachezaji hao. Hataki mtu yeyote mharibifu kwenye kikosi chake.”
Kocha Amorim yupo kwenye presha kubwa akijaribu kuweka mambo sawa kwenye kikosi hicho baada ya kumaliza katika nafasi ya 15 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ikiwa ni nafasi ya hovyo zaidi kuwahi kushika tangu iliposhuka daraja msimu wa 1973-74.
Kazi ya Amorim ya kuijenga upya Man United imeshaanza baada ya kutumia Pauni 62.5 milioni kunasa huduma ya mkali wa Wolves, Matheus Cunha na bado wapo kwenye mchakato wa kumfukuzia Bryan Mbeumo kutoka Brentford. Kocha huyo wa zamani wa Sporting yupo pia kwenye vita kali na kocha wa Arsenal, Mikel Arteta katika kufukuzia huduma ya straika wa Sporting, Viktor Gyokeres.
Kwa kuwaondoa kwenye kikosi Garnacho, Rashford, Antony na Sancho kutaifanya Man United kuokoa pesa ambazo zitawasaidia katika mchakato wa kunasa wakali wapya wa kuja kupiga kazi kikosini. Kwa namna hiyo, wakali hao huenda wasiwepo kwenye mechi tatu za ziara ya Man United kwenye pre-season yao Marekani.
United itakipiga huko New Jersey dhidi ya West Ham United, Julai 26 na baada ya hapo itakwenda Chicago kukabiliana na Bournemouth siku nne baadaye na itamaliza ziada yake huko Atlanta kwa kumenyana na Everton, Agosti 3.
Garnacho, 20, tayari amewekwa ubaoni na kwamba Napoli inataka huduma yake kwa Pauni 45 milioni, lakini Man United inataka kuvuna Pauni 70 milioni kwenye dili la kumuuza Muargentina huyo. Mabingwa hao wa Italia wameonyesha pia dhamira yao ya kumsajili Sancho, baada ya hatima ya maisha yake kuwa kwenye mashaka makubwa baada ya Chelsea kuachana na mpango wa kumchukua jumla baada kumnasa kwa mkopo kwenye nusu ya pili ya msimu uliopita.
Chelsea ilipaswa kulipa Pauni 25 milioni kumchukua jumla staa huyo, lakini badala yake imeamua kulipa Pauni 5 milioni na kumrudisha Old Trafford Sancho. Kuhusu Rashford, miamba mingine ya Ligi Kuu England, Newcastle United kuhitaji huduma ya winga huyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri alipokuwa kwa mkopo Aston Villa.
Winga wa Kibrazili, Antony naye alicheza kwa mkopo Real Betis na kufanya vizuri huko Hispania, lakini kwa kocha Amorim mastaa hao wote wanne hawana nafasi kwenye timu yake, anataka wampishe.