Amorim anacheka tu kuhusu Mainoo
Muktasari:
- Man United iliambulia sare katika mechi hiyo iliyofanyika uwanjani Old Trafford baada ya Soungoutou Magassa kuisawazishia West Ham kufuatia bao la utangulizi la Diogo Dalot.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Ruben Amorim amebaki akicheka tu mbele ya waandishi wa habari wakati walipojaribu kumwambia kiungo Kobbie Mainoo alipaswa kuchezeshwa kwenye mechi ya West Ham United.
Man United iliambulia sare katika mechi hiyo iliyofanyika uwanjani Old Trafford baada ya Soungoutou Magassa kuisawazishia West Ham kufuatia bao la utangulizi la Diogo Dalot.
Mainoo aliishia tu kukaa benchini bila ya kutumika katika mechi hiyo ya Old Trafford, huku akiwa ametumika kwenye dakika 171 tu kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Katika mkutano wa waandishi wa habari, kocha Amorim aliulizwa kuhusu mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kushambulia ambaye anapaswa kuingizwa kwenye dakika za mwisho za mchezo huo. Na mwandishi huyo alipoweka ubaoni jina la kiungo Mainoo ubaoni, kocha huyo wa Man United aliishia tu kucheka.
Ikumbukwe kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Mainoo alitaka kuondoka ili akapate timu itakayompa nafasi ya kucheza, huku ikielezwa kulikuwa na klabu 12 zilizokuwa zikihitaji saini yake, ikiwamo mabingwa wa Serie A, Napoli.
Dirisha lijalo la usajili litafunguliwa Januari, lakini Man United inaweza isimfungulie mlango wa kutokea Mainoo kwa sababu kuna wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo watakwenda kucheza mashindano ya Afcon 2025.
Wachezaji watakaokwenda kwenye Afcon 2025 ni Bryan Mbeumo, Amad Diallo na Noussair Mazraoui watakapokwenda kujiunga na timu za Cameroon, Ivory Coast na Morocco mtawalia.
Kuhusu Mainoo, Amorim alisema: “Sijui nini kitatokea. Itategemea. Kama nikiona mazoezini anafanya vizuri, nitamtumia. Hicho ndicho kitu pekee ninachoweza kukisema kujibu hilo. Kazi yangu ni kutoa majibu, lakini siku zote nitajibu kilekile.”