Amorim ampa maagizo Mainoo
Muktasari:
- Na kitu kizuri kwa staa huyo zao la akademia ya Man United, ametumia muda mwingi benchini kumtazama Casemiro anachokifanya ndani ya uwanja.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amemtaka kiungo Kobbie Mainoo kumtazama Casemiro kama mfano ili kubadili hali ya maisha yake kwenye kikosi hicho cha Old Trafford na kupata nafasi ya kucheza kila dakika.
Na kitu kizuri kwa staa huyo zao la akademia ya Man United, ametumia muda mwingi benchini kumtazama Casemiro anachokifanya ndani ya uwanja.
Man United ilizuia ombi la Mainoo kuondoka kwa mkopo kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, huku mechi yake pekee aliyoanzishwa kwa msimu huu ukiweka kando mechi ya Bournemouth usiku wa Jumatatu ilikuwa ile ya raundi ya pili kwenye Kombe la Ligi dhidi ya Grimsby Town iliyofanyika Agosti mwaka huu.
Mainoo, 20, anataka muda wa kutosha wa kucheza na ndio maana anataka kuondoka, lakini Man United inamtaka abaki na haina mpango wa kumwondoa hata kwenye dirisha la Januari kwa sababu Noussair Mazraoui, Bryan Mbeumo na Amad Diallo wataondoka kwa muda kwenye timu kwenda kuzitumikia timu zao za taifa katika mashindano ya Afcon 2025 huko Morocco.
Amorim, ambaye kikosi chake cha Man United kilitarajia kukabiliana na Bournemouth kwenye mchezo wa Ligi Kuu England usiku wa Jumatatu, hajakaa kitako na kiungo Mainoo kwa ajili ya kujadiliana juu ya hatima ya maisha yake.
Na kocha huyo Mreno alisema kwamba mara zote amekuwa akiweka kipaumbele kwa timu kuliko mchezaji mmoja mmoja. Kisha alionya kwamba si mara zote maisha yanakwenda kuwa mazuri unapoondoka Man United kutokana na kile kilichotokea kwa wachezaji wengine ambao ni zao la kutoka kwenye akademia ya klabu hiyo.
Amorim alisema: “Timu ni kipaumbele cha kwanza na kama Kobbie atakuja kuzungumza na mimi, tutazungumza. Sitasema ni kitu gani nitamwambia Kobbie, lakini nitashukuru kama atakuja kuzungumza na mimi.
“Ninachotaka wachezaji wangu kuwa na furaha na nafahamu kila mtu ana malengo yake. Kuchukia hakumsaidii yeyote. Kwa sasa, akili yetu ipo kwenye mechi na kuona ni kitu gani kitatokea.”
Amorim aliulizwa kama anamweka Mainoo kwenye hesabu zake baada ya kumwanzisha kiungo huyo Mwingereza mara 16 tu katika mechi 58 alizoongoza miamba hiyo ya Old Trafford kabla ya mechi ya usiku wa Jumatatu dhidi ya Bournemouth.
Amorim alisema: “Bila shaka. Kama ilivyo kwa yeyote aliyepo hapa. Tatizo ni kwamba tunacheza na viungo wawili na nyie watu mnamtazama Kobbie katika namna tofauti na ninavyomtazama mimi.
“Pengine kama tutacheza na viungo watatu, sio wawili. Lakini, kama watakuwa viungo watatu, Kobbie atapata dakika za kutosha za kucheza. Hebu fikiri hilo linaweza kutokea na hapo kuna mtu pale mbele atapoteza namba. Wakati mwingine ni suala la muda tu, kwa sababu hilo limeshathibitika huko nyuma.
“Unaweza kunibadili msimamo wangu, kwenye hilo Casemiro nadhani ni mfano mzuri. Alikuwa chaguo la chini kabisa nyuma hata ya Toby Collyer, lakini kwa sasa ni staa panga pangua. Collyer alichezea kikosi cha kwanza cha Man United. Ametokea kwenye akademia yetu, alikuwa hapa.
“Amekwenda West Bromwich. Kule hachezi. Hapa alikuwa akicheza. Hivyo, wakati mwingine si kwa sababu unatokea kwenye akademia ndiyo maana kuchezi mara kwa mara. Ni hali ya mambo tu na vile mambo yamekuwa yakitokea. Sijui nini kitakwenda kutokea baadaye kwa Mainoo. Ngoja tuone baada ya mechi dhidi ya Bournemouth.”
Mainoo amekuwa akichuana na nahodha Bruno Fernandes kwenye majukumu ya kiungo ya kushambulia katika fomesheni pendwa ya kocha Amorim ya 3-4-2-1. Kocha Amorim alisema pia inamweka kwenye wakati mgumu kutoa Casemiro kwa ajili ya kumwingiza Mainoo kwenye kiungo ya kukaba, kwa sababu Mbrazili huyo anafanya kazi kubwa.
Mainoo aliingia kuchukua nafasi ya Casemiro wakati Man United ilipokuwa na faida ya mtu mmoja uwanjani kwenye mechi ya kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Everton mwezi uliopita. Lakini, Mbrazili Casemiro mara zote amekuwa akitoka ili kuingia Manuel Ugarte, ambaye kiuchezaji wamekuwa wakishabihiana.
Amorim alisema: “Nilimtoa Casemiro na kumwingiza Kobbie dhidi ya Everton kwa sababu tulijaribu kucheza staili tofauti. Anaweza kucheza kwenye hiyo nafasi. Lakini, ni ngumu wakati mwingine. Kama ukitazama timu yetu ikiwa na Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na wakati mwingine Bruno, ambaye watu husema ni Namba 10, wakati mwingine Kobbie, Manu (Ugarte), unaweza kuona mimi ni mtu nisiyependa soka la kushambulia haraka. Anahitaji kuwa na muda wa kujifunza kwenye hilo, atakuwa sehemu ya mtindo huyo wa kiuchezaji kwa siku za baadaye.”
Gwiji wa Man United, Paul Scholes, ambaye pia ni zao la akademia ya miamba hiyo ya Old Trafford, alimtaka Mainoo kuondoka kwenye timu hiyo katika dirisha la Januari huku akimponda kocha Amorim kuwa hafai.
Makocha waliopita Man United, Louis van Gaal, Jose Mourinho na Erik ten Hag walikuwa wakikerwa sana na maneno ya magwiji hao wachezaji wa zamani wa Old Trafford, lakini Amorim amekuwa wala hana shida na maneno yao.