Amorim akataa kazi Benfica, ampa ‘ulaji’ Marco Silva
Muktasari:
- Kabla ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, Amorim alikuwa anahusishwa na kiti hicho cha Benfica mapema wiki hii. Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa Amorim alikataa ofa hiyo.
KITENDO cha Ruben Amorim kukataa ofa ya kuinoa Benfica ya Ureno, imempa nafasi kocha wa Fulham, Marco Silva, kuchukua dili hilo.
Silva mwenye umri wa miaka 48, amekuwa akitafuta changamoto mpya baada ya kudumu Craven Cottage kwa miaka mitano, huku kipaumbele chake kikubwa kikiwa ni kurejea nyumbani kwao Ureno.
Mwandishi wa habari za usajili, Sacha Tavolieri, amethibitisha kuwa Silva amefikia makubaliano na miamba hiyo ya soka la Ureno ili kuchukua mikoba ya Jose Mourinho, ambaye anatajwa kurejea Real Madrid kipindi kijacho cha majira ya kiangazi.
Kabla ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, Amorim alikuwa anahusishwa na kiti hicho cha Benfica mapema wiki hii. Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa Amorim alikataa ofa hiyo.
Amorim aliondoshwa Manchester United mapema mwaka huu baada ya kuinoa timu hiyo kwenye mechi 63, akipata ushindi mara 25, sare 15 na vipigo 23. Alitua kwa miamba hiyo ya Old Trafford, Novemba 2024.
Kabla ya kwenda England, Amorim alianzia ukocha nchini Ureno akizifundisha Casa Pia, Braga na baadaye Sporting Lisbon kuanzia mwaka 2020 hadi 2024.
Kwa upande wake, Marco Silva anaondoka magharibi mwa London akiwa amesimamia Fulham jumla ya michezo 228, amefanikiwa kupata ushindi katika mechi 103, sare 42 na kupoteza 83.
Kabla ya kujiunga na Fulham mwaka 2021, kocha huyo Mreno alizinoa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya England ikiwemo Everton, Watford na Hull City. Pia miamba ya Ugiriki, Olympiacos.
Kama ilivyo kwa Amorim, Silva alianzia ukocha nchini Ureno katika klabu ya Estoril, pia amewahi kuinoa Sporting Lisbon kwa muda wa mwaka mmoja.