Gamondi amtaja aliyeiua Stars
Muktasari:
- Septemba 25, 2026, Taifa Stars ilipoteza mchezo huo wa Kundi L kufuzu AFCON 2027 kwa mabao 2-0 baada ya Guinea-Bissau kutumia vyema nafasi ilizopata, ikiwemo mpira mrefu uliozaa bao la kwanza lililofungwa na Franculino Djú dakika ya 33 akimalizia pasi ya Beto na shambulio la kushtukiza lililozaa bao la pili dakika ya 58, mfungaji akiwa Mama Baldé.
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema tofauti kubwa iliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Guinea-Bissau wa kufuzu Fainali za AFCON 2027 ilikuwa uwezo wa wapinzani kutumia nafasi chache walizopata, huku akitaja pia uwepo wa mshambuliaji mzoefu aliyekipiga Ligi Kuu England, Norberto Betuncal maarufu Beto kuchangia hilo.
Septemba 25, 2026, Taifa Stars ilipoteza mchezo huo wa Kundi L kufuzu AFCON 2027 kwa mabao 2-0 baada ya Guinea-Bissau kutumia vyema nafasi ilizopata, ikiwemo mpira mrefu uliozaa bao la kwanza lililofungwa na Franculino Djú dakika ya 33 akimalizia pasi ya Beto na shambulio la kushtukiza lililozaa bao la pili dakika ya 58, mfungaji akiwa Mama Baldé.
Gamondi alisema uwepo wa Beto aliyewahi kuitumikia Everton kabla ya msimu huu kutimkia Ligi Kuu Italia katika kikosi cha Fiorentina, uliifanya Taifa Stars kukutana na changamoto kubwa, huku akisisitiza kuwa kikosi chake kilistahili kupata angalau bao kutokana na namna kilivyocheza.
“Tofauti kubwa unaweza kuiona wanapokuwa na mchezaji kama mshambuliaji aliyecheza Ligi Kuu England, ilikuwa vigumu sana kwetu. Lakini kwa ujumla, sikufurahishwa na matokeo kwa sababu nadhani tulistahili angalau kupata bao,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema tatizo kubwa la Taifa Stars lilikuwa kushindwa kutumia vyema nafasi ilizopata katika mita 25 za mwisho za eneo la usambuliaji, akitolea mfano nafasi za mapema alizopata Simon Msuva.
“Mpira wa miguu si kuhusu kusema unastahili, ni kuhusu kuweka mpira kimiani. Kama tungetumia nafasi zile za mapema za Simon Msuva, mchezo ungebadilika kabisa,” alisema.
Pamoja na matokeo hayo, Gamondi amepongeza nidhamu na moyo wa upambanaji ulioonyeshwa na wachezaji wake, akisema hawakukata tamaa hata baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili.
“Saikolojia ilikuwepo katika kiwango kikubwa. Hata tukiwa nyuma kwa mabao mawili, wachezaji hawakukata tamaa kabisa. Hili ni jambo chanya sana kwetu,” alisema.
Gamondi pia alisema hana wasiwasi kuhusu maelewano ndani ya kikosi na namna timu inavyojengwa, akibainisha kuwa Taifa Stars ilitawala mchezo licha ya kukosa umakini katika pasi za mwisho.
“Sina wasiwasi na kemistri ya timu na jinsi tunavyojenga kikosi kwani ilikuwa sawa. Tulitawala mchezo, ingawa wakati mwingine tulikosa umakini katika pasi za mwisho,” alisema.
Akizungumzia namna ya kuimarisha safu ya ushambuliaji katika mechi zijazo, Gamondi alisema anatarajia kuwa na baadhi ya wachezaji waliokosekana kutokana na sababu mbalimbali, akiwemo Clement Mzize, Dickson Job na Novatus Dismas.
“Ni wazi tunahitaji wachezaji zaidi katika eneo la usambuliaji. Pengine katika mechi zijazo tutakuwa na Clement, pia tunawasubiri Job na Novatus,” alisema.
Kikosi hicho jana kiliondoka Dar es Salaam kuelekea Morocco kucheza mechi ya pili dhidi ya Madagascar itakayopigwa Septemba 29, mwaka huu nchini humo.
Kuhusu mechi hiyo, Gamondi alisema muda mfupi wa maandalizi pamoja na safari ya kwenda Mji wa Fez nchini Morocco ni miongoni mwa changamoto zitakazoikabili Taifa Stars.
“Tunasafiri kwenda Morocco na tutatumia saa tano kwenye basi kwenda Fez. Tutakuwa na siku moja ya kupumzika na siku moja pekee ya mazoezi. Hakuna muda mwingi wa kubadili mambo, hivyo tutaendelea na mfumo wetu na kujaribu kuboresha,” alisema.
Kocha huyo amesema licha ya muda mfupi wa maandalizi, Taifa Stars itaendelea na mfumo wake huku ikilenga kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Guinea-Bissau, hasa katika pasi za mwisho na matumizi ya nafasi.