Achraf Hakimi kalizua tena huko
Muktasari:
- Waendesha mashtaka wa Ufaransa wametia saini hati ya mwisho ya mashtaka inayopendekeza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 afikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya jinai.
PARIS, UFARANSA: NYOTA wa PSG, Achraf Hakimi, anaripotiwa kukabiliwa na kesi ya ubakaji inayodaiwa kuwa aliifanya baada ya kumwalika mwanamke nyumbani kwake karibu na jijini la Paris.
Waendesha mashtaka wa Ufaransa wametia saini hati ya mwisho ya mashtaka inayopendekeza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 afikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya jinai.
Ijumaa, msemaji wa ofisi ya waendesha mashtaka wa Nanterre alithibitisha kuwa wameomba ‘jaji mpelelezi’€ atoe uamuzi wa kupeleka kesi hiyo mahakamani.
Hii inafuatia hatua ya Hakimi kushtakiwa rasmi kwa ubakaji Machi 03, 2023, na kuachiwa kwa dhamana akiwa chini ya uangalizi wa polisi.
Iwapo atapatikana na hatia, raia huyo wa Morocco anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 jela ambayo ni adhabu ya juu kwa kosa la ubakaji huko Ufaransa.
Kesi hii inahusiana na tukio la Februari 25, 2023. Kwa mujibu wa Le Parisien, mwanamke mwenye umri wa miaka 24 aliiambia polisi kuwa alikutana na Hakimi kupitia Instagram Januari mwaka huo.
Baada ya mawasiliano ya mwezi mmoja, inadaiwa Hakimi alimtumia Uber kumleta nyumbani kwake huko Boulogne-Billancourt.
Mke wake wa zamani ambaye ni muigizaji mwenye asili ya Hispania na Uturuki, Hiba Abouk, 38, alikuwa likizo Dubai na watoto wao wawili wakati huo.
Mwanamke huyo anadai kuwa, alipowasili, Hakimi alianza kumbusu mdomoni na kwenye matiti kupitia nguo zake, licha ya kumkataza.
Anasema kuwa baadaye alimfanyia unyanysaji wa kijinsia bila ridhaa yake na mwanamke huyo anadai aliweza kumsukuma Hakimi kwa kutumia mguu na akakimbia nje, kisha akamtumia rafiki yake ujumbe ili aende amchukue.
Alikwenda kituo cha polisi siku hiyo hiyo kutoa maelezo, ingawa awali alikataa kufungua rasmi kesi.
Baadaye alitoa ujumbe alioutuma kwa rafiki unaoonyesha hali ya mshtuko aliyoipitia baada ya tukio hilo.
Ilipofika Machi 03, 2023, Hakimi alishtakiwa rasmi na kuwekwa chini ya uangalizi wa mahakama lakini yeye mwenyewe amekuwa akikana tuhuma hizo hadi sasa.
Desemba 8, 2023, mwanamke huyo alikabiliana uso kwa uso na Hakimi mbele ya jaji mpelelezi, ambapo aliweza kusisitiza tena madai yake, wakati Hakimi akikataa na kusema hana hatia yoyote.
PSG ilimruhusu Hakimi kukosa mazoezi kwa kile walichokiita “sababu za binafsi.”
Kwa sasa Hakimi yupo likizo huko Puerto Rico pamoja na rafiki yake wa zamani wa PSG, Kylian Mbappe.
Katika mahojiano aliyofanya Januari 2024, Hakimi alidai kuwa kesi hiyo ni njama ya kumuharibia jina:
“Ukweli ni kwamba unapofanikiwa na mambo yako yakienda vizuri, unakuwa mlengwa rahisi kwa watu fulani. Inanifundisha kwamba huwezi kumwamini kila mtu. Walitaka kunibambikizia kesi kwa ajili ya pesa, ndiyo maana tuliwasilisha malalamiko, na mambo yanaenda vizuri. Mahakama imekuwa ya haki.”
Wakati wote wa uchunguzi, Hakimi amedai mwanamke huyo aliyekuwa na miaka 23 wakati wa tukio anajaribu kutaka kumtapeli kwa mamilioni ya pesa.
Mawakili wake wamesema kesi hiyo ni “jaribio la wizi,†huku Hakimi naye akiwasilisha kesi ya madai dhidi ya mwanamke huyo.
Wakili wake, Fanny Colin, alipinga vikali hatua ya sasa ya waendesha mashtaka, akisema:
“Maombi haya hayana mantiki wala msingi wowote ikilinganishwa na ushahidi uliopo.
Yanathibitisha uongo wa mlalamikaji, hasa kupitia tathmini za kisaikolojia zilizofanywa juu yake.
Hakimi na mimi tupo watulivu kama tulivyokuwa tangu mwanzo. Iwapo maombi haya yatakubaliwa, tutakata rufaa kupitia njia zote za kisheria. Kwa sasa Hakimi yuko nje kwa dhamana akisubiri uamuzi wa jaji mpelelezi.”
Msimu uliopita Hakimi alishinda taji la Ligi Kuu Ufaransa pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na PSG.