Abramovic kuipiga bei Chelsea
Muktasari:
- Tajiri huyo inaripotiwa ameiagiza Benki ya America ya Raine Group kusimamia suala la mauzo ya klabu hiyo ya jijini London.
London, England. Tajiri huyo inaripotiwa ameiagiza Benki ya America ya Raine Group kusimamia suala la mauzo ya klabu hiyo ya jijini London.
Uamuzi wa Abramovich kuiuza Chelsea umekuja baada ya siku chache tangu Bilionea huyo wa Russia alipoamua kujiweka kando na maamuzi ya timu pamoja na uendeshaji wake kwa bodi ya hisani ya klabu hiyo ikiwa ni hatua za kuwajibika na kile kinachoendelea kati ya Russia na Ukraine.
Tangu sakata hilo lilipoibuka, kumekuwa na mashinikizo mbalimbali kwa serikali ya Uingereza kumuwajibisha Abramovich na wawekezaji wengine kutoka Russia nchini humo kama njia ya kuonyesha kutounga mkono kile kinachoendelea huko Ulaya Mashariki.
Na Abramovich ndio ameonekana mlengwa mkuu kutokana na ukaribu wake uliopitiliza na Rais wa Russia, Vladimir Putin ambapo baadhi ya wabunge huko England wamekuwa wakishinikiza bilionea huyo atimuliwe nchini mwao na mali zake zishikiliwe.
Tajiri huyo inadaiwa anataka kiasi cha Pauni 3 bilioni (Sh 9.2 Trilioni) ili aiachie klabu hiyo na tayari baadhi ya mabilionea wameanza kuonyesha nia ya kuinunua.
Miongoni mwa matajiri ambao wameonyesha nia ya kuinunua Chelsea kutoka mikononi mwa Abramovich ni bilionea wa Uswizi, Hansjorg Wyss ambaye hata hivyo ameonyesha kushangazwa na kitendo cha bilionea mwenzake kutaka fedha nyingi kwa ajili ya kuiuza Chelsea.