‘Muujiza wa Istanbul’ waigeuka Liverpool
Muktasari:
- Baada ya Alexander Isak kuifungia Liverpool kwa kichwa dakika ya 69 na kuifanya timu yake iongoze kwa mara ya pili, ilionekana wageni hao walikuwa njiani kupata ushindi mkubwa ugenini dhidi ya Fenerbahce.
ISTANBUL, UTURUKI: Liverpool ina historia kubwa ya matokeo ya kishujaa mjini Istanbul, lakini safari hii timu ya Andoni Iraola ilifanya comeback ya aina isiyohitajika.
Baada ya Alexander Isak kuifungia Liverpool kwa kichwa dakika ya 69 na kuifanya timu yake iongoze kwa mara ya pili, ilionekana wageni hao walikuwa njiani kupata ushindi mkubwa ugenini dhidi ya Fenerbahce.
Hata hivyo, Liverpool iliporomoka katika mazingira yenye presha kubwa, huku wenyeji wakiongozwa na kocha wa muda Dirk Kuyt, shujaa wa zamani wa Liverpool, wakigeuza matokeo na kupata ushindi wa kushtukiza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa kufungwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Sukru Saracoglu, Liverpool iliweka rekodi isiyopendeza haijawahi kuongoza kwa kuchelewa kiasi hicho katika mechi kubwa ya Ulaya na hatimaye kufungwa.
Iraola alielezea mabao waliyofungwa kuwa “rahisi” na “ya uzembe”. Baada ya Liverpool kupoteza pointi tatu zilizokuwa mikononi mwake, Kuyt amesema aliwahimiza wachezaji wa Fenerbahce kushikamana na kupambana hadi mwisho, kama Liverpool ilivyofanya katika mafanikio yake makubwa ya Ulaya.
Kuyt alijiunga na Liverpool mwaka 2006, mwaka mmoja baada ya timu hiyo kufanya comeback maarufu ya “Muujiza wa Istanbul” katika fainali ya Ligi ya Mabingwa, na alicheza Anfield kwa miaka sita.
“Tuliambiana tushikamane na kuwa wamoja. Hilo ni jambo nililojifunza kutoka Liverpool, timu tuliyocheza nayo,” amesema Kuyt. “Tumefanya muujiza usiku huu si wengi waliotarajia tushinde.”
Kuyt na Fenerbahce wataukumbuka mchezo huo kwa muda mrefu. Liverpool itataka kuusahau haraka.
Baada ya kushinda mechi tano mfululizo, timu ya Iraola imepoteza mara mbili ndani ya siku nne kwanza dhidi ya Arsenal Jumapili, kisha dhidi ya Fenerbahce.
Katika safari ya kurejea nyumbani kutoka Istanbul, Liverpool itakuwa na mengi ya kujutia kuhusu namna ilivyoshindwa kuumaliza mchezo ikiwa mbele.
“Ni jambo la kukatisha tamaa kwa sababu ni vigumu kuja hapa na kucheza,” amesema Iraola. “Kwa sehemu kubwa ya mchezo tuliamini tunaweza kushinda, lakini haikutokea.”
Mabao yote matatu ya Fenerbahce yalitokana na mipira iliyokufa, na mawili yalifungwa na wachezaji wa England.
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Mason Greenwood, alipata bahati baada ya mpira wake wa adhabu kugonga Jeremy Jacquet na kuingia wavuni kipindi cha kwanza, akisawazisha bao la kwanza la Fenerbahce.
Liverpool ilijilaumu yenyewe kwa bao la pili. Kichwa cha Cody Gakpo kilielekea kwa kipa Alisson, lakini mpira ukamponyoka na kumpa Archie Brown, aliyezaliwa Birmingham, nafasi ya kuusukuma wavuni na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Dakika sita baadaye, Liverpool ilishindwa kuondoa mpira wa juu uliopigwa na Brown ndani ya eneo la hatari. Vedat Muriqi aliwashinda wachezaji watatu wa Liverpool na kufunga kwa kichwa mbele ya Alisson.
“Mabao hayo ni rahisi. Ni mabao ya uzembe,” amesema Iraola.
“Ni mpira wa adhabu, umetoka mbali na umepita kwenye ukuta. Makosa yanaweza kukugharimu. Kwa bao la mwisho, ni mpira mrefu wa kurusha; awamu ya kwanza tuliiweza, lakini baada ya mpira mwingine mrefu, Muriqi aliushinda.
“Kwa bao la pili, Cody ndiye aliyeugusa mpira mbele ya Ali [Alisson]. Uwanjani ilikuwa vigumu sana kuwasiliana kwa sababu kelele zilikuwa nyingi. Hata kwangu ilikuwa vigumu kutoa maelekezo. Nadhani mawasiliano kati ya Ali na Cody yalikuwa magumu.”
LIVERPOOL BADO INA TATIZO LA KUJILINDA
Baada ya kuonyesha dalili za maendeleo katika wiki za karibuni, Liverpool ilipoteza ushindi uliokuwa karibu kwa namna inayotia wasiwasi.
Bao la kwanza la Trey Nyoni akiwa na timu hiyo liliwapa wageni uongozi mapema, lakini shuti lake lililopindishwa na mchezaji wa Fenerbahce lilijibiwa na Greenwood dakika nne baadaye.
Mchezo uliamua zaidi kati ya dakika ya 69 na 79. Liverpool iliongoza tena na kukaribia ushindi wake wa nne mfululizo katika mashindano hayo, lakini haikuweza kulinda matokeo.
“Ni kama kurudi nyuma ukilinganisha na tulichoona dhidi ya Arsenal, kwa sababu kila mtu alifikiri Liverpool ilikuwa ikionyesha maendeleo makubwa,” amesema beki wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock.
“Walikuwa na kikosi kilichobadilishwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, makosa rahisi waliyofanya kwenye mipira iliyokufa au mipira ya kawaida iliyoingia eneo la hatari hayakubaliki.
“Kinachowakatisha tamaa mashabiki wa Liverpool ni kwamba sote tunajua matatizo yao. Suluhisho liko wapi? Hilo ndilo Iraola anajaribu kulipata, lakini swali ni itachukua muda gani.
“Tatizo kubwa ni kwamba hali hii inaendelea kujirudia. Liverpool inaonekana inaweza kufungwa wakati wowote na inakuwa wazi sana inaposhambuliwa kwa kushtukiza. Mabao wanayofungwa yanafanana na yanaharibu kazi nzuri wanayofanya wanaposhambulia.
“Unapoongoza mara mbili ugenini dhidi ya Fenerbahce kwenye Ligi ya Mabingwa, timu kama Arsenal ingeweza kushinda na kulinda matokeo dhidi ya mpinzani wa aina hiyo.
“Kwa sasa Liverpool haina uwezo huo, na hilo ndilo linalokatisha tamaa zaidi.”