Mabao 44 yafungwa usiku mmoja UEFA, Como yaweka rekodi
Muktasari:
- Wakati Como ikituma ujumbe mzito kwa vigogo wa Ulaya, Real Madrid ilihitaji bao la dakika za nyongeza kuibuka na ushindi, Liverpool ikaangushwa nchini Uturuki, huku Manchester City na Arsenal zikiondoka na pointi tatu ugenini.
LENS, UFARANSA: USIKU wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League), umekuwa wa kipekee kufuatia matokeo ya kushangaza na rekodi zilizowekwa baada ya mabao 44 kupatikana katika mechi tisa zilizochezwa Novemba 4, 2026, huku Como ya kocha Cesc Fabregas ikiteka shoo kwa ushindi wake wa kutisha wa mabao 9-1 dhidi ya Lens ikiwa ugenini.
Wakati Como ikituma ujumbe mzito kwa vigogo wa Ulaya, Real Madrid ilihitaji bao la dakika za nyongeza kuibuka na ushindi, Liverpool ikaangushwa nchini Uturuki, huku Manchester City na Arsenal zikiondoka na pointi tatu ugenini.
LENS 1-9 COMO
Como imeandika moja ya matokeo makubwa zaidi ya usiku huo baada ya kuichapa Lens mabao 9-1 nchini Ufaransa.
Timu hiyo inayofundishwa na Fabregas, haikuonyesha huruma, ikitumia kwa kiwango kikubwa nafasi ilizopata mbele ya lango la wenyeji, huku mshambuliaji Anastasios Douvikas akionyesha kiwango cha juu kwa kufunga hat-trick.
Douvikas alianza kuandika mabao dakika ya saba, akaongeza la pili dakika ya 32 na kukamilisha hat-trick dakika ya 57. Nico Paz alifunga dakika ya 40, Lucas Da Cunha dakika ya 47, Marc-Oliver Kempf dakika ya 53, Mattia Liberali dakika ya 62 na Martin Baturina dakika ya 69, kabla ya Matteo Papaccioli kufunga la tisa dakika ya 90+1.
Kwa upande wa Lens, Ruben Aguilar ndiye aliyefunga bao lao pekee dakika ya 65.
Ushindi huo umeifanya Como kuwa gumzo kubwa Ulaya, ikipeleka ujumbe kwamba haipo kwenye mashindano hayo kwa ajili ya kujifunza, bali kupambana na timu yoyote.
Pia, kwa ushindi huo, Como imeweka historia ya kuwa timu ya kwanza kufunga mabao tisa ugenini katika mashindano makubwa ya Ulaya tangu Feyenoord ilipoichapa Olympiakos Nicosia mabao 9-0 mwaka 1971.
AEK ATHENS 2-3 REAL MADRID
Real Madrid ililazimika kupambana hadi dakika za mwisho kuondoka na pointi tatu dhidi ya AEK Athens.
AEK ilianza kwa kasi na kupata bao kupitia Aboubakary Koita dakika ya 12, lakini Jude Bellingham akaisawazishia Real dakika ya 32.
Kipindi cha pili, wenyeji walipata bao la pili kupitia Stavros Pilios dakika ya 75 na kuifanya Real kuwa katika wakati mgumu.
Hata hivyo, Kylian Mbappe alisawazisha dakika ya 78 kabla ya Federico Valverde kuamua mchezo kwa bao la ushindi dakika ya 90+2.
Mchezo huo pia ulimshuhudia Koita akionyeshwa kadi nyekundu katika dakika za nyongeza.
Matokeo hayo yameifanya Real Madrid kufikisha pointi 12 baada ya mechi nne na kuendelea kushika nafasi ya pili katika msimamo.
FENERBAHCE 3-2 LIVERPOOL
Liverpool imepata pigo kubwa mjini Istanbul baada ya kufungwa mabao 3-2 na Fenerbahce.
Liverpool ilitangulia kupitia Trey Nyoni dakika ya 25, lakini Mason Greenwood akaisawazishia Fenerbahce dakika ya 29 kwa mkwaju wa adhabu.
Kipindi cha pili, Alexander Isak aliyeingia akitokea benchi aliirejeshea Liverpool uongozi dakika ya 69.
Hata hivyo, Archie Brown alisawazisha dakika ya 73 kabla ya Vedat Muriqi kufunga bao la ushindi dakika ya 79.
Matokeo hayo yamekatisha mwanzo mzuri wa Liverpool katika mashindano hayo, huku Fenerbahce ikipata ushindi muhimu mbele ya mashabiki wake.
DORTMUND 2-1 BETIS
Borussia Dortmund iliendelea kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani baada ya kuichapa Real Betis mabao 2-1.
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila mabao, Fabio Silva aliwapa Dortmund uongozi dakika ya 49.
Real Betis ilisawazisha kupitia Aitor Ruibal dakika ya 67, lakini furaha yao haikudumu muda mrefu baada ya Konstantinos Karetsas kufunga bao la ushindi dakika ya 72.
Karetsas alikuwa ameingia akitokea benchi na kuibuka shujaa wa Dortmund katika mchezo huo.
Ushindi huo umeifanya Dortmund kufikisha pointi tisa baada ya mechi nne na kuendelea kupambana kuwania nafasi nane za juu.
FC PORTO 4-1 NAPOLI
FC Porto imeonyesha makali yake nyumbani baada ya kuichapa Napoli mabao 4-1 katika mchezo uliokuwa na mabadiliko ya matokeo.
Jan Bednarek alianza kuifungia Porto dakika ya 11, lakini Scott McTominay akaisawazishia Napoli dakika ya 43 na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili Porto iliongeza kasi na Gabri Veiga akaifungia bao la pili dakika ya 73, kabla ya Jakub Kiwior kuongeza la tatu dakika ya 80.
Samu Aghehowa alikamilisha ushindi huo kwa kufunga bao la nne kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 90+1.
Matokeo hayo yameipa Porto ushindi wake wa kwanza katika hatua ya ligi ya mashindano hayo msimu huu.
PSV 1-2 CLUB BRUGGE
Club Brugge imeondoka Uholanzi na ushindi wa thamani baada ya kuifunga PSV Eindhoven mabao 2-1.
Nicolò Tresoldi aliipa Brugge uongozi dakika ya 25, lakini PSV ikasawazisha kupitia Kodai Sano dakika ya 54.
Hata hivyo, Carlos Forbs aliihakikishia Club Brugge ushindi kwa kufunga bao la pili dakika ya 65.
Ushindi huo wa ugenini umeifanya Club Brugge kuendelea kuimarisha nafasi yake katika mbio za kusaka tiketi ya hatua inayofuata.
RB LEIPZIG 2-3 MAN CITY
Manchester City ililazimika kufanya kazi kubwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya RB Leipzig.
City ilipata bao la kwanza dakika ya 37 kupitia mchezaji wa Leipzig, Castello Lukeba, aliyejifunga wakati akijaribu kuokoa hatari langoni mwake.
Leipzig ilisawazisha kupitia Ridle Baku dakika ya 49, lakini Enzo Fernandez akairejeshea City uongozi dakika ya 58.
Antonio Nusa aliisawazishia Leipzig tena dakika ya 61, kabla ya Erling Haaland kufunga bao la ushindi dakika ya 78 akimalizia pasi ya Elliot Anderson.
SLAVIA PRAGUE 1-2 ARSENAL
Arsenal nayo imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Slavia Prague, wenyeji walifanikiwa kupata bao lao mwishoni mwa mchezo.
Noni Madueke aliipa Arsenal uongozi dakika ya tisa akimalizia pasi ya Viktor Gyokeres, kabla ya mshambuliaji huyo wa Sweden kuongeza bao la pili dakika ya 38 akimalizia vizuri muunganiko na Mikel Merino.
Slavia Prague haikukata tamaa na ilipambana hadi dakika za mwisho, Wiktor Nowak akifunga bao lao dakika ya 90+1.
Licha ya kufungwa, Slavia ilipata jambo la kusherehekea kwa kufunga bao katika kampeni hiyo ya Champions League, huku Arsenal ikifikisha pointi 10 baada ya mechi nne.
Hata hivyo, Slavia Prague imeendeleza rekodi mbaya ya kutoshinda katika mechi 23 za mashindano ya Ulaya, ikilingana na rekodi zilizowekwa na AEK Athens (1989-2006) na FCSB (2006-2013).
VIKING 4-1 SABAH
Katika mchezo mwingine wa usiku huo, Viking ya Norway iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Sabah ya Azerbaijan baada ya kuanza ikiwa nyuma kwa bao moja.
Orphé Mbina aliwapa Sabah uongozi dakika ya 11, lakini Erik Botheim akaisawazishia Viking dakika ya 27 na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya 1-1.
Kipindi cha pili Viking ilirejea kwa nguvu na Zlatko Tripic kufunga bao la pili dakika ya 69, kabla ya Henrik Falchener kuongeza la tatu dakika ya 81.
Botheim alikamilisha ushindi huo kwa kufunga bao lake la pili na la nne kwa Viking dakika ya 90+4.
Sabah ilipata pigo lingine baada ya mchezaji wake Aden McCarthy kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 78.
Ushindi huo ulikuwa muhimu kwa Viking katika harakati zake za kuimarisha nafasi yake kwenye msimamo, huku Sabah ikishindwa kuzuia kasi ya wenyeji.
MATOKEO YA NOVEMBA 4, 2026
AEK Athens 2-3 Real Madrid
Fenerbahce 3-2 Liverpool
Dortmund 2-1 Betis
FC Porto 4-1 Napoli
Lens 1-9 Como
PSV 1-2 Club Brugge
RB Leipzig 2-3 Man City
Slavia Prague 1-2 Arsenal
Viking 4-1 Sabah