MILELE...Mastaa bado wapo sana
Muktasari:
- Hiyo imemfanya kuwa mchezaji mwenye mkataba wa muda mrefu zaidi katika ligi tano bora barani Ulaya na anayelipwa zaidi katika ligi hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: HIVI karibuni straika wa Manchester City, Erling Haaland alisaini mkataba mpya wa miaka tisa utakaomwezesha kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2034.
Hiyo imemfanya kuwa mchezaji mwenye mkataba wa muda mrefu zaidi katika ligi tano bora barani Ulaya na anayelipwa zaidi katika ligi hiyo.
Mbali ya yeye, pia kuna orodha ya wachezai wengine watano ambao wana mikataba ya muda mrefu zaidi katika ligi hizo tano na hapa tumekuletea mastaa hao na takwimu zao kwa msimu huu.
5. Oihan Sancet
Ni zao la akademi ya Athletic Bilbao na yupo katika orodha hii akiwa na mkataba wa miaka minane unaotarajiwa kumalizika mwaka 2032.
Kwa sasa anasumbuliwa na majeraha aliyoyapata tangu kuanza kwa msimu huu na amecheza mechi 20 za michuano yote na kufunga mabao manane akiwa mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Bilbao.
Licha ya urefu wa mkataba wake, timu nyingi barani Ulaya zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kutokana na kiwango chake.
4. Dani Vivian
Fundi mwingine kutoka Athletic Bilbao ambaye ana mkataba mrefu. Ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na alipandishwa akitokea kikosi chao cha akiba.
Vivian ambaye mkataba wake pia unamalizika mwaka 2032, msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote na licha ya kuwa beki wa kati pia ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga, akitupia kambani mara tatu.
3. NicolAus Jackson
Ana mkataba unaomwezesha kusalia kwenye viunga vya darajani kwa miaka minane kuanzia mwaka huu.
Ni mmoja wa wachezaji tegemeo Chelsea na msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote, amefunga mabao tisa na kutoa asisti nne.
Mkataba huu alisaini mwaka 2023 alipojiunga nao akitokea Villarreal ya Hispania dirisha la majira ya kiangazi kwa ada ya Euro 37 milioni.
2. Cole Palmer
Alisaini dili hili mwaka 2023, alipojiunga na matajiri wa darajani kwa ada ya uhamisho ya Euro 47 milioni.
Ana mkataba wa miaka minane ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2033 na amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Man City.
Msimu huu amecheza mechi 24 za michuano yote, amefunga mabao 14 na kutoa asisti sita akiwa mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Chelsea.
Licha ya wingi wa wachezaji staa huyu amekuwa chaguo la kwanza katika safu ya ushambuliaji chini ya Enzo Maresca.
1. Erling Haaland
Amesaini mkataba mpya utakaomfanya kukaa kwenye viunga hivyo kwa miaka tisa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2034.
Staa huyu wa kimataifa wa Norway, mbali ya kuwa na mkataba mrefu zaidi kuliko mchezaji yoyote barani Ulaya, pia anakunja mshahara mkubwa wa Pauni 525,000 ambao unamfanya kuwa mchezaji anayekunja mkwanja mrefu zaidi kwenye ligi tano bora barani Ulaya.
Haaland alisainishwa mkataba mpya baada ya kiwango bora alichoonyesha tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2022 akiisaidia timu hiyo kushinda mataji mbalimbali ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya.