Simba yabeba kiungo Mkenya
Muktasari:
- Taarifa kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa nyota huyo amemaliza mkataba wake na Police Bullets na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Tanzania.
SIMBA Queens imeendelea kujiimarisha kuelekea msimu mpya baada ya kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo Mkenya, Diana Wacera kutoka kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Kenya, Kenya Police Bullets.
Taarifa kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa nyota huyo amemaliza mkataba wake na Police Bullets na amekubali kusaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao wa Tanzania.
Wacera ni mmoja wa viungo wenye uzoefu mkubwa katika Ligi ya Kenya na pia ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakitegemewa na kikosi cha timu ya taifa Harambee Starlets. Huo ni mkakati wa Simba Queens kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kinachojiandaa na mashindano ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake ambayo yatafanyika mwezi ujao nchini Rwanda.
Nyota huyo anasajiliwa ili kuziba nafasi ya Odama Amarachi ambaye amepewa mkono wa kwaheri na Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kutoonyesha ushindani mkubwa.
Wacera anatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa kwenye eneo la kiungo kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kutoa pasi za mwisho na kusaidia safu ya ulinzi. Mwanaspoti linafahamu kuwa viongozi wa mchezaji huyo wanashighulikia ITC yake na mambo yakikamilika mapema kiungo huyo atamwaga wino.
“Siwezi kuzungumza kwa sababu kuna mambo hayakamilika hususani kwenye ITC yake nafikiri hadi wiki ijayo mambo yatakuwa sawa,” amesema mmoja wa viongozi wachezaji huyo.