TRA United inasaka ushindi wa kwanza Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Hiyo ni raundi ya tano ya Ligi Kuu Bara na kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, saa 10:00 jioni, mechi hiyo itachezwa, kisha saa 1:00 usiku, Dodoma Jiji itaikabili Mashujaa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
KATI ya timu ambazo zinaumiza kichwa kuweka vizuri mikakati yao katika Ligi Kuu Bara ili kupata ushindi wa kwanza, TRA United inayofundishwa na Etienne Ndayiragije ni mojawapo na leo Ijumaa, ina kibarua nyumbani dhidi ya Mbeya City.
Hiyo ni raundi ya tano ya Ligi Kuu Bara na kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, saa 10:00 jioni, mechi hiyo itachezwa, kisha saa 1:00 usiku, Dodoma Jiji itaikabili Mashujaa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mechi zote zinaonekana kuwa na uzito mkubwa kutokana na hali ya timu hizo kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, TRA bado inatafuta ushindi wake wa kwanza, wakati Mbeya City imeanza msimu kwa kasi na tayari imekusanya pointi tisa ikishinda mechi tatu na kupoteza moja.
TRA United inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo, ikikusanya pointi mbili baada ya mechi nne baada ya sare mbili na kupoteza mbili. Timu hiyo haijapata ushindi hadi sasa.
Mechi ya mwisho ni dhidi ya Dodoma Jiji Agosti 29, 2026 na ilipoteza kwa bao 1-0. Kabla ya hapo, TRA ilitoka sare ya 1-1 na Coastal Union, ikafungwa 2-1 na Azam. Kumbuka ilianza msimu kwa sare ya 1-1 dhidi ya JKT Tanzania.
Mbeya City iko kwenye nafasi nzuri zaidi ambayo ni ya tano ikiwa na pointi tisa baada ya mechi nne, ikiwa imeshinda tatu na kupoteza moja. Imefunga mabao sita na kufungwa mawili.
Kikosi hicho kilianza kwa kupoteza 1-0 dhidi ya Geita Gold, lakini kikafuata ushindi wa 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji, 2-1 dhidi ya Mashujaa na 2-0 dhidi ya Fountain Gate.
Mbeya City pia ina rekodi nzuri dhidi ya TRA katika mechi za karibuni na ya mwisho, Juni 30, 2026 uliisha kwa sare ya 0-0, huku Mbeya City ikiishinda 2-0 zilipokutana Februari 7, 2026.
Kocha wa Mbeya City, Salum Mayanga amesema maandalizi yao ni mazuri na wachezaji wawili watakosekana kutokana na majeraha.
“Baraka Maranyingi na Aziz Kada bado wanaendelea na matibabu, hivyo watakosa mechi ya kesho (leo) na TRA ni timu bora, hivyo tutacheza kama ambavyo huwa tunacheza,” amesema Mayanga.
Kwa upande wa mchezaji wa Mbeya City, Baraka Maranyingi, amesema wanaishi kwenye malengo waliyopanga na mafunzo ya kocha wao na muhimu kwao kupata pointi tatu.
Kocha wa TRA, Etienne Ndayiragije amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kucheza na moja ya timu ngumu kwenye ligi.
“Mbeya wameanza vizuri sana, ni timu inayoshambulia na wako vizuri kwenye kulinda, hatujaanza vizuri nyumbani, lakini tunaamini tutacheza vizuri kesho (leo),” amesema Ndayiragije.
Pia nahodha wa TRA, Nasri Kombo amesema hawatokata tamaa kwa matokeo waliyoyapata katika mechi zilizopita.
DODOMA JIJI VS MASHUJAA
Dodoma Jiji iko nafasi ya 10 ikiwa na pointi nne baada ya mechi nne. Imefungwa mbili, imeshinda moja na sare moja.
Cha kuipa matumaini ni mechi ya mwisho na ilishinda 1-0 dhidi ya TRA United Agosti 29, 2026.
Kabla ya hapo, Dodoma Jiji ilipoteza 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, ikafungwa 2-0 na Mbeya City na sare ya 1-1 na Pamba Jiji.
Mashujaa iko nafasi ya nane ikiwa na pointi sita. Imecheza mechi nne, ikishinda mbili na kupoteza mbili. Imefunga mabao manne na kufungwa manne.
Vijana hao kutoka Kigoma, walianza msimu vizuri baada ya kuishinda Fountain Gate bao 1-0, lakini ikapoteza 2-1 dhidi ya Mbeya City. Baadaye waliamka na kuishinda Kagera Sugar 2-1.
Kwa hiyo, Mashujaa nayo inaingia ikiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mechi ya mwisho na haitakuwa tayari kuipa Dodoma Jiji nafasi kirahisi.
Katika mchezo wao wa mwisho wa ligi msimu uliopita, Dodoma Jiji na Mashujaa zilitoka sare ya 1-1, Mei 20, 2026. Kabla ya hapo, zilitoka 0-0 Novemba 28, 2025.
Kocha wa Dodoma Jiji, Vicent Mashani amesema wanatambua ubora wa Mashujaa lakini wamejiandaa vizuri na wanahitaji kutumia faida ya kucheza nyumbani kupata pointi tatu na kurejesha morali ya kikosi.
“Mashujaa ni timu nzuri na tunaiheshimu, lakini sisi tumejiandaa vizuri kwa mechi hii. Tunajua tunacheza nyumbani na kupata pointi tatu ni muhimu kwetu. Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Mashami.
Kocha wa Mashuja, Amani Josiah ambaye anakutana na Dodoma Jiji kwa mara ya kwanza tangu aondoke alipoiongoza msimu wa 2025-2026 akifanya kazi na Mashami, amesema ana furaha kukutana na Dodoma Jiji na anamini ni timu imara sana kwenye ligi kuu.
“Mashujaa bado ni timu inayojitengeneza na tumejiandaa vizuri na hii mechi kuanzia mazoezi na saikoloji ya wachezaji, hivyo naamini tutapata matokeo mazuri.” amesema Josiah.