Kutoka Wema Sepetu hadi Maua Sama, nyuma ya pazia kuna nini?
Muktasari:
- Kuanzia kwa mwigizaji Wema Sepetu, ambaye safari yake ya kuwa mama imekuwa ikifuatiliwa kwa miaka, kisha mwanamuziki Zuchu aliyejifungua mtoto wake wa kwanza na Diamond Platnumz, hadi Maua Sama, mastaa hao wameingia kwenye ukurasa mpya wa maisha huku kila mmoja akiacha gumzo lake.
MWAKA 2026 umeendelea kuandikwa kwa matukio mbalimbali katika ulimwengu wa burudani, lakini safari za uzazi za baadhi ya mastaa wa Bongo Muvi na Bongo Fleva, zimekuwa miongoni mwa simulizi zilizowavuta mashabiki kwa namna ya kipekee.
Kuanzia kwa mwigizaji Wema Sepetu, ambaye safari yake ya kuwa mama imekuwa ikifuatiliwa kwa miaka, kisha mwanamuziki Zuchu aliyejifungua mtoto wake wa kwanza na Diamond Platnumz, hadi Maua Sama, mastaa hao wameingia kwenye ukurasa mpya wa maisha huku kila mmoja akiacha gumzo lake.
Mwigizaji Chuchu Hans naye amepokea mtoto mwingine katika familia yake na Vincent Kigosi ‘Ray’, huku mwanamuziki Maua Sama akiwa ameongeza jina lake kwenye orodha hiyo baada ya kutangaza kupata mtoto wa kike Septemba hii.
Lakini hapa si suala la nani kajifungua, bali ni namna ujio wa watoto hao ulivyogeuka kuwa habari kubwa na gumzo kwa mashabiki, huku nyuma ya pazia watu wanajiuliza imekuaje mfululizo huo wa mastaa kujifungua.
WEMA SEPETU
Kwa Wema Sepetu, habari ya kujifungua haikuwa habari ya kawaida. Kwa miaka kadhaa, maisha yake yalikuwa yakifuatiliwa na mashabiki kuhusu suala la kupata mtoto, huku yeye mwenyewe katika vipindi tofauti akizungumza kuhusu ndoto yake ya kuwa mama.
Hatimaye, Juni 12, 2026, habari kubwa ikavuma kwamba Wema amejifungua mtoto wa kiume. Kilichofanya habari hiyo iwe na uzito zaidi ni historia iliyokuwa nyuma yake.
ZUCHU
Agosti 2, 2026, ilikuwa siku nyingine kubwa kwa mashabiki wa Bongo Fleva.
Zuchu na Diamond Platnumz walipokea mtoto wao wa kwanza wa kike, habari ambayo ilithibitishwa na familia na kupewa nguvu zaidi baada ya Diamond kuweka picha ya Zuchu akiwa hospitalini baada ya kujifungua.
Jina Sanura lilitajwa katika taarifa mbalimbali, likihusishwa na jina la mama mzazi wa Diamond, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’.
Kwa Zuchu, Agosti haikuwa tu mwezi wa kuachia au kusikiliza muziki wake; ilikuwa mwezi ambao aliingia rasmi kwenye maisha ya umama.
CHUCHU HANS
Wakati gumzo la Zuchu likiwa bado linaendelea, upande wa Bongo Muvi nao ulikuwa na habari yake.
Chuchu Hans na Vincent Kigosi ‘Ray’ walitajwa kuwa wamepokea mtoto wao wa pili, huku taarifa za mitandaoni zikieleza kuwa mtoto huyo wa kike alizaliwa mwishoni mwa Agosti 2026.
MAUA SAMA
Septemba 2026 Maua Sama naye akaingia kwenye orodha ya mastaa waliopokea baraka ya mtoto.
Mwanamuziki huyo alitangaza Septemba 2 kupata mtoto wa kike na kufanya habari hiyo kuwa miongoni mwa taarifa mpya zaidi za uzazi katika burudani kwa sasa.
Kwa Maua, safari hii ilikuwa tofauti kwa sababu ujio wa mtoto uliingia sambamba na hatua mpya kabisa katika maisha yake binafsi.
SWALI LIKO HAPA
Ukiweka kumbukumbu sawa utapata muda wa lini mimba hizo ziliingia kwa mastaa hao, kwani hesabu za kibaiolojia zinaonyesha kwamba, ili mwanamke aweze kupata mtoto, kwa hali ya kawaida anatakiwa kubeba ujauzito kwa miezi tisa. Wakati mwingine inatokea chini ya miezi hiyo lakini inakuwa kwa dharura.
Namna mastaa hao walivyojifungua sasa, bila shaka huenda walipata ujauzito kuanzia Oktoba 2025 mpaka mwanzoni mwa Novemba 2025, kipindi ambacho Taifa lilikuwa chini ya uangalizi, huku kila raia akilazimika kukaa ndani kwake kwa sababu za kiusalama.