Zimamoto Zanzibar yajipanga AFCON 2027
NAIBU Kamishna wa Zimamoto na Uokoaji Zanzibar, Mrisho Iddi Mbaraka, amesema kikosi hicho kimejipanga kuhakikisha huduma za uokozi na dharura zinapatikana kwa urahisi wakati wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Amesema katika kufanikisha hilo, tayari Zimamoto imeweka kituo maalumu katika eneo la Fumba kwa ajili ya kutoa huduma za dharura zitakazohitajika kabla, wakati na baada ya mashindano hayo.
Amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa wachezaji, viongozi na mashabiki wakati wote wa michuano hiyo, ambayo pia inatarajiwa kuongeza fursa za kuitangaza Zanzibar kupitia utalii.
“Tayari Zimamoto tumeweka kituo maalumu Fumba kwa ajili ya kutoa huduma za dharura zitakazojitokeza kabla, wakati na baada ya mashindano hayo,” amesema.
Ameongeza kuwa kikosi hicho kinapanga kuwajengea uwezo na kutoa mafunzo maalumu ya kiutendaji kwa maofisa na askari watakaohusika na masuala ya usalama wakati wa mashindano hayo ili waweze kukabiliana na majanga ya aina mbalimbali kwa weledi.
Pia, Naibu Kamishna huyo aliwahakikishia wananchi na wageni watakaowasili Zanzibar kuwa usalama wa maisha na mali zao umepewa kipaumbele, huku akiwataka kufuata taratibu na maelekezo ya kiusalama wanapokuwa viwanjani.
Kauli ya kamishna huyo imekuja ikiwa imesalia takribani miezi saba kabla ya kuanza kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) zitakazofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.