Karia atoa neno ukaguzi viwanja vya AFCON 2027
Muktasari:
- Kwa Tanzania, mbali na Fumba, viwanja vingine vitakavyotumika kwa mechi za AFCON 2027 ni Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam na Samia Suluhu Hassan unaoendelea kujengwa jijini Arusha.
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeridhishwa na maendeleo ya viwanja vya hapa nchini vitakavyotumika kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027).
Karia ameyasema hayo leo Novemba 1, 2026 katika ziara ya Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adamu wakati alipotembelea Uwanja wa Fumba unaoendelea kujengwa Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja.
Amesema hatua ya uwanja huo umefikia pazuri na unategemewa kukamilika ifikapo Desemba 31, 2026.
Rais huyo alisema Tanzania imepata fursa na baraka kwani mambo mengi yamefanyika kuelekea maandalizi ya AFCON 2027, hivyo wananchi wasikae nyuma, bali wanapaswa kuichangamkia fursa hiyo.
"Tanzania tuko vizuri na hilo linaonekana kupitia nyuso zao wanaokuja kufanya ziara nchini, hivyo AFCON imetulea mambo mazuri," amesema.
Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, amesema CAF imesisitiza kuendelea kujipanga na kufanyakazi kwa bidii ili itakapofika muda wa kukabidhi wawe tayari.
Amesema, viwanja vyote bado havijafikia asilimia 100 ya ujenzi wake, lakini vinaendelea vizuri na uwezo wa kumaliza kwa wakati unawezekana.
Kwa upande wake, Kamishna wa Michezo Zanzibar, Ameir Mohamed Makame, amesema ujio huo ni faraja upande wao kwani unawapa hamasa ya kuongeza bidii ya kufanyakazi inavyopaswa.
Amesema, kwa sasa uwanja huo unaendelea na kazi za ndani ikiwemo kuweka umeme, tiles, mabomba ya maji taka na safi pamoja na umaliziaji wa uwekaji wa paa.
Uwanja wa Fumba unaojengwa na kampuni ya Orkum Group ya nchini Uturuki, hadi sasa umefika asilia 87 ya ujenzi wake ambapo unatarajiwa kutumika katika Fainali za AFCON 2027 zitakazofanyika Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Kwa Tanzania, mbali na Fumba, viwanja vingine vitakavyotumika kwa mechi za AFCON 2027 ni Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam na Samia Suluhu Hassan unaoendelea kujengwa jijini Arusha.