Yoyote aje tu! Gomes kiroho safi
Muktasari:
MASHABIKI wa Simba wanahesabu saa tu kabla ya leo jioni kujua chama lao litavaana nani kwenye mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati droo ya hatua hiyo itakapofanyika jijini Cairo, Misri huku Kocha Didier Gomes akisisitiza yeyote atakayepangwa nao kwake freshi tu.
MASHABIKI wa Simba wanahesabu saa tu kabla ya leo jioni kujua chama lao litavaana nani kwenye mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati droo ya hatua hiyo itakapofanyika jijini Cairo, Misri huku Kocha Didier Gomes akisisitiza yeyote atakayepangwa nao kwake freshi tu.
Droo hiyo itakayohusisha pia robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itafanyika saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki ambapo Simba itajua kama itavaana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, MC Alger au CR Boulizdad za Algeria.
Mapema tu kocha Gomes, alisema kwa hatua aliyofikia ya kufika robo fainali hana presha na timu yoyote, kwani akipangwa na Wasauzi au Waarabu yeye freshi tu, kwa vile kikosi chake kimeshajiandaa mapema kukutana na timu yoyote.
“Muhimu kwetu ilikuwa ni kumaliza kundi kama vinara na sasa tuna hakika ya kucheza mechi ya awali ugenini na kumalizia nyumbani, hatuhofii timu yoyote tutakayopangiwa,” alisema Gomes na kusisitiza kwa kufika robo fainali, kiu yao sasa ni kuona wanavuka hadi nusu fainali ya Afrika.
Simba ilifika hatua ya nusu fainali mara ya kwanza na mwisho ikiwa klabu pekee ya Tanzania mwaka 1974 wakati michuano hiyo ya Afrika ikiitwa Klabu Bingwa.
Mbali na Simba iliyoongoza Kundi A, timu nyingine zilizofuzu hatua hiyo ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco na Esperance ya Tunisia zilizoongoza makundi ya B, C na D, huku Al Ahly ya Misri nayo ipo katika kapu moja na timu za Kaizer, MC Alger na CRB.
Kaizer Chiefs ilimaliza katika nafasi ya pili katika Kundi C ikiwa na alama 9 na ni timu tishio ikiwa na nyota ambao Simba inapaswa kuwa makini nao kama itatokea droo hiyo ya leo itawakutanisha.
Nyota kama Khama Billiat mwenye umri wa miaka 30 na kimo cha Sentimita180 ni hatari kama ilivyo kwa Bernard Parker, mshambuliaji wa Afrika Kusini mwenye miaka 35 na kimo cha sm 170.
Mbali na hao Kaizer pia ina wakali wengine ambao ni lazima vijana wa Gomes wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kukabiliana nao.
Mbali na hao pia ndani ya CR Boulizdad, kuna majembe mengine matata wakiwamo mshambuliaji Amir Sayoud mwenye mabao matatu kwa sasa akiwa na umri wa miaka 30 na beki Mohamed Sofiane Bouchar mwenye miaka 26 ambaye kina Luis Miquissone, Chriss Mugalu, Francis Kahata na Clatous Chama na wenzake ni lazima wajipange kwelikweli kukabiliana naye.
Kwa upande wa MC Alger mabingwa wa zamani wa Afrika 1976 yenye nayo sio timu ya kubezwa kwani ni timu yenye kujaa vipaji, lakini ikiwategemea zaidi wakali kadhaa akiwamo kipa wake Abdelkader Salhi, aliyeruhusu mabao manne tu katika michuano ya msimu huu sambamba na beki wake Mouad Haddad.
Hata hivyo, Simba inajivunia wakali walioipaisha hadi hatua hiyo ikiwa ni mara yao ya pili ndani ya misimu mitatu, kwani 2018-2019 ilitinga na kung’olewa na TP Mazembe ya DR Congo. Mechi za robo fainali zitapigwa kati ya Mei 14-22 kabla ya zitakazovuka kuvaana nusu fainali itakayopangwa leo pia sambamba na ile ya fainali.
Baadhi ya wadau wa soka wameliambia Mwanaspoti kuwa, kwa Simba hii ilivyo yeyote anapasuka kama Wekundu hao watakomaa nje ndani.
Wachambuzi maarufu wa michezo nchini, Ally Mayay na Mwalimu Kashasha wameipa nafasi kubwa Simba ya kushinda mbele ya mpinzani yeyote watakayepangwa naye kati ya watatu hao.
“Timu hizo tatu sio mbaya, ila Simba kwa sasa imejengeka kwa kila idara, pili wana faida ya kuanzia mechi ya kwanza ugenini hiyo itawasaidia endapo wataingia na lengo zuri la kujilinda na kutafuta ushindi kama walivyofanya dhidi ya AS Vita ugenini kwenye hatua ya Makundi, naamini watasonga mbele,” alisema Mayay huku Kashasha akiongeza kwa kusema;
“Nimetazama mechi za hao wapinzani wa Simba, kila mmoja ana ubora na madhaifu yake lakini bado naipa Simba nafasi kubwa.”