Gomes apiga mkwara mapema
Muktasari:
YANGA mpo?! Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amekiangalia kikosi chake kisha akakilinganisha na kile cha watani wao, Yanga na kujikuta akitabasamu kabla ya kuchimba mkwara kwamba Mei 8 kitaeleweka kwa kuwa amepania kupata ushindi ili kukamilisha lengo lao msimu huu.
YANGA mpo?! Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes amekiangalia kikosi chake kisha akakilinganisha na kile cha watani wao, Yanga na kujikuta akitabasamu kabla ya kuchimba mkwara kwamba Mei 8 kitaeleweka kwa kuwa amepania kupata ushindi ili kukamilisha lengo lao msimu huu.
Gomes ameliambia Mwanaspoti anajua ugumu wa pambano la watani, lakini anaamini huo ndio mchezo ambao utawafungulia njia ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo, lakini akisema anataka kumalizana kabisa na Kagera Sugar kwenye michuano ya ASFC.
Simba itaikaribisha Kagera kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wikiendi hii katika mfululizo wa mechi za 16 bora ya michuano hiyo ya shirikisho ambayo Wekundu hao ni watetezi kabla ya kujiweka sawa kumalizana na Yanga katika Kariakoo Derby kwenye uwanja huo, Mei 8.
Kocha huyo Mfaransa alisema baada ya matokeo mazuri kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa sasa anataka kuichapa Yanga ili kujisafishia njia ya ubingwa msimu huu kwani ushindi huo utaweka pengo kubwa la pointi kileleni.
Gomes alisema licha ya kuongoza msimamo kwa sasa, lakini ushindi dhidi ya Yanga utakuwa mtamu zaidi kwani utaongeza pengo la pointi kutoka nne kwa sasa hadi saba na kuwarahisishia kazi ya kutetea ubingwa wanaoushikilia kwa misimu mitatu mfululizo tangu 2017-2018.
Simba inaongoza msimamo kwa sasa ikiwa na pointi 61 baada ya juzi kuichapa Dodoma Jiji mabao 3-1, ikizidi kujikita kileleni tangu waiengue Yanga yenye pointi 57, huku ikiwa imecheza michezo miwili zaidi ya Wekundu hao. Yanga imecheza michezo 27, ilhali Simba ikicheza 25.
“Nilishawahi kusema kila mechi iliyopo mbele yetu ni kama fainali, hivyo mchezo unaofuata wa ligi tutacheza na Yanga na tutacheza kama fainali. Nimefuatilia wanavyocheza, ni timu ngumu na yenye morali pia. Nimeona zinapokutana Yanga na Simba unakuwa mchezo wenye kuacha historia kubwa kwani ndio timu kubwa hapa nchini,” alisema Gomes.
“Nawaheshimu na natambua wapo nyuma yetu kwa alama nne, hivyo watahitaji ushindi kutusogelea, ila tunatarajia kucheza soka letu la kila siku kwa lengo la kupata ushindi dhidi yao. Hata wachezaji wanatambua umuhimu na ugumu wa mechi hiyo, hivyo vyovyote itabidi tushinde ili kusafisha njia ya ubingwa kwa msimu huu.”
Kama atamzima Nasreddine Nabi wa Yanga kwenye mchezo huo, Gomes atakuwa ameutafuna mfupa mgumu uliowashinda watangulizi wake, Wabelgiji Sven Vandebrock na Patrick Aussems ambao mechi za kwanza dhidi ya vijana wa Jangwani waliwatesa kabla ya kutimka Msimbazi.
Sven aliyeinoa Simba tangu Desemba 2019 na kutimka Januari, mwaka huu hakuwahi kuifunga Yanga katika Ligi Kuu, kwani Januari 4, 2020 alibanwa na kutoka sare ya mabao 2-2 kabla ya kukubali kipigo cha 1-0 katika mechi iliyopigwa Machi 8, mwaka jana na katika mechi ya msimu huu ya mkondo wa kwanza walitoka sare ya 1-1.
Kwa upande wa Aussems aliyejiunga na Simba, Julai 2018 na kutimuliwa Desemba 2019, naye katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Yanga alishindwa kufurukuta baada ya kutoka suluhu katika mchezo uliofanyika Septemba 30, 2018, ila alishinda 1-0 kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Februari 16, 2019.
Kagera kazi wanayo
Katika hatua nyingine, Kocha Gomes anasema amepanga kutumia mchezo a 16 bora wa Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Kagera Sugar, kutengeneza morali ya wachezaji kabla ya mchezo wa watani, huku akisisitiza haachi kitu msimu huu.
Gomes alisema anaamini ushindi wa Jumamosi utawaweka pazuri kutetea taji hilo, lakini kuongeza morali kabla ya kuvaana na Yanga, na hata kwa michezo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akilisikilizia Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuwapanga na timu ipi katika hatua hiyo.
Simba ni miongoni mwa timu nane zilizotinga robo fainali ya Caf na huenda kesho Ijumaa ikajikuta mikononi mwa CR Belouizdad au MC Alger za Algeria au Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. “Tukishinda mechi hiyo ya ASFC utakuwa mwendelezo mzuri kwa matokeo upande wetu, jambo ambalo hata wachezaji watakuwa na hamu ya kufanya hivyo katika mechi ya Yanga ambao tupo nao katika mbio za ubingwa,” alisema Gomes.
Imeandikwa na Olipa Assa, Oliver Albert na Thobias Sebastian