Yanga yasitisha kambi Morocco, warejea Dar kwa mafungu
Yanga imesitisha ratiba ya kambi yao ya hapa Morocco na kutangaza rasmi wanarejea jijini Dar es Salaam kumalizia maandalizi yao.
Maamuzi hayo yametangazwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM mhandisi Hersi Said akisema zipo sababu mbalimbali zilizowapelekea kufanya maamuzi hayo.
Hersi amesema kumeguka kwa baadhi ya wachezaji wao ambao wanatakiwa kujiunga na timu za taifa ndio sababu ya kwanza ambapo jumla ya wachezaji wao nane kuitwa timu za taifa.
"Ukiangalia tumeona timu itameguka hivi karibuni wachezaji wetu wasiopungua nane wanatakiwa kwenda kujiunga na timu za taifa utaona hapo tutabaki na wachezaji wachache sana hapa," amesema Hersi
Hersi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ameongeza kwamba changamoto ya hali ya hewa haopa nchini Morocco huku pia wakikabiliwa na ratiba ya mchezo wa wiki ya mwananchi na ule wa hatua ya awali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pia zimewapelekea kuchukua uamuzi huo.
"Tangu tufike hapa tumekuwa na changamoto ya hali ya hewa hapa Marrakech sasa kuna joto kali sana sasa tumeona ni bora timu irudi nyumbani ambako hali yake ya hewa hata kama kutakuwa na joto lakini sio kama la huku.
"Tuna ratiba pia ya mechi ya wiki ya mwananchi ambayo itafanyika wiki hii mwishoni lakini pia mnajua kwamba tuna mechi ya hatua ya kwanza ya ligi ya mabingwa palepale nyumbani kwahiyo sababu hizi tumeiona ni bora maandalizi yetu yakafanyike palepale katika kumalizia.
"Tulikuwa tuondoke hapa tarehe 27 lakini kuondoka kwetu leo kunatufanya sasa kuondoka kwa makundi mawili kundi la kwanza litaondoka leo na kufika nyumbani Tanzania kesho Jumanne mchana na kundi lingine litaondoka siku chache zijazo.
"Kipo ambacho tumekipata katika kambi hii, walimu wamepata muda wa kukaa na wachezaji kwa pamoja lakini pia maandalizi yetu yamekuwa yakifanyika katika eneo ambalo linavifaa vya kutosha ambavyo vinaviwango bora, kwahiyo kambi yetu imekuwa ya mafanikio,"