Ishu ya kipa mpya Simba ipo hivi
Muktasari:
- Simba juzi iliwatambulisha wachezaji wake kwenye Uwanja wa Uhuru wakati wa kilele cha Tamasha la Simba Day ambapo staa huyo hakuwa mmoja kati ya wale waliotambulishwa.
ZIMETAJWA sababu za kwanini Simba haijamalizana na kipa Ahmed Issa “Bolo” kutoka JKU inayocheza Ligi Kuu ya Zanzibar licha ya kukaa naye kambini na kufanya mazoezi kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Simba juzi iliwatambulisha wachezaji wake kwenye Uwanja wa Uhuru wakati wa kilele cha Tamasha la Simba Day ambapo staa huyo hakuwa mmoja kati ya wale waliotambulishwa.
Ishu yake ipo hivi: Simba ilimtumia nauli kipa huyo kutoka Zanzibar na kutua Dar es Salaam lengo lilikuwa ni kumalizana naye na kumtangaza Simba Day, lakini maslahi ikawa kipengele ambacho kimelifanya jambo hilo lisikamilike pamoja na kufanya mazoezi na wenzake.
Chanzo kutoka Simba kikizungumza na Mwanaspoti kimesema kuwa:”Tulimhitaji Bolo ili kuja kuongeza nguvu kwa makipa waliopo ambao ni Hussein Abel na Mahamadou Kassali ambaye msimu wake wa kwanza uliyopita kuichezea Simba alimaliza na cleansheets 16.
“Ukiachana na hilo kocha Steve Barker alitaka kumuona ndiyo maana alifanya mazoezi na timu na alikuwa kambini, lakini bado suala hilo halijakamilika kwani mchezaji huyo bado ana mkataba na timu yake na tunaona sasa.”
Chanzo hicho kilisema lengo la kutaka kumsajili Bolo ni kutokana na changamoto ya majeraha anayopitia Yakoub Suleiman itakayomuweka nje kwa muda: “Yakoub bado anahitajika Simba ndiyo maana ametajwa ni miongoni mwa wachezaji wa Simba wa msimu unaoanza Agosti 14, 2026”.
Alipotafutwa Katibu wa JKU, Shadhil Khatibu alikiri kuwepo kwa mazungumzo ya klabu ya Simba kuhitaji huduma ya Bolo, lakini kuna vitu havijaenda sawa:”Makubaliano hajaenda sawa, mchezaji ana mkataba wa miaka miwili, ameongeza wiki tatu zilizopita, tayari mchezaji karejea Tanzania baada ya kuona kile alichokitarajia hakijawa.”
Ukiachana na hilo, taarifa mpya za kipa huyo zinadai yupo katika mazungumzo na Coastal Union, ili kwenda kuongeza nguvu baada ya kuondoka kwa Wilbol Maseke.