Prime
Kigogo Simba atabiri penalti dabi
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Crescentius Magori amesema Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga haina mnyonge na timu yoyote inaweza kupoteza, huku akisema mshindi atapatikana kwenye mikwaju ya penalti.
Mechi ya Ngao ya Jamii ambayo inahusisha Simba na Yanga itapigwa kesho kwenye Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar ukiwa ni ufunguzi rasmi wa msimu mpya wa ligi.
Magori amesema historia ya mechi hizo imekuwa ikionyesha kuwa kila upande huingia uwanjani ukiwa na nafasi ya kushinda, hivyo Simba haipaswi kudhani itakuwa na mchezo mwepesi dhidi ya Yanga pamoja na kwamba wapinzani wao hawajazoeana kwa kuwa wana wachezaji wengi wapya.
Amesema dabi hiyo huwa na presha yake na mara nyingi kiwango cha timu kinachonekana kabla ya mchezo hakiwezi kuwa kipimo cha matokeo yatakayopatikana uwanjani siku husika.
“Mechi ya Simba na Yanga haina mnyonge. Haijalishi timu moja inaonekana kuwa katika hali nzuri au mbaya kuelekea mchezo, dabi yenyewe huwa tofauti na mechi nyingine atakayekosea ameumia,” amesema Magori.
Magori pia amesema uwepo wa wachezaji wapya katika vikosi vya timu hizo unaweza kuathiri kiwango cha mechi, hasa kwa upande wa ufundi, kwa sababu baadhi yao bado watakuwa katika hatua za kuzoeana na wenzao pamoja na kuingia kwenye mazingira ya presha ya Dabi ya Kariakoo.
Amesema hali hiyo inaweza kufanya mchezo kuwa wa tahadhari zaidi, huku kila timu ikiepuka kufanya makosa ambayo yanaweza kumpa mpinzani nafasi ya kupata bao.
“Katika Ngao ya Jamii, mara nyingi huwezi kuona kiwango cha juu sana cha ufundi kwa sababu kuna wachezaji wapya ambao bado hawajazoeana vizuri na mazingira ya timu, hasa wanapokutana kwenye mchezo wenye presha kubwa kama huu,” amesema.
KUHUSU MABAO
Kutokana na hali hiyo, Magori amesema hatarajii kuona mabao mengi katika mchezo huo, akitabiri uwezekano mkubwa wa mshindi kupatikana kwa njia ya penalti endapo dakika 90 zitamalizika bila timu kutengeneza tofauti.
Amesema tahadhari zitakazochukuliwa na timu zote mbili pamoja na changamoto ya kuunganisha wachezaji wapya zinaweza kufanya mchezo uwe wa kusubiri kosa la mpinzani.
“Siwezi kutarajia mabao mengi kwenye mchezo huu. Kuna uwezekano mkubwa timu zote zikawa makini na mwisho wa siku mshindi akaamuliwa kwa penalti,” amesema.
SIMBA BADO INA NAFASI
Pamoja na kutabiri mchezo mgumu, Magori ameweka wazi kuwa anaamini Simba inaweza kuibuka na ushindi kutokana na msingi wa kikosi chake ambao kwa mtazamo wake, bado ni imara.
Amesema Simba ina faida ya kuwa na wachezaji waliokuwepo msimu uliopita ambao tayari wanaelewana na wanaifahamu mifumo ya timu, hivyo kocha anaweza kuwatumia kama msingi wakati akiwapa nafasi wachezaji wapya.
“Naamini Simba inaweza kushinda kwa sababu msingi wa kikosi bado upo. Kama wachezaji wapya watashindwa kuingia haraka kwenye mfumo, mwalimu bado anaweza kuwatumia wale waliokuwepo msimu uliopita ambao tayari wana muunganiko mzuri,” amesema Magori.
WATAKAOAMUA MECHI
Magori aliwataja Clatous Chama, Anicet Oura, Ellie Mpanzu, Libasse Gueye ni wachezaji ambao mchanganyiko wao unaipa Simba uwezo wa kupambana katika mchezo huo.
Kwa upande mwingine, Magori amesema Ngao ya Jamii haitakiwi kutazamwa kama mchezo wa kawaida, bali ni sehemu ya maandalizi ya Simba kuelekea msimu mpya ambao malengo yake ni makubwa.
Amesema Simba inahitaji kutumia mchezo huo kujipima kabla ya kuingia kwenye mashindano ya msimu mpya, huku akitaja malengo ya kufanya vizuri zaidi kimataifa pamoja na kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara.