Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga wanatoboa, hawataboi?

NI miujiza pekee itakayoweza kuifanya Yanga leo itabasamu. Ndivyo ukweli ulivyo, Julai sio mwezi mzuri hata kidogo kwa vijana wa Jangwani kila wanapokutana na watani wao wa jadi, Simba.

Wapo watakaobisha, lakini kwa kuwa siku zote namba huwa hazidanganyi, chungulia tu matokeo ya mechi za Kariakoo Derby zilizochezwa Julai, ndio utajua hali ilivyo.

Achana na matokeo ya michuano mingine kama ya Kombe la Shirikisho (ASFC, zamani FA) ama Kombe la Nyerere, Kombe la Hedex au ile ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) ambapo Yanga imekuwa na wakati mgumu mbele ya Simba, hapa tuzungumzie mechi za Ligi Kuu Bara.

Yanga wamepigika sana mbele ya Simba kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, kwani katika mechi zao sita walizokutana ndani ya Julai, Vijana wa Jangwani hawajawahi kushinda hata mara moja na Mwanaspoti linakuletea rekodi ya mechi zao kuona hali ilivyo;

JULAI 19, 1977

Hii ni siku ngumu na isiyosahaulika kwa mashabiki wa Jangwani, kwani ilikuwa Julai ya uchungu kwao, waliposhuhudia chama lao likipewa kipigo cha paka mwizi.

Ndio ilikuwa ni Julai yao ya kwanza kukutana na watani wao na ngoma ilipigwa Jumanne na Yanga kugaragazwa kwa mabao 6-0.

Kipigo hicho ni kama kiliitia gundu Yanga ndani ya Julai, kwani haijawahi kushinda katika Ligi ya Bara ndani ya mwezi huo.

Katika mchezo huo wa kwanza kwao ndani ya Julai, Simba ilikuwa ikilipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 na Yanga kwenye mechi yao iliyopigwa mwaka 1968.

Simba iliibuka na ushindi huo mnono kwa mabao ya Abdallah Kibadeni aliyepiga hat-trick, ambayo haijawahi kurudiwa tena katika Kariakoo Derby tangu wakati huo.

King Kibadeni alifunga mabao yake katika dakika za 10, 42 na 89, huku mabao mengine yakiwekwa kimiani na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ dk. 60 na 73, ilhali beki wa Yanga Selemani Sanga alijifunga dakika ya 20.


JULAI 14, 1984

Ilikuwa mechi ya jasho na damu, kila timu ilipambana kuhakikisha inapata matokeo. Simba ndio walianza kuwafunga watani wao kupitia kwa Zamoyoni Mogella dakika ya 17.

Yanga ziliwachukua dakika 22 tu kusawazisha makosa na kufanikiwa kurudisha bao dakika ya 39 mfungaji Abeid Mziba ‘Tekero’. Ikaisha 1-1.


JULAI 23, 1988

Yaani hata ile Simba mbovu zaidi katika historia ambayo ilikaribia kushuka daraja, iliifunga Yanga 2-1 mwezi Julai, ushindi ambao ndio uliowaokoa Wekundu kushuka daraja. Kwenye mechi hiyo iliyochezwa Julai 23, 1988, Yanga walihitaji japo sare ili kutwaa ubingwa. Wakapasuka.

Edward Chumila aliitanguliza Simba kwa bao, Issa Athuman kuisawazishia Yanga kabla ya John Makelele ‘Zigzag’ kuifungia Simba bao muhimu lililoibakisha kwenye Ligi katika dakika ya 58 na Yanga kuukosa ubingwa ulioenda kwa Coastal Union.


JULAI 17, 1993

Dua Said aliiduwaza Yanga kwa bao la dakika ya 69 katika mechi hii, bao ambalo lilidumu hadi dakika tisini na kuendeleza rekodi yao ya kuwanyanyasa Yanga kila wanapokutana ndani ya Julai.


JULAI 2, 1994

Mwaka 1994, nyota wa Yanga waliingia kwenye mgogoro wa makundi mawili yaliyokuwa yakivutana ya Yanga Asili na Yanga Kampuni na kuamua kuukomoa uongozi wa timu.

Walifungwa na Simba 4-1 kwa kinachosadikiwa kutekeleza mgomo huo, mabao ya Simba yalifungwa na George Masatu, Athuman China, Madaraka Selemani, Dua Saidi na bao lao la kufutia machozi lilifungwa na beki Constantine Kimanda.


JULAI 8, 2007

Mechi hiyo ilipigwa kwa dakika 120, ilimalizika kwa sare ya 1-1, wafungaji wakiwa ni Moses Odhiambo (penalti dk 2) na Yanga ni Said Maulid ‘SMG’ (dk. 55) baada ya sare hiyo, zilipigwa penalti Simba ikashinda kwa 5-4 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.


MICHUANO MINGINE

KOMBE LA KAGAME

Mshambuliaji Mghana wa Yanga, Kenneth Asamoah ni miongoni mwa wachezaji walioweka rekodi katika mechi ya watani zilizochezwa Julai akifunga bao dakika za jioni.

Ilikuwa ni fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame) iliyochezwa Julai, 10, 2011, Yanga walishinda bao 1-0. Asamoah alifunga bao hilo dakika ya 108 akimalizia krosi ya Rashid Gumbo mchezo uliochezwa kwa dakika 120.


JULAI 27, 2008

Achana na tukio la msimu huu ambapo Yanga aliondoka uwanjani kutokana na kuahirishiwa muda wa kucheza mechi siku ya mchezo ambapo wao ndio walikuwa wa kwanza kufika uwanjani huku watani zao Simba wakifuata na kukuta wapinzani wao wameondoka kwa kusisitiza wamefuata sheria za soka.

Kumbe sio mara yao ya kwanza, kwani Julai 27, 2008, Yanga ilisusa kabisa kwenda uwanjani kwa kile kilichoelezwa walikubaliana na Simba kuigomea mechi hiyo ya kusaka mshindi wa tatu wa michuano ya Kagame na Simba kupewa ushindi wa chee huku CECAFA ikiiadhibu kwa kosa hilo.


KOMBE LA HEDEX, JULAI 13, 1996

Timu hizo zilirudiana kwenye fainali ya michuano hii maarufu kama Hedex Cup, Uwanja wa Taifa. Dakika 90 ziliisha bila kupatikana mbabe baada ya kufungana bao 1-1, Simba ilipata tuta lililowekwa kimiani na kiungo fundi wake wa mpira, Hussein Marsha kisha Yanga ikachomoa kupitia Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’.


JULAI 2, 2005

Mashabiki wa Simba jijini Mwanza walitoka kwa shangwe kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, baada ya timu yao kuwashushia kipigo watani wao Yanga cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Gabriel ‘Batigol’ dakika ya 60, Mussa Hassan ‘Mgosi’ dakika 72.


KOMBE LA SHIRIKISHO, JULAI 12, 2020

Wala sio mbali ni mwaka jana tu, kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) watani hao wajadi walikutana Uwanja wa Benjamin Mkapa na goma likapigwa, baada ya tambo na kejeli nyingi zilizotokana na matokeo na mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu huo.

Mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya 2-2 Yanga ikichomoa, kisha bao la Bernard Morrison la friikiki likaizima Simba katika mechi ya marudiano ya ligi, hivyo kuwafanya vijana wa Jangwani kujiamini kwenye mchezo huo wa ASFC.

Hata hivyo, Julai kama kawaida ikawaendea kombo kwa kufumuliwa mabao 4-1. Ndio Yanga walipasuka 4-1 na Simba kwenda fainali kubeba ubingwa dhidi ya Namungo, huku Yanga waking’oka kwa aibu.

Katika mchezo huo dakika 15 za awali za kipindi cha kwanza Yanga walionekana kuanza vizuri, kabla ya kutepeta na kufungwa mabao na Mbrazil, Gerson Fraga, na mengine matatu kupitia Clatous Chama, Luis Miquissone na Mzamiru Yasin. Bao la Yanga liliwekwa kimiani na Feisal Salum ‘Fei Toto’.


WASIKIE HAWA

Licha ya Julai kuonekana kuwakalia vibaya Yanga, baadhi ya nyota wa zamani wa klabu hizo, bado wanaamini Yanga itatoboa Jumamosi kwa vile soka la Simba na Yanga huwa halitabiriki.

Winga aliyeanzia Msimbazi na kumalizia Jangwani, Said Maulid ‘SMG’ anasema anachokiamini kwenye mchezo wa watani wa jadi kupata matokeo ni bonasi zinazotolewa kwa wachezaji.

Alisema anatarajia mchezo mzuri kesho na timu itakayopewa hamasa nzuri ndiyo itakayoibuka kidedea, huku akiweka wazi kuwa suala la kuamini Julai Yanga haipati matokeo haina tofauti na ishu ya timu iliyo bora inaweza kufungwa na timu dhaifu.

Beki Bakar Malima aliyezitumikia klabu hizo te mbili alisema; “Simba ni bora na Yanga imeonyesha mabadiliko inacheza mpira wa pasi, hivyo mashabiki watarajie burudani nzuri kutoka pande zote mbili. Mechii hii haitabiriki.”