Simba yamvizia Mgunda kumrithi Mwalimu
Muktasari:
- Mwalimu alikuwa akicheza Simba, alikofunga mabao tisa na kutoa asisti moja msimu uliopita kwa mkopo kutoka klabu ya Wydad AC, ambako mkataba wake unasoma kuwa utamalizika Juni 30, 2029, huku Yanga ikimchukua kwa mkataba wa mwaka mmoja.
VIONGOZI wa Simba ni kama hawataki maneno, badala yake wameamua kufanya kwa vitendo baada ya mshambuliaji Selemani Mwalimu kwenda kujiunga na watani wao wa jadi, Yanga, hivyo wameanza kusaka mbadala wake kwa haraka sana.
Mwalimu alikuwa akicheza Simba, alikofunga mabao tisa na kutoa asisti moja msimu uliopita kwa mkopo kutoka klabu ya Wydad AC, ambako mkataba wake unasoma kuwa utamalizika Juni 30, 2029, huku Yanga ikimchukua kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka Simba kwamba viongozi hawakutaka kulaza damu, tayari wameanzisha mazungumzo na washambuliaji wa ndani. Miongoni mwa majina yanayotajwa ni mshambuliaji wa Mashujaa, Ismail Mgunda, ili awe mbadala wa nafasi hiyo kama mchezaji mzawa.
Mgunda msimu uliopita alifunga mabao mawili. Msimu wa 2024/25 alikuwa AS Vita ya Congo, huku msimu wa 2023/24 akiwa Singida BS akifunga mabao sita.
Chanzo hicho kimesema: “Dirisha la usajili bado halijafungwa, miongoni mwa wachezaji wazawa ambao tunazungumza nao ni Mgunda, lakini kunaweza kukawa na sapraizi kubwa ya hiyo.”
Simba, kama inahitaji kumalizana na Mgunda, itatakiwa kuvunja mkataba wa mwaka mmoja uliobaki wa mchezaji huyo na Mashujaa.
Kuhusu kuondoka kwa Mwalimu, wanahabari walipomuuliza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crecentius Magori, amesema: “Hakuna taharuki yoyote kuhusiana na Mwalimu na wala siyo jambo la kuliongelea.”