Yanga: Tunaanza na nyie, Jamhuri yasema liwalo na liwe
UTAMU wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 unazidi kukolea, ikiingia siku ya nne wakati Yanga watakaposhuka kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kukabiliana na Jamhuri iliyojeruhiwa na KVZ katika mechi ya kwanza ya Kundi C iliyopigwa juzi.
Jamhuri ya Pemba ilianza vibaya michuano ya msimu huu kwa kufumuliwa mabao 2-0 na leo itajiuliza mbele ya Yanga ambayo imetua Unguja jana kuanza kusaka taji la tatu la Mapinduzi tangu michuano hiyo ilipoasisiwa kwa mfumo wa sasa 2007.
Kabla ya pambano hilo litakaloanza saa 2:15 usiku, mapema jioni KVZ itaikaribisha Jamus FC ya Sudan Kusini kwenye mchezo wa Kundi C, huku wenyeji wakiongoza msimamo wa kundi baada ya ushindi mechi ya kwanza dhidi ya Jamhuri. Yanga imetua Unguja bila baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza waliopo timu za taifa zinazojiandaa na michuano ya Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 itakayofanyika kati ya Januari 13 na Februari 11, 2024 huko Ivory Coast.
Licha ya kuwakosa kina Diarra Djigui, Ibrahim Bacca, Bakar Mwamnyeto, Dickson Job, Mudathir Yahya na Stephane Aziz KI, bado Yanga ina mastaa kibao wanaotarajiwa kupewa nafasi ili kujiweka fiti baada ya kukosa nafasi kikosi cha kwanza cha Kocha Miguel Gamondi.
Gamondi raia wa Argentina anayeshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, alikaririwa anataka kutumia Mapinduzi kuwapa nafasi wachezaji wasiotumika mara kwa mara kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na hamu ya kuona majembe mapya.
Yanga imemsajili na kumtambulisha kiungo nyota Shekhan Ibrahim Khamis kutoka JKU ya Zanzibar na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Augustine Okrah anayedaiwa atatambulishwa kabla ya mechi hiyo.
Licha ya Jamhuri kuanza vibaya Mapinduzi na ikiwa haina mwenendo mzuri hata kwenye Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) ikishika nafasi ya 14 kati ya timu 16, bado inacheza soka la kuvutia kutokana na kuundwa na vijana wenye vipaji.
Hivyo, Yanga, haipaswi kuidharau hata kama imetoka kupoteza mechi iliyopita mbele ya KVZ, ili yasije yakawakuta kama ya watani wao Simba msimu uliopita walipoanza Mapinduzi kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mlandege iliyochukuliwa poa na ambao waliibuka mabingwa mwishoni.
Yanga inapaswa kuwa makini zaidi na wachezaji Hussein Abyubakr Ahmad, Abdulrahman Salum Omar, Suleiman Masoud na Khamis Khatib Hassan ambao kila mmoja amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu ya Zanzibar, kwani ni wasumbufu na wanaojua kuibeba timu uwanjani sambamba na kipa wao.
Hata hivyo, rekodi zinaibeba Yanga mbele ya Jamhuri kwenye Kombe la Mapinduzi, kwani hii sio mara ya kwanza kukutana, mwaka 2010 zilikutana na Jamhuri iliiduwaza Yanga kwa kuifunga bao 1-0, kabla ya Yanga kulipa kisasi 2017 kwa kuifumua mabao 6-0.
Mechi ya tatu ilipigwa 2019 na Yanga kushinda 3-1, kisha 2020 zilikutana tena na vijana wa Jangwani kushinda 2-0 na 2021 zilicheza na mara ya mwisho zikiwa kundi moja mchezo uliisha bila kufungana, hivyo kuifanya Jamhuri leo iwe na kazi ya kutaka kulipa kisasi.
Licha ya kazi ya kulipa kisasi, Jamhuri pia inajua ikipoteza mchezo huo itakuwa ni kama imeaga kwani itasaliwa na mechi dhidi ya Jamus inayoshiriki Mapinduzi kwa mara ya kwanza ikitoka kutwaa Kombe la FA ya Juba, Sudan Kusini.
Kwa hesabu zilivyo ni wazi Jamhuri italazimika kuzitumia vyema dakika 90 za pili kujitutumua mbele ya Yanga ambao nao sio rahisi kukubali kuaibika kwenye uwanja mpya wa Amaan unaotumiwa kwenye michuano hiyo inayoenda sambamba na miaka 60 ya sherehe za Mapinduzi Zanzibar
Kinachonogesha mchezo huo ni jinsi Yanga inavyocheza soka la kasi na kukaba kuanzia juu kitu kinachoweza kuisumbua Jamhuri, inayopaswa kuwa makini na mabeki wa pembeni wa Yanga hasa Yao Kouassi, Kibwana Shomary, Joyce Lomalisa sambamba na viungo washambuliaji wa timu hiyo.