Tanzania yacharazwa 4-1 kufuzu AFCON U-23
Muktasari:
- Katika mchezo huo wa hatua ya kwanza ya kufuzu AFCON U23, wenyeji Kenya walianza kwa kasi na kupata bao la mapema dakika ya pili kupitia Paul Osama, kabla ya Lawrence Okoth kuongeza bao la pili dakika ya 45+4.
TIMU ya Taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23, imejikuta kwenye kibarua kizito cha kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U23) mwaka 2027, baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 ugenini dhidi ya Kenya katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa leo Septemba 28, 2026, kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.
Katika mchezo huo wa hatua ya kwanza ya kufuzu AFCON U23, wenyeji Kenya walianza kwa kasi na kupata bao la mapema dakika ya pili kupitia Paul Osama, kabla ya Lawrence Okoth kuongeza bao la pili dakika ya 45+4.
Kipindi cha pili kilipoanza, Kevin Wangaya aliandika bao la tatu dakika ya 50, huku Kelly Madada akihitimisha ushindi huo kwa Kenya dakika ya 75 na kuacha safu ya ulinzi ya Tanzania ikiwa haina la kufanya huku lile moja la Tanzania likiwekwa kambani na Shekhan Khamis dakika ya 54 kwa mkwaju wa penalti.
Kipigo hicho kinaiweka Tanzania kwenye mtihani mkubwa kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa jijini Dar es Salaam, Oktoba 6, 2026.
Ili kufufua matumaini na kusonga mbele katika hatua inayofuata ambapo mshindi wa jumla atakutana na Ivory Coast, Tanzania inahitaji kupata ushindi wa mabao 3-0.
Fainali hizo zitakazofanyika nchini Misri, zina umuhimu mkubwa kwani ndiyo njia kuu ya kukata tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2028 itakayofanyika Los Angeles, Marekani, hivyo vijana wa Tanzania watalazimika kupambana nyumbani ili kupindua matokeo hayo mabaya.