Mamia washiriki mazishi ya Mzee Mpili
Muktasari:
- Mazishi ya Mzee Mpili yamefanyika leo Septemba 28, 2026, Ikwiriri Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, yakiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alexander Ngai.
MAMIA ya wananchi wameshiriki mazishi ya mwanachama na shabiki mkubwa wa Yanga SC, Haji Omari Ramadhan Mpili maarufu Mzee Mpili aliyefariki Septemba 27, 2026.
Mazishi ya Mzee Mpili yamefanyika leo Septemba 28, 2026, Ikwiriri Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, yakiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alexander Ngai.
Mbali na Ngai, viongozi wengine walioshiriki mazishi hayo ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine, Meneja wa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe na Msemaji wa Timu za Taifa za Tanzania, Haji Manara.
Msiba huo wa Mzee Mpili umegusa mamia ya wadau wa soka wakiwemo mashabiki wa Yanga, Simba na Azam waliosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda kushiriki mazishi hayo.
Akizungumza mara baada ya mazishi hayo, Ngai amesema msiba wa Mzee Mpili ni pigo kwa klabu ya Yanga, kutokana na maisha yake wakati wote kuwa tayari kuipigania klabu hiyo.
Ngai amesema kutambua nguvu ya Mzee Mpili, klabu hiyo imetoa ubani wa Sh1,100,000, lakini pia kundi la wanachama wa Black Card za uanachama wa klabu hiyo nalo likikabidhi Sh3,000,000.
"Mzee Mpili alikuwa na msemo wake kwamba ana watu na leo mazishi yake yameakisi msemo wake kwa huu umati wa watu waliokuja kumsindikiza," amesema Ngai na kuongeza.
"Klabu ya Yanga imepoteza mtu jasiri ambaye wakati wote alikuwa tayari kuipambania timu anayoipenda, maisha yake ni fundisho kubwa kwetu."
Naye Manara amesema sekta ya michezo imepoteza shabiki mcheshi ambaye alikuwa ameyaweka maisha yake kwa ajili ya klabu anayoishabikia.
"Mzee Mpili alikuwa wajina wangu, wakati wote alikuwa ana kauli zake za misimamo ya kuitetea Yanga, serikali kupitia Waziri wake wa michezo, Paul Makonda ametoa ubani wa Sh1 milioni na anawapa pole familia na mashabiki wa klabu ya Yanga," amesema Manara.