Yanga sasa yahamia kwa winga wa KMC
Muktasari:
- Mwijage amekamilisha usajili wa kujiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuachana na kikosi cha KMC FC ambacho msimu wa 2025-2026, imeshuka daraja, kufuatia kumaliza mkiani katika Ligi Kuu na pointi tisa.
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Klabu ya Yanga chini ya Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi inaendelea kufanya maboresho ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027 na sasa inadaiwa kuwa inafanya mazungumzo na kumsajili winga, Erick Mwijage.
Mwijage amekamilisha usajili wa kujiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuachana na kikosi cha KMC FC ambacho msimu wa 2025-2026, imeshuka daraja, kufuatia kumaliza mkiani katika Ligi Kuu na pointi tisa.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza mchezaji huyo tayari yupo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuonyesha kiwango bora msimu wa 2025-2026 lakini akiwa na ofa pia kutoka kwenye timu nyingine za ndani na nje ya nchi.
Mwijage ambaye alijiunga na KMC FC Agosti 14, 2025, baada ya kuachana na Kagera Sugar na kwa msimu wa 2025-2026, alihusika na mabao matatu ya Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga mawili na kuasisti moja kati ya mabao 16, yaliyofungwa na kikosi hicho.
Nyota huyo aliyewahi pia kuzichezea, Geita Gold na West Armenia ya Armenia, atakuwa ni mchezaji wa tano mzawa kusajiliwa na Yanga kwa msimu wa 2026-2027, baada ya winga, Juma Issa Abushiri kutokea Fountain Gate FC.
Wachezaji wengine waliosajiliwa na Yanga kwa msimu huu wa 2026-2027, ni beki wa kulia, Abdulnasir Assa ‘Gamal’, beki wa kati, Mohamed Mussa na mshambuliaji kinda, Hussein Juma Mihambo ambao wote wametokea kikosi cha maafande wa Mashujaa FC.