Amrouche, Dube wataja sifa tano zitakazombeba Mtasingwa Kaizer Chiefs
Muktasari:
- Mbali na hilo, kocha huyo ametaja sifa tatu za Mtasingwa kuwa ana uwezo mzuri wa kupiga pasi, kubadilisha mchezo na kimo kizuri, huku Prince Dube akibainisha nidhamu na kuleta uwiano katika eneo la kiungo ndiyo silaha kubwa aliyonayo.
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Adel Amrouche mwenye uraia wa Ubelgiji huku akiwa na asili ya Algeria, amemfananisha kiungo mpya wa Kaizer Chiefs, Adolf Mtasingwa Bitegeko, na kiungo nyota wa Ufaransa, Paul Pogba, baada ya mabingwa hao wa Soweto kumsajili kutoka Azam FC.
Mbali na hilo, kocha huyo ametaja sifa tatu za Mtasingwa kuwa ana uwezo mzuri wa kupiga pasi, kubadilisha mchezo na kimo kizuri, huku Prince Dube akibainisha nidhamu na kuleta uwiano katika eneo la kiungo ndiyo silaha kubwa aliyonayo.
Kaizer Chiefs imethibitisha kumsajili Mtasingwa mwenye umri wa miaka 27 kutoka Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili, huku ikiwa na kipengele cha kuongeza msimu mmoja zaidi.
Hatua hiyo imekuja wakati kiungo Thabo Cele akiwa kwenye hatua za mwisho za kuondoka katika klabu hiyo. Mtasingwa, ambaye anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kuichezea Kaizer Chiefs, anaingia klabuni hapo akiwa na uzoefu mkubwa.
Kiungo huyo ametumia miaka sita akicheza soka Scandinavia, ambako aliwahi kuzitumikia klabu za KR Reykjavík, Keflavík na Völsungur ÍF nchini Iceland, pia amekuwa na vipindi vya kucheza nchini Norway na Finland.
Tangu alipojiunga na Azam FC mwanzoni mwa mwaka 2024, Mtasingwa alikuwa mchezaji muhimu na kujijengea nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Amrouche, ambaye ndiye aliyempa Mtasingwa nafasi ya kwanza kucheza timu ya taifa wakati akiwa kocha wa Taifa Stars kuanzia Machi 4, 2023 hadi Januari 19, 2024, anaamini Kaizer Chiefs imemsajili mchezaji ambaye bado ana miaka bora zaidi mbele yake.
“Ana urefu mzuri, anacheza kwa urahisi na hafanyi mambo kuwa magumu akiwa uwanjani. Anaweza kuwa bora zaidi kama atapata mazingira ambayo ataaminiwa na kusimamiwa vizuri,” amesema Amrouche akizungumza na FARPost.
“Anafanana na Pogba. Adolf ana uwezo mzuri wa kupiga pasi. Anajua namna ya kubadilisha mchezo kwa kutumia pasi ndefu na fupi. Nilimuita kwenye timu ya taifa wakati akiwa hana klabu. Ni mtu mnyenyekevu sana na ana uwezo mkubwa wa kufanya makubwa zaidi ya yale aliyokwishaonyesha.”
Wakati huo huo, Prince Dube aliyewahi kucheza na Mtasingwa katika kikosi cha Azam FC msimu wa 2023-2024, amemwelezea kiungo huyo kama mchezaji mwenye nidhamu anayefaa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji na mwenye uwezo wa kuleta uwiano katika eneo la kiungo la Kaizer Chiefs.
“Yeye ni kiungo mkabaji wa aina yake ambaye anakaa mbele ya safu ya ulinzi na kulinda vizuri mabeki wa nyuma,” amesema Dube aliyetua Yanga msimu wa 2024-2025 akitokea Azam.
Mshambuliaji huyo ambaye hivi karibuni amehamia Hardrock FC ya Zimbabwe akitokea Yanga alipodumu misimu miwili, amesema: “Nadhani atafaa sana Kaizer Chiefs. Anahitaji muda wa kuzoea kwa sababu soka la Afrika Kusini lina kasi zaidi, lakini uwezo wake wa kupiga pasi ni mzuri sana.”
Dube anaamini uwezo wa Mtasingwa wa kuvunja mashambulizi ya wapinzani, kutunza mpira na kuamua kasi ya mchezo akiwa nyuma ya kiungo unaweza kuipa Chiefs utulivu ambao imeukosa katika misimu ya karibuni.
Kwa mtazamo wa kiufundi, Mtasingwa anaonekana kuwa usajili wa kimkakati kwa Kaizer Chiefs. Akiwa na umri wa miaka 27, anaingia katika kipindi kizuri cha kilele cha uwezo wake, akiwa na uzoefu wa kimataifa na anakwenda kuziba nafasi ambayo klabu hiyo imekuwa ikihitaji kuimarisha kwa muda mrefu.
Hata hivyo, kuna changamoto zinazoweza kujitokeza. Jeraha lilimzuia kucheza sehemu kubwa ya msimu wa 2025-2026 akiwa na kikosi cha Azam FC, pia kuhamia Afrika Kusini kutahitaji muda wa kuzoea mazingira.