Namungo kusuka upya kikosi
Muktasari:
- Namungo haikuwa na matokeo mazuri baada ya kusubiri mechi za mwisho kujihakikishia kubaki salama Ligi Kuu wakivuna pointi 34 na kumaliza Ligi Kuu nafasi ya 10.
UONGOZI wa Namungo umesema presha waliyokutana nayo msimu uliopita hawatarajii tena iwakute msimu ujao, wakitangaza kusuka upya kikosi kwa kutema nyota wanane na kuleta wapya 12 huku wakiitaja Yanga.
Namungo haikuwa na matokeo mazuri baada ya kusubiri mechi za mwisho kujihakikishia kubaki salama Ligi Kuu wakivuna pointi 34 na kumaliza Ligi Kuu nafasi ya 10.
Ligi Kuu msimu ujao inatarajia kuanza Agosti 14, ambapo timu hiyo ya mkoani Lindi inatarajia kuingia kambini Jumapili ya wiki hii huko jijini Dodoma kujiwinda na mashindano hayo ikianza na Yanga mchezo wa ufunguzi.
Hadi sasa Namungo imeshasajili nyota wapya wanane wakiwa ni Awesu Awesu, Lipapa Bakari, George Makang’a, Yahaya Kaniki, Rashid Gambo, Redemtus Mussa, Samson Casian na Gabriel Lusingi, huku wakisakwa wengine wanne kumaliza usajili.
Wakati ikimalizana na nyota hao, tayari imewaonesha mlango wa kutokea mastaa wake watano akiwamo Heritier Makambo, Ali Machupa, Shafih Maulid na Leny Kissu huku ikiendelea na mchujo wa wengine wanne.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa timu hiyo Ally Suleiman amekiri msimu uliopita kutokuwa mzuri kwao licha ya kubaki salama, akieleza kuwa tatizo lilikuwa kwa nyota wao haswa eneo la ushambuliaji.
Amesema kutokana na presha iliyotokea, wamejipanga msimu ujao kutorudia makosa na kwamba ripoti ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda wameifanyia kazi na matarajio yao ni kufanya vizuri.
“Ndio maana tumefanya usajili wa maana kwa kuangalia mapendekezo ya benchi la ufundi, hatutarajii presha ijirudie tena msimu ujao, tutakuja na nguvu mpya kwakuwa mipango inaenda vyema” amesema Suleiman.
Kuhusu maandalizi ya jumla kwa timu hiyo, kigogo huyo amesema kuwa wataanza kambi yao Dodoma ambapo wanaamini itakuwa sehemu nzuri ya kwao kujiweka vyema na mchezo dhidi ya Yanga.
“Tunajua Ligi yetu imepiga hatua, tunafahamu Yanga si timu ndogo ila kwakuwa tunaanza nao, lazima tujiandae kuwakabili na tuanze vyema msimu kwa ushindi, Namungo tutakuja kwa upya” ametamba bosi huyo.