Yanga Day ya mfano
Muktasari:
- Yanga Day ya mwaka huu ni mara ya nane linakwenda kufanyika tangu kuanza kwake mwaka 2019, huku klabu hiyo ikilitumia tamasha hilo kutoa burudani mbalimbali sambamba na kutambulisha kikosi cha msimu na benchi zima la ufundi.
KILELE cha tamasha la Yanga Day ni leo Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na hitimisho lake ni mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Yanga dhidi ya Les Aigles Du Congo.
Yanga Day ya mwaka huu ni mara ya nane linakwenda kufanyika tangu kuanza kwake mwaka 2019, huku klabu hiyo ikilitumia tamasha hilo kutoa burudani mbalimbali sambamba na kutambulisha kikosi cha msimu na benchi zima la ufundi.
Yamefanyika matamasha saba ya Yanga Day, lakini la mwaka huu, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesisitiza wamejipanga kuhakikisha mashabiki wanapata burudani ya kipekee tangu wanapoingia uwanjani, huku akibainisha litakuwa la mfano.
“Tukifungua mageti tunaanza burudani moja kwa moja. Kama kuna msimu ambao tumetamani tukate kiu cha wanachama wetu ni msimu huu wa Yanga Day. Tunataka liwe la mfano,” amesema.
Kamwe aliongeza: “Saa tano kamili asubuhi mageti ya Uwanja wa Uhuru yote yatafunguliwa kwa ajili ya kuwapokea mashabiki, wananchi na wanachama mbalimbali wa klabu yetu.”
Wakati upande wa viongozi wakijipanga kwa namna yao, wachezaji nao wameahidi burudani ya kutosha pindi watakapocheza mechi ya kirafiki.
Winga raia wa Uganda, Allan Okello ambaye anakwenda kushiriki wa mara ya kwanza Yanga Day kufuatia kutua kikosini hapo dirisha dogo la Januari 2025-2026, amesema: “Kwangu itakuwa ni mara yangu ya kwanza katika shughuli hii ya Yanga Day na nina furaha sana kuwepo.”
Nyota mpya raia wa Zambia aliyetua hivi karibuni, Albert Kangwanda, amewahimiza mashabiki kujitokeza kutoa sapoti ya hali ya juu kwa timu yao.
“Njooni kwa wingi kutusapoti. Itakuwa ni mara yangu ya kwanza, nimekuwa nikitazama hii na nina msisimko mkubwa kuwepo,” amesema.
Kwa upande wake, mshambuliaji Peter Shalulile ambaye ni mara ya kwanza akiwa ametua akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, amesema: “Njooni mfurahie Yanga Day na muwe na wakati mzuri.”